RAIS mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika sherehe za utoaji wa tuzo za wanamichezo bora Tanzania kesho kwenye
ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Abbas Pinto amesema katika
Mkutano na Waandishi wa Habari mchana huu, ukumbi wa City Sports Lounge, Mtaa wa
Samora, Dar es Salaam kwamba, wamemchangua Mwinyi kwa sababu alikuwa ana mchango
mkubwa katika sekta ya michezo enzi zake, akiwa Ikulu tangu 1985 hadi 1995
alipomuachia Benjamin William Mkapa.
Pinto amesema kwamba
maandalizi ya sherehe hizo yamekamilika na anawashukuru sana wadhamini wa tuzo
hizo, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa mchango wao mkubwa.
Katika tuzo hizo, kiungo wa
kimataifa wa Rwanda, Haruna Fadhil Hakizimana Niyonzima wa Yanga, atachuana na
Kipre Tchetche wa Ivory Coast anayechezea Azam FC na Mganda Emmanuel Okwi wa
Simba kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa mwaka wa kigeni.
Kwa upande wa wanasoka
wazalendo, tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka inawaniwa na John Bocco, Aggrey
Morris, wote wa Azam na Juma Kaseja wa Simba, wakati kwa wachezaji wa Tanzania
wanaocheza nje wanaoshindana ni Henry Joseph wa Kongsvinger ya Norway na Mbwana
Samatta wa Tout Puissant Mazembe ya DRC.
Kwa upande wa wanawake, Sophia
Mwasikili anayecheza Uturuki, anashindana na Asha Rashid ‘Mwalala’, Mwanahamisi
Omary wote wa Mburahati Queens, Fatuma Mustapha wa Sayari na Eto’o Mlenzi wa
JKT.
No comments:
Post a Comment