MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imechukua jukumu la kufanya uchunguzi wa
umri wa muigizaji wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, anayekabiliwa
na kesi ya mauaji ya aliyekuwa muigizaji mwenzake Steven
Kanumba.
Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo jana kufuatia maombi
yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea mshtakiwa huyo
likiongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama.
Lulu ambaye anakabiliwa na kesi
hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu umri wake ulizua mvutano baina ya
mawakili wanaomtetea kwa upande mmoja na upande wa mashtaka(Jamhuri na pamoja na
Mahakama ya Kisutu kwa upande mwingine.
Mawakili wa mshtakiwa huyo
walidai kuwa mshtakiwa huyo bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18
kama hati ya mashtaka inavyosomeka na kwamba na maana hiyo anapaswa kushtakiwa
katika Mahakama ya Watoto (Juvenile Court).
Katika maombi hayo namba 46
ya mwaka 2012 yaliyowasilishwa Mahakama Kuu Mei 15 na mmoja wa mawakili wake,
Peter Kibatala walikuwa wakiiomba Mahakama Kuu itoe uamuzi kama Mahakama ya
Kisutu ina uwezo wa kuamua ufanyike uchunguzi wa umri halali wa msanii
huyo.
Waliiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu
haina uwezo huo, basi Mahakama Kuu yenyewe ifanye uchunguzi huo.
Akitoa
uamuzi wa maombi hayo jana Jaji Dk Fauzi Twaib alitengua na kutupilia mbali
uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi kukataa kuwa haina uwezo wa kushughulikia
maombi hayo, akisema kuwa mahakama hiyo ilikosea.
Akirejea uamuzi ya
Mahakama Kuu katika kesi mbalimbali zenye mazingira sawa na kesi hiyo, Jaji Dk,
Twaib alielezea kushangazwa kwake na Mahakama ya Kisutu kukataa maombi hayo
akisema kuwa ilikosea kwa kuwa ina mamlaka ya kuyashughulikia.
Jaji Dk
Twaib pia alikubaliana na hoja za upande wa Jamhuri walizozitoa wakati wa
usikilizwaji wa maombi hayo kuwa maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo
isivyo halali kwa mujibu wa sheria.
Alisema kifungu cha 100 (2) cha Sheria ya
mtoto ya mwaka 2009 kilichotumiwa na upande wa waombaji hakikustahili kwa kuwa
hakuna shauri liloko mbele ya mahakama hiyo kama kifungu hicho kinachoelekeza
bali shauri hilo liko Mahakama ya kisutu.
Kutokana na mazingira hayo Jaji
Dk Twaib alisema kuwa kuna njia mbili ambazo moja ni kuwasilisha upya maombi
hayo mahakamani hapo na ya pili ni mahakama hiyo kutumia mamlaka yake chini ya
Kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi kujiridhisha usahihi wa
uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.
Alisema kulingana na unyeti wa kesi hiyo
Mahakama Kuu kwa kutumia mamlaka yake na kwa kuzingatia kifungu cha 44 cha
Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi imeamua kufanya uchunguzi huo
yenyewe.
Alisisitiza kuwa kulingana na asili na unyeti wa mashtaka
yanayomkabili mwombaji, kutokuwa na uwezekano wa kupata dhamana na uharaka suala
lenyewe kuhitaji uchunguzi wa utata wa umri wake linahitaji uchunguzi wa
haraka.
Aliongeza kuwa kwa sababu hizo ameamua kutumia kifungu cha 44(1)
cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi, ili Mahakama hiyo iweze kufanya
uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo kama ilivyoombwa na
waombaji.
Kutokana na uamuzi huo pia Jaji Twaib kwa mamlaka ya mahakama
hiyo aliamuru mwenendo wa kesi hiyo katika Mahakam ya Kisutu usimame kusubiri
kumalizika kwa uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo.
Sambamba na uamuzi
huo Jaji Twaib aliamuru upande wa waombaji kuwasilisha mahakamani hapo hati ya
kiapo na nyaraka za ushahidi wa umri wa mteja wao kesho.
Pia aliauagiza
upande wa wajibu maombi (Jamhuri) kuwasilisha mahakamani ushahidi wowote kuunga
mkono msimamo wake Juni 20, 2012 na Juni 22, 2012 muombaji awasilishe majibu ya
ufafanuzi (Rejoinder) na akaamuru maombi hayo kusikilizwa Juni 25, 2012.
No comments:
Post a Comment