Friday, January 31, 2014

Wafanyabiashara Bukoba wakerwa na kodi wanazotozwa na Jeshi la Zima moto



Na Theonestina Juma
 BAADHI ya Wafanyabiashara wa mjini Bukoba wameitaka serikali kufuta kodi wanaozotozwa na Jeshi la Zimamoto kutokana na wao huduma wanazotoa ni kama majeshi mengine nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakizungumza na Naibu Waziri wa fedha,  Adam Malima katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Kagera mjini Bukoba.
“Unakuta kila mwezi Jeshi la zima moto linazunguka katika maeneo ya biashara zetu kukusanya kodi ambazo hatuzijui ni kwa ajili ya nini, wao hawana tofauti na majeshi mengine zaidi ya sita wanazotoa huduma kwetu bure, mbona Jeshi la polisi wanatulinda na mali zetu bila kututoza kodi”alisema mfanyabiashara, Jemsi Mwanga.
 Mwanga alienda  mbali zaidi kwa  kwa kuhoji kuwa huenda Jeshi la Wananchi (JWT) ambao wanajukumu kubwa la kulinda mipaka yetu wakianza kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara hali itakuwaje kwao?
Kuhusu mashine ya EFD wafanyabiashara hao waliitaka Serikali kuwaacha wajinunulie mashine yao kokote wanakojua na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)wawauzie kadi (line) kama ilivyo kwa upande wa simu za kiganjani.
“Tunaomba serikali iwache wafanyabiashara wanunue mashine za EFD wenyewe halafu TRA wawauzie line kama ilivyo kwenye simu, na si kuwalazimisha wafanyabiashara wanunue mashine hizo ambazo bei yake ni ghali”alisema Remigius maafuru mjini hapa kwa jina la Dkt. Remmy.
Hata hivyo, kwa upande wa Naibu Waziri, Malima akizungumzia juu ya kodi za Jeshi la Zima moto, alisema wao wana ‘theory’ yake ambayo wao wameiweka lakini hata wao katika baraza la Mawaziri wamekuwa wakihoji hilo ambapo hata hivyo utoaji huduma zao kwa jamii iko tofauti na majeshi mengingine.
Alisema”Nawambieni wazi hili la asuala la Jeshi la ZimaMoto hata sisi kwenye baraza la Mawaziri tulihoji, hii kodi  ni ya nini? Inakwenda wapi? Mpaka sasa hata bado tunasubiri majibu lakini kaeni mkijua kuwa kila Jeshi lina utaratibu wake”
Alisema hata yeye binafsi suala hilo la zimamoto linamsumbua, kwani hajui tozo hizo  ni kwa ajili ya nini kwani hata kwa wakulima, wafanyabishara wadogo  na  wa wakati wote wanalalamikia hilo tozo.
Hata hivyo, Naibu huyo aligeuka kuwa mbogo baada ya Remigius kutoa pendekezo la serikali kuondoa tozo za kusafirisha fedha nje ya nchi pindi  mfanyabiashara kwenda kununua bidhaa nje ya nchi kwani ni miongoni mwa sababu ya bidhaa kupanda bei na hivyo kumuumiza mlaji.
Alisema kamwe haiwezekani na wala serikali haiweze kuondoa tozo hilo na wasije wakafikiria kuwa iko siku serikali itaondoa tozo hiyo.
“Hivi kuna nchi yoyote ambayo inasafisha fedha zake kwenda nchi nyingine bila kutoza ushuru, haiwezekani”alisema.
Awali  Kamishina wa TRA Taifa,Patrick  Kasera akizungumzia umuhimu wa mashine ya EFD alisema kuwa ni kumwezesha mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za mauzo na biashara zake, ambapo asilimia kubwa ya wafanyabiashara wengi ambao hawasimamii katika biashara zao wamekuwa wakiibiwa pasipokujua ni kiasi gani wanachoibiwa.
Halikadhalika alisema tatizo kubwa kwa Watanzania ni kumbu kumbu  ambapo hasara yake ni kukadiriwa  kipato chake kutokana na biashara yake  na matokeo yake huona kuwa anaonewa na TRA bila kuwa na uthibitisho.
Alisema “Kazi ya mashine hizo ni kutunza kumbukumbu vizuri na kukuwezesha kulipa kodi stahili na anayeona anaonewa hata ona hilo tena, kwani watu wengine wanafilisika bila kujua kama wao wenyewe hawasimamii biashara zao, lakini kwa kupitia TFD huweza kubaini hata kama hatakuwepo kwenye biashara zake”alisema.    
Alisema mashine za EFD zinamwezesha kila mtu kulipa kodi vizuri  bila kufilisika kwani atapewa makadirio ambayo  anaweza kuyamudu tofauti na hapo aawali ambapo mtu alikadiriwa tu kodi kumbe kiasi hicho kilikuwa ni kikubwa tofauti  na uwezo wake.
Mwisho.

   


Wanafunzi 14 tu waripoti sekondari ya kaigara



Na Theonestina Juma, Bukoba
WANAFUNZI 14 kati ya 175 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika shule ya sekondari ya Kaigara Wilayani Muleba ndiyo wamesharipoti shuleni, tangu shule zifunguliwe Januari 13, mwaka huu.
Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa shule hiyo, Bw. Sadru Majid wakati akizungumza  kwenye mkutano wa wazazi uliofanyika shuleni hapo.
Alisema chanzo cha wanafunzi hao wachache kuripoti ni  kutokana na baadhi ya wazazi wao kutokuwa na fedha za kuwalipia mahitaji mbali mbali yanayohitajika shuleni hapo kama vifaa vya shule.
Alisema “wazazi wengi wanalalamika kuwa hawana fedha kwa ajili ya kuwalipia watoto wao mahitaji mbali mbali za shule hivyo, hadi tunaanza mwaka wa masomo ni watoto 14 tu ndiyo wamesharipoti kati ya watoto 175 waliopangiwa katika shule hii”
Hata hivyo, baadhi ya wazazi wakizungumza katika mkutano huo walidai kuwa wameshindwa kuwapeleka watoto wao shuleni kutokana na kuwepo kwa michango mingi inayohitajiwa shuleni hapo.
Pia walidai kuwa kushindwa kwa mitihani ya kidato cha pili kwa baadhi ya wanafunzi ni miongoni mwa chanzo cha watoto kuacha shule na kunawakatisha tamaa kwa kuhofia kuharibu fedha zao huku watoto nao wakijiingiza katika shughuli zingine kama usafirishaji wa abiria kwa kutumia baiskeli na uvuvi.
Hata hivyo kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya MUleba, Bw. Lembris Kipuyo amewataka wazazi na walezi wa watoto wao kuwapeleka watoto shuleni mara moja hata kama hawana fedha za kuwalipia ada na vifaa vinavyohitajika shuleni hapo.
“Alisema Wazazi na walezi wa watoto ambao hawajariporiti shuleni, wahakikishe watoto wao wanaripoti shuleni mara moja, kwani huko watapewa maelekezo namna ya kuwalipia watoto wao vifaa vya shule, hata kama hawana fedha kwa  wakati huu”alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Halikadhalika amewataka Madiwani na watendaji wa kata husika kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia agizo hilo ili kuwabaini wazazi na walezi watakaobainika kukiuka agizo hilo wachukuliwe hatua za kisheria

Kagasheki:- Mtu asiye raia wa nchi akipewa madaraka makubwa ni kitanzi



Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la BUkoba mjini (CCM), Balozi Khamis Kagasheki amesema kwa sasa ameanza kuongopa kwa mtu ambaye si raia wa nchi akaomba uraia akapewa na madaraka makubwa  kuwa ni kitanzi.
 Balozi Kagasheki ambaye ni Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini alisema hayo hivi karibuni wakati akiwahutubia mamia ya wakazi wa mjini Bukoba ambapo kwa sasa anaendelea na mikutano yake ya kukutana na viongozi mbali mbali  wanaotokana na (CCM)kuanzia ngazi ya nyumba kumi  kujadili masuala mbali mbali huku akihimiza ushirikiano na kuondokana na makundi.
Alisema kutokana na hali hiyo” ndiyo maana katika nchi ya Marekani imo ndani ya sheria  mtu akiomba uraia wa Marekani Katiba yao iko sawa sawa, kwani  yako maeneo wanakuambia umepewa uraia wala si wa kuzaliwa  hivyo nchini humo  yapo maeneo huwezi ukagusa wala hata usiombe”.
“Hapa naweza kusema kuna mtu … huwezi kwenda katika nchi za watu wakakupa uraia … tena uraia wakupewa..wa kuomba .. .matokeo yake wewe unaanza sasa kuwahujumu, kuwaibia, kuwakejeli,kuwakiburi na kujaa jeuri  haiwezekani kama umepewa uraia unapaswa kufanya kazi na wale raia wa kuzaliwa  wa nchi hiyo nenda kwa utaratibu wa nchi hiyo”aliongeza 
Alisema yote yanafanyika kwa nia nzuri lakini mtu akipewa uraiwa anapaswa kufanya kazi vyema na waliozaliwa pale na si kufanya unavyotaka.
“Nenda kamulize hata leo kuhusu uraia wake umekaaje …. atakuwambia kuwa Waziri wa mambo ya ndani alitia mkono wake pale ndiyo maana nikapewa, umeshapewa sasa fanya vizuri …yote haya nayasema kwa nia nzuri sio kwa nia ubaya”alisema
Na kuhoji kuwa … “Wazungu wanasema, After role …if we can not speak for her…. yaani  baada ya yote hayo kama hawataisemea bchi yao ni nani atakaye isemea? Hayupo!
Alisema kutokana na hali hiyo, kwa sasa katika harakati zao za kuanza kujenga mji wa Bukoba kwa wale ambao wana nia ya kuvuruga wawapishe wakae pembeni .
“Mnajua kuna watu wengine wako humu mjini wana maneno sikuweza kuwataja majina yao … kwa sababu hata nikiwataja nitakuwa nimejiteremsha kwao… ndiyo sababu sitaki kuwataja “alisema.
Alisema kwa sasa wataanza kuaza kukaa vikao mbali mbali kwa nguvu zote ili kujenga kwa pamoja mji wao kwani Bukoba itajengwa na wana Bukoba wenyewe na kwamba katika vita iliokuwemo ndani ya Manipaa hiyo, aliyeishinda ni WanaBukoba na wala si Mbunge na  baadhi ya Madiwani.
Alisema upotevu wa sh. bilioni 2.5 zilizopotea ambazo zingewezesha kuleta mabadiliko makubwa ndani ya Manipaa hiyo hakuna anayeiona zaidi ya kuona ‘kamunobele’.
Alisema pamoja na  kuwepo kundi la watu wanaosema kuwa wapo watu wanaosema kuwa  Kagasheki ni mwiba anayewachuma yeye yuko na atakuna nao katika uchaguzi Mkuu unaoratajia kufanyika mwakani.
“Mimi hapa bado nilikuwa najifikiria, itakuwaje mwakani… kuna watu nasikia kuwa wanamwandaa mtu I mwingine aje awe Mbunge wa Jimbo hili, kwa kuwa wapo watu wanaojifanya wanajua siasa nawambieni fanyeni mtakavyofanya mtanikuta uwanjani”alisema”
Alisema waliosema kuwa Madiwani wa CCM wameungana na upizani kumwondoa meya hayo ni maneno ya kahawa, kwani walikuwa wakitetea haki ya wana Bukoba na hatua iliofikia ya kuwafukuza  madiwani wanane, hakuna chama chochote kinachoweza kufanya hivyo, kwani kuwafukuza wajue kuwa CCM kwa heri.
“Hata ngazi ya CCM haifanyi hivyo,  kuna vitu vya kuangalia… kwa watu wenye akili hawawezi kufanya  kama nyie mlivyoamua”alisema
Matamshi hayo ya Mbunge Kagasheki yanakuja siku chache baada ya Mdhibiti na Mkaguzi wa mahesabu ya serikali (CAG ), Bw. Ludovick Utouh kutoa taarifa ya uchunguzi maalum uliokuwa ukifanywa ndani ya Manispaa hiyo kufuatia ombi  la Waziri Mkuu  Mizengo Pinda kutokana na mvutano uliodumu kwa miaka miwili kati ya Mstahiki, Meya Dkt. Anatory Amani, Mbunge na baadhi ya Madiwani kupinga uendeshaji wa Manispaa hiyo katika utekelezaji wa miradi.
Katika ripoti ya CAG ulibaini kuwepo kwa ufisadi mkubwa uliofanywa katika Manispaa hiyo wakati wa utekelezaji wa miradi mbali mbali kama viwanja 5,000 ujenzi wa soko la kisasa, kituo cha kitega uchumi, kituo cha mabasi, kituo cha kuoshea magari.
Pia si mara ya kwanza Mbunge Kagasheki kusema kuwa ndiye alimpa urai Dkt. Amani ambaye inadaiwa kuwa ni raia wa nchini Uganda ambapo pia amekuwa akieleza kuwa yeye ndiye aliyemchonga hadi akafikia hatua ya kuwa Meya wa Manispaa hiyo, hali iliomfanya kukorofishana na aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa hiyo, Bw. Samuel Luangisa, ambapo Balozi Kagasheki amekuwa akikiri wazi kumkosea Bw. Luangisa.

Bibi kizee anusurika kuuawa kwa tuhuma ya uchawi



Na Theonestina Juma, Bukoba

BIBI kizee mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja anayedaiwa kuwa ni mkazi wa kata ya Karagabaine amenusurika kuuawa kwa kutuhumiwa ni mchawi baada ya kukutwa ndani ya chumba cha wanafunzi wa kike usiku wa manane.

Tukio hilo la aina aina yake ilivovutia hisia za wakzzi wengi wa Manispaa ya Bukoba limetokea  jana Januari 31, mwaka huu katika mtaa wa KambaMilembe kata ya Hamugembe mjini hapa.

Bibi huyo aliyekuwa amevaa kiguo cheusi kukuu kilichomfunika sehemu ya mauungo yake na kifuani inadaiwa kuwa aligunduliwa na baadhi ya wanafunzi wa vyuo vilivyoko katika jengo la Vijana mjini hapa.

Akizungumza na gazeti hili mwangalizi wa nyumba hiyo, aliyejulikana kwa jina la mama Halima, alisema yeye alipigia simu saa 8 usiku na wanafunzi hao kuwa wameingiliwa na mtu ndani ya chumba chao.

“Mimi nilipigiwa simu usiku wa manane, kuwa kuna mtu ameingia ndani ya chumba chao, kwa njia ya mazingara, niliwaambia kuwa kama wanauwezo wa kumlinda hadi asubuhi asiondoke wafanye hivyo, ili ukuche waweze kuangalia namna ya kufanya”alisema mama Halima.

Mama akizungumzia ni namna gani wanafunzi hao wa kike walivyogundua mtu kuwemo ndani ya chumba chao, alisema kuwa hiyo inatokana na wafunzi kuwa kila mmoja kuwa na imani yake kwani kuna wale wanaosali sana.

“Unajua kuna wengine wanaimani zao, na ni makabila mchanganyiko, lakini  kuna msichana mmoja ndiye alihisi kama ndani kuna upepo mzito sana, jambo alilolazimika kuwaamisha wenzake, kuwa ndani kuna kitu, waamuke waache taa, ndipo walipowasha taa walimkuta huyo bibi akiwa ameketi pembeni mwa vitanda vyao”alisema

Hata hivyo alisema kuwa, alipofika katika hosteli hiyo alfajiri na kumkuta bibi huyo, ambapo alikuwa hazungumzi, huku akiwazuia watu kuingia humo zaidi ya viongozi na watu ambao hakuweza kuwatilia shaka kama wanaweza kumdhuru bibi huyo.

Mama alisema alisema kuwa yeye ameishi katika nyumba hiyo kwa kipindi cha miaka 21 na hakuweza kutokea na tukio hilo, ambapo hili ndilo tukio la kwanza kutokea katika nyumba hiyo, ambayo wanafunzi hao walianza kuishi humo Agosti mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya watu walioshika dini waliitwa kuweza kusoma sala mbali mbali ili aweze kufunguka ambapo hata hivyo, bibi huyo hakuweza kuzungumza na hivyo uongozi wa mtaa, Bw. Athuman Yunus kwa kushirikiana na  uongozi wa kata  hiyo walilazimika kupiga simu kituo cha polisi.

Bi. Kizee huyo ambaye kwa wakati huo, alikuwa maefungiwa humo na mwangalizi wa nyumba hiyo, ambayo mumiliki wake anadaiwa kuwa anaishi Jijini Arusha  kwa kushirikiana na wanafunzi  kwa lengo la kuokoa maisha yake baada ya kundi la watu waliokuwepo eneo hilo la tukio kutaka atolewe nje ili aweze kuuawa.

Hata hivyo polisi walifika eneo la tukio, takriban saa 3. Asubuhi  na kufanikiwa kumwondoa kwenye nyumba hiyo pasipo kudhuriwa na umati huo na kumpeleka katika kituo cha polisi.

Pamoja na hayo, baadhi ya watu walidai kuwa Bi kizee huyo alionekana katika kituo cha mabasi cha Bugabo mjini hapa ilihali wengine wakidai kuwa alionekana katika baadhi ya viunga vya mjini hapa huku wengine wakidai kuwa ni kichaa.

Hata hivyo, jinsi gazeti hili lilivyomshuhudia bibi huyo, ni mtu ambaye haoneshio dalili ya kuwa na ukichaa wowote, kutokana na afya yake ilivyo na alivyokuwa msafi, huku akionekana mnene na mwenye siha njema.

Desemba 11,mwaka 2012 nyumba ya mwalimu  wa shule ya msingi Kashai, Bi. Benedetha Katabaro (56)  ilinusurika kuchomwa moto baada ya kutuhumiwa  mchawi na kuwahifadhi watoto sita kama msukule ambapo aliweza kuokolewa kwa mabomu ya machozi na risasi za moto.

Halikadhaka  Machi 13, mwaka 2012 watoto wawili wa familia moja waliokolews na Jeshi la polisi mjini hapa baada ya kuzingirwa na wananchi wakitaka kuwauawa kwa tuhuma za a tuhuma ya kutaka kumwiba mtoto mchanga kwa njia ya uchawi  katika mtaa wa Kashabo kata ya Hamugembe mjini hapa.

Sunday, January 26, 2014

Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia na watoto yalaani mauaji ya kikatili kwa wanawake Butiama

sophiasimbaHivi karibuni kumekuwa na taarifa za kutisha katika Wilaya ya Butiama mkoa wa Mara ambapo imearifiwa baadhi ya wanawake kuuawa kikatili kwa kukatwa vichwa. Sababu ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni pamoja na imani za kishirikina, uchu wa kumiliki mali, kulipiza visasi na kuendekeza hulka ya ukatili kwa kudhani kuwa mhusika anapata heshima yoyote katika jamii.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuwepo kwa mauaji hayo ya kikatili na inawataka wananchi kutoa ushirikiano thabiti ili kuhakikisha kuwa matukio hayo ya udhalimu YANAKOMA MARA MOJA.
Wizara inalaani vikali mauaji ya wanawake waliokatishwa maisha yao kutokana na kuuawa na watu wenye fikra potofu dhidi ya wanawake. Wizara inasisitiza kwamba  wanawake wanayo haki ya kuishi kama inavyosisitizwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977  inayotamka kuwa ‘Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake kwa Mujibu wa Sheria.’
Wakati mwingine wanawake wamekuwa wakikandamizwa katika jamii kutokana na tofauti za kimaumbile na hivyo kusababisha ukatili au mauaji. Wizara inaitaka jamii itambue kuwa wanawake wana haki ya kuthaminiwa utu wao na kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao unaweza kuhatarisha haki zao ikiwemo haki ya kuishi ambayo ndio haki kuu kuliko haki zote.
Vitendo vya mauaji ya kikatili wanavyofanyiwa wanawake wa wilaya ya Butiama ni jambo ambalo linasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanawake. Mauaji hayo yana wakosesha amani na utulivu na hivyo kuzorotesha ari yao katika shughuli za uzalishaji mali kwa wanawake wa  wilaya ya Butiama na Taifa kwa ujumla.  Mwananchi ambaye anawindwa kama mnyama kamwe hawezi akashiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi kwa kuogopa kuwa,  maisha yake yako hatarini.
Kwa kutambua hili Wizara inaagiza wadau wote kuiunga mkono Serikali katika kuhakikisha kwamba uhai wa wanawake wa Butiama na  kote nchini  unalindwa. Wananchi watambue kuwa tukio la mauaji dhidi ya mtu yeyote ni kinyume na haki za binadamu na ni kosa la jinai.
 Katika kipindi hiki cha majonzi, Wizara inatoa pole kwa familia ambazo zimeguswa na mauaji ya ndugu zao waliopoteza maisha,  Wizara inahimiza wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji wanafichuliwa na kuchukuliwa hatua ili kukomesha tabia hiyo.
Mwisho, Wizara  inapenda kuikumbusha jamii kuwa, mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake yanapingana na jitihada kubwa za Taifa katika kutekeleza  sheria za nchi na Mikataba ya Kimataifa na Kikanda kuhusu haki na usawa wa kijinsia,
  Aidha ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania wanaishi katika hali ya usalama, amani na utulivu.
Sophia M. Simba (Mb)
                    Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto
                                                                                                                                  23 Januari, 2014