Tuesday, June 26, 2012

Pinda Ole wenu' wauza unga'

WAZIRI Mkuu, Mizengo  Pinda ametangaza kiama kwa vigogo wa dawa za kulevya na kuwataka watafute kazi nyingine za kufanya vinginevyo siku za kukamatwa kwao zinahesabika.Pinda alisema hayoleo jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya.
Alisema tatizo la dawa za kulevya bado linazidi kuwa kubwa , licha ya juhudi zinazofanywa na vyombo vya dola katika kuwakamata.
Alisema kutoka na hali hiyo, Serikali iko katika mchakato wa kuanzisha chombo huru kitakachokuwa na uwezo wa hali ya juu ya kupambana na dawa za kulevya.
“ Ole wenu mnaoendelea kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ni suala la muda tu , tumejipanga na tutawakamata tu,” alisema alisema Pinda katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi.
Alisema biashara ya dawa za kulevya inakithiri kwa sababu ya tamaa ya baadhi ya watu kutaka  utajiri bila ya kufanya kazi halali.
Aidha waziri mkuu huyo pia, alizungumzia pia tatizo la bangi ambapo alisema, matumizi yakebangi yanaendelea kuwa makubwa kutokana na kulimwa kwa wingi katika baadhi ya mikoa.
“ Nawataka viongozi wa mikoa inayolima bangi kudhibiti kilimo hicho ili wananchi wajishughulishe na kilimo cha mazao ya chakula na biashara yenye kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema.
Pinda alisikitishwa na matukio yaliyoanza kujitokeza ya baadhi ya  wanawake kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“ Kama wanawake tunaowategemea katika kujenga maadili ya vijana nao wanakamatwa basi tatizo hili sasa ni kubwa na tunatakiwa kujipanga zaidi kulidhibiti,” alisema Pinda.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema urefu wa mipaka ya nchi yetu na kukithiri kwa rushwa miongoni mwa watendaji wa Serikali  ni changamoto inayoikabili Serikali katika kupambana na biashara hiyo.
Alisema licha ya changamoto hizo, serikali imejipanga kuendelea kupambana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kadiri ya uwezo wake wote.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishina wa Tume ya Kuratibu na kudhibiti wa Dawa za Kulevya, Aida Tesha alisema,  tangu Januari hadi Mei mwaka huu, jumla ya kilogramu 234 za dawa aina ya Heroine zilikamatwa.
“ Kiasi hicho ni kikubwa kukamatwa katika kipindi hicho cha miezi mitano, zamani kiasi kama hicho kilikamatwa katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu,” alisema Tesha.
Alisema ongezeko la kukamatwa kwa wahusika wa dawa za kulevya kumetokana na ushirikiano wanaoutoa wananchi kwa Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment