Bukoba
BAADA ya kuelezwa kuwa bei ya zao la kahawa kushuka katika soko la dunia wakulima wa zao mkoani Kagera wamesema hawapo tayari kuuza kahawa
yao kwa bei ya chini tofauti na iliyotangazwa kwenye mkutano mkuu wa makisio wa
Chama Kikuu cha Ushirika (KCU 1990 LTD).
Wakizungumza mjini Bukoba jana kwa nyakati
tofauti, wakulima hao walisema katika mkutano uliofanyika mwezi Aprili mwaka huu walitangaziwa bei
itakayotumika msimu huu, lakini wanashangaa kupelekewa barua ya kupunguzwa kwa
bei ya awali.
Walisema maandalizi ya kahawa yanachukua muda mrefu na
inaandaliwa kwa gharama kubwa, hivyo hawatakubaliana na sababu yoyote ya
kupunguza bei hiyo.
Mmoja wa wakulima hao, Burchard Lawrent, alisema bei
ya awali ilikuwa nafuu ndiyo maana wakakubaliana nayo na kwamba, wanapinga kauli
ya KCU kuwa tatizo hilo limetokana na bei ya kahawa kushuka soko la
dunia.
“Hatukubali. Kama kweli bei imeshuka soko la dunia mbona kampuni
binafsi wananunua kwa bei ya juu na hawajatangaza kupunguza, hilo soko
linaiathiri KCU pekee?” alihoji Lawrent.
Alisema kama KCU wataendelea
kug’ang’ania kununua kahawa kwa bei ya punguzo hawatauza, badala yake watauzia
kampuni binafsi.
Mwanzoni mwa Mei mwaka huu, KCU ilitangaza bei ya
kununulia kahawa ya wakulima msimu wa 2012/13, kahawa aina ya Robusta maganda
ilitangazwa kununuliwa kwa Sh1,360 kwa kilo, huku Arabica maganda ikitangazwa
Sh1,550.
Pia, Robusta safi ilitangazwa kununuliwa kwa Sh2,700 kwa kilo
na Sh3,200 kwa Arabica safi, huku kahawa ya Arabica organic iliyotangazwa
ilikuwa Sh3,800, Robusta ya Organic Sh3,650 na Robusta Organic ya Uganda
Sh1,700.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa Juni 19, mwaka huu na kusainiwa
na Meneja wa KCU, Vedasto Ngaiza na kusambazwa kwa vyama vyote vya ushirika vya
msingi, bei ya kahawa inapungua tofauti na iliyotangazwa awali kwa madai ya
kushuka kwa bei soko la dunia.
Barua hiyo inasema robusta ya maganda
imepungua kutoka Sh1,360 hadi Sh1,100 kwa kilo moja, robusta safi imepungua
kutoka Sh2,700 hadi Sh2,200.
Pia, barua hiyo inasema kahawa aina ya
Arabica maganda imepungua kutoka Sh3,200 hadi Sh2,600.
Chama hicho katika
msimu huu kinatarajia kukusanya tani 15,000 za kahawa kati ya makusanyo hayo
tani 1,750 zinatarajiwa kuwa kahawa safi.
No comments:
Post a Comment