Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akiongea na baadhi ya Viongozi wa
mashirikisho ya wasanii wa filamu na Muziki kuhusu urasimishaji wa kazi za
wasanii wa Filamu na Mziki jijini Dar es Salaam (jana). (Picha na Benjamin Sawe
wa WHVUM)
Na
Concilia Niyibitanga- WHVUM
Serikali imeamua kuweka mfumo rasmi
utakaowawezesha Wasanii wa Filamu na Muziki nchini kunufaika na
kazi wanazozibuni na kuzitengeneza.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na Viongozi wa Mashirikisho
ya Wasanii wa Filamu na Muziki.
Dkt. Mukangara amesema kuwa Serikali
imesikia kilio cha Wasanii kwa kuirasimisha Sekta ya Filamu na Muziki ili
kuondokana na kilio cha muda mrefu cha Wasanii kutonufaika na jasho
lao.
Amesema kuwa Serikali itatumia mfumo
wa kuziwekea kazi hizo stampu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo
zitakuwa na usalama kwa nia ya kuondokana na uzalisha na udurufishaji ovyo wa
kazi hizo na kazi hizo zitawekewa ‘bar code’ kwa wepesi wa
ufuatiliaji.
Urasimisaji huu unaotarajia kuanza
rasmi Januari, 2013 utawezesha wasanii kukopesheka ili kupata mitaji
itakayowawezesha kutengeneza kazi bora na zenye viwango na
zitakazoweza kuingia katika soko la ushindani. Ameeleza Dkt.
Mukangara.
Amesema kuwa kwa sasa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Wizara ya Fedha; na Wizara ya Viwanda na
Biashara zinaweka katika mfumo wa kielektroniki taratibu zinazowezesha
utekelezaji wa mfumo huu kuwa rahisi.
Aidha, Dkt. Mukangara ametoa wito kwa
kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha kero ya Wasanii
kuibiwa na kutofaidika na kazi zao inaondoka na kuwataka vijana kujipanga vizuri
ili kuitumia fursa hii na hata katika siku za usoni waweze kuwa na
Saccos za vijana katika tasnia ya filamu na muziki na waweze kukopesheka
kupitia Mfuko wa Vijana.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la
Sanaa za Ufundi, Bw. Adrian Nyangamalle ameipongeza Serikali kwa hatua ya
kuirasimisha Sekta ya Filamu na Muziki na kuiomba Serikali kuangalia uwezekano
pia wa kurasimisha Sanaa za Ufundi ambazo zinaonekana kusahaulika
katika mfumo huo.
Bw. Nyangamalle amesema kuwa katika
Wasanii milioni 9 nchini, takribani Wasanii milioni 4 ni Wasanii wa Ufundi,
hivyo ni changamoto kwa Serikali hususan Wizara yenye dhamana na Sekta hiyo
kuona umuhimu wa kurasimisha kazi za Sanaa za Ufundi.
No comments:
Post a Comment