MJUKUU BATROMEO BRUNO NA BIBI YAKE
EVANIA SEPHANGA WAKISHUKA KATIKA GARI LA POLISI BAADA YA KUFIKISHWA KITUO CHA
POLISI CHA KATI
Na Pardon Mbwate na
Felister Chubwa, wa Polisi Kigoma
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limefanikiwa kuwaokoa
watu watatu waliokuwa wamezingirwa na kundi la wananchi wakitaka kuwaua kwa
tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ushirikina.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma SSP Joseph Konyo,
aliwataja watu hao waliokolewa kuwa ni Evania Sephanga(50), mkazi wa wilaya ya
Kibondo, Bruno January(46), mkazi wa kijiji cha Nyamhoza na mtoto mmoja mwenye
umri wa miaka kumi na mkazi wa kijiji cha Nyamhoza Kigoma mjini ambaye jina lake
linahifadhiwa.
Kamanda Konyo amesema kuwa wiki iliyopita majira ya saa
tisa mchana, watu hao walizingirwa na kundi hilo kwa madai kuwa walimroga na
kumuua msichana mmoja aitwaye Faines Zawadi(20) mkazi wa kijiji hicho cha
Nyamhoza ambaye siku moja kabla ya kifo chake alionekana kama mtu
aliyechanganyikiwa na kuwa kama kichaa.
Alisema katika tukio hilo, bibi kizee mmoja ambaye
alikuwa mshirika wa kundi la waliodaiwa kuwa wachawi, alifanikiwa kutoroka
katika mazingira ya kutatanisha alipojifanya kuwa anakwenda kujisaidia.
Kamanda Konyo amemtaja bibi huyo aliyefanikiwa kutoroka
kuwa ni Bibi Editha Dosiyo mkazi wa kijiji hicho ambaye baadaye alipatikana na
kuhojiwa kabla ya kukabidhiwa kwa Idara ya ustawi wa jamii baada ya kuonekana
kuwa maisha yake yangekuwa hatarini.
Amesema baada ya Polisi kupata taarifa za tukio hilo,
walikimbia na kwenda kuwaokoa kutoka katika mikono ya kundi la wananchi lakini
wakiwa wameshaadhibu ingawa ilikuwa haijawa kwa kiasi kikubwa.
Habari zinasema kuwa, baadhi ya wananchi walipata
taarifa kutoka kwa mtoto aliyeokolewa akisema kuwa baadhi ya watoto waliofariki
kijijini hapo, akiwataja (majina tunayahifadhi) alikuwa akiwaona nyumbani kwao
nyakati za usiku wakiosha vyombo na baadaye kupewa chakula.
Siku ya tukio hilo, baadhi ya wananchi walisema kuwa
kabla ya bibi huyo kutoweka alimnong’oneza jambo mjukuu wake ili amfanyie
mareheme ikiwa ni pamoja na kumruka mara saba kisha bibi huyo alitoweka
akijifanya anakwenda kujisaidia.
Walisema mara baada ya bibi huyo kutoweka, mtoto huyo
wa kiume ambaye ni miongoni mwa waliozingirwa wakitaka kuuawa, aliamza
kutekeleza maagizo ya bibi huyo na alipomaliza kitendo cha kumruka kwa mara ya
saba, msichana yuyo ambaye alikuwa ni marehemu alizinduka na kuomba uji.
Wamesema msichana huyo ambaye alikuwa mfu, alipewa uji
na kunywa kisha akapelekwa hospitalini ambako hadi sasa hali yake inasemekana
kuwa inaendelea vizuri.
Hata hivyo Kamanda Konyo ametoa wito kwa wananchi
kuacha kuchukua sheria mkononi na badala yake watoe taarifa Polisi kwa kila
jambo wanaloliona kuwa linaweza kuleta uvunjifu wa amani ili hatua za haraka
zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Mwezi uliopita watu wawili mke na mume, waliuawa na
kundi la watu wenye hasira kisha miili yao kuchomwa kwa moto mkoani Kigoma baada
wa kutuhumiwa kuwa walikuwa ni wachawi
No comments:
Post a Comment