Tuesday, June 26, 2012

Bilioni 300 zafichwa na vigogo nchini Uswizi

KITENGO cha Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kinachunguza Sh303.7 bilioni ambazo zinadaiwa kukutwa kwenye akaunti sita za Watanzania, wakiwamo wanasiasa, katika benki mbalimbali nchini Uswisi.Habari zilizopatikana hapa nchini kutoka ndani ya Interpol zimesema baadhi ya wanasiasa nchini na watu wengine ndiyo wanahusika na ufisadi huo kwa kuwa na akaunti zenye fedha nyingi nchini Uswisi.
Fedha hizo zimeelezwa ziliingizwa katika akaunti hizo na kampuni za uchimbaji mafuta na kampuni za uchimbaji madini, ambazo zinafanya kazi Tanzania.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba fedha hizo zipo katika akaunti sita tofauti, zinazomilikiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa.
Kiasi hicho cha fedha kilichofichwa Uswisi, kinatosha kuendesha Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitano, au kusaidia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuendesha shughuli zake kwa miaka miwili.
Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi moja.
"Wenzetu wa Uswisi wameeleza fedha hizo zimeingizwa na kampuni kadhaa ambazo zinahusika na mafuta pamoja na madini hapa nchini," kilidokeza chanzo hicho.
Mabilioni hayo yamebainika kufichwa wakati takwimu zilizotolewa na Umoja wa Taasisi za Kupambana na Rushwa barani Afrika ikiwamo Tanzania, zikionyesha kwamba Sh22 trilioni, zimekuwa zikitoroshwa nchini humo na kufichwa katika nchi za kigeni, ikiwamo Uswisi.
 Fedha hizo zimebainishwa na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB), iliyotolewa hivi karibuni, ikibainisha nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, na kiwango cha fedha zake zilizohifadhiwa huko.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hivi sasa inafuatilia suala hilo kwa mamlaka za Uswisi, ili kujua fedha hizo ziliko na nani anazimiliki.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine ambazo zina fedha nyingi katika benki za Uswisi ni Kenya (dola 857 milioni), Uganda (dola 159 milioni), Rwanda (dola 29.7 milioni) na Burundi dola 16.7 milioni.
Jumla ya fedha zilizoko katika benki za Uswisi kutoka nchi hizo nyingine za Afrika ni Faranga 1.53 trilioni za nchi hiyo na ripoti hiyo imeelezwa kuwa kuna msukumo wa kimataifa wa kuitaka nchi hiyo izitake benki zake, kubadilishana taarifa za wateja na serikali za kigeni.
Ripoti hiyo imekuja wakati pia Uswisi ikiwa na rekodi ya kuhifadhi mabilioni ya dola kutoka nchi za kigeni ikiwamo Afrika, kwani iliwahi pia kuhifadhi dola zaidi ya bilioni 1.5  za aliyekuwa Kiongozi wa Kijeshi wa Nigeria, Jenerali Sani Abacha na dikteta Mobutu Seseseko wa iliyokuwa Zaire.
Gavana azungumza
Akizungumzia ripoti hiyo, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Beno Ndulu (pichani) alisema uamuzi huo wa Uswisi wa kuanza kufungua milango utaiwezesha BoT kuwa na rekodi ya kiasi halali cha fedha zilizopo katika nchi hiyo.
Profesa Ndulu alifafanua kwamba katika siku za nyuma, Uswisi haikuwa imefungua milango kwa kutaja kiasi cha fedha za wateja wake walioweka fedha katika benki zake, hivyo ilikuwa vigumu kwa mamlaka za ndani kuweza kufanya uchunguzi.
"Ndiyo kwanza wameanza kufungua milango, sisi siku zote tulikuwa hatuwezi kujua nini kinaendelea. Lakini, angalau sasa tutaweza kujua na kuwa na rekodi baada ya uamuzi huo wa kufichua kiasi cha fedha kilichomo katika benki zake," alifafanua gavana.
Kiutaratibu, BoT inapaswa kuwa na rekodi ya fedha halali za Watanzania zilizopo nje ya nchi.
Kauli ya Takukuru
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alikaririwa na The Citizen hivi karibuni alisema kuwa ofisi yake ina taarifa kuhusu suala hilo na kwamba wanaanza mawasiliano na Serikali ya Uswisi kujua ukweli wake.
Dk Hoseah alisema taasisi hiyo inataka kujua jinsi gani fedha hizo ziliwekwa kwenye benki za Uswisi, watu waliohusika na namna uhamishaji wa fedha hizo ulivyofanyika.
"Tutakapogundua fedha hizo zimetoka wapi, tutafuata taratibu zinazohusika kuhakikisha zinarudi nchini," alisema Dk Hoseah na kuongeza: "Tutatumia sheria zilizopo katika nchi hizi."
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba hakutaka kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa yuko likizo, hivyo aulizwe msemaji wa Jeshi la Polisi.
Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso alisema hawajapata ripoti hiyo na kwamba atawaomba watu wa uchunguzi kumpatia, ili aweze kutoa taarifa.

No comments:

Post a Comment