Tuesday, July 31, 2012

Waandishi wa habari zaidi 166 kutoka Kanda ya Ziwa wapata mafunzo ya Sensa ya watu na makazi

 Baadhi ya waandishi wa habari wa mikoa ya kanda ya ziwa wakiwa katika mafunzo ya Sensa ya watu na makazi katika hotel ya Annox jijini Mwanza,Afisa uhamasishaji wa Sensa nchini Said Amier akitoa mada katika mafunzo hayo.
 Waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini mafunzo ya Sensa ya watu na makazi yanayotolewa kwa muda wa siku mbili jijini Mwanza kwa waandishi wa habari mikoa ya kanda ya Ziwa.
 Mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Evarist Ndikilo wakati akifungua mafunzo ya Sensa ya watu na makazi kwa waandishi wa habari  mikoa ya kanda ya Ziwa,ambapo mkuu huyo aliwataka waandishi hao kuelimisha umma umuhimu wa Sensa ya watu na makazi na kuwaepusha na dhana ya kuhusisha zoezi la Sensa na masuala ya kisiasa na kidini. 
 Waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Ndikilo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya Sensa yanayofanyika kwa muda wa siku mbili.
Picha ya pamoja mkuu wa mkoa wa Mwanza na waandishi wa habari wa mkoa wa Mara wakati wa mafunzo hayo.

Wednesday, July 25, 2012

Denti aamua kujitia kitanzi baada ya kula ada na hawara yake badala ya kwenda


Na Theonestina Juma, Bukoba
MWANAFUNZI mmoja aliyekuwa akisoma kidato cha sita nchini Uganda amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba kwa madai kuwa amechoshwa na wazazi wake kufuatilia maisha yake.
Tukio hilo ambalo limethibitishwa na kamanda wa polisi Mkoani Kagera, Phillip Kalangi limetokea juzi katika mtaa wa Kashenye katika Manispaa ya Bukoba.
Mwanafunzi huyo aliyeamua kukatisha maisha yake kwa kujinyonga ametajwa kuwa ni Remmy Mulima (17) mkazi wa mjini hapa.
Imeelezwa kuwa hadi kufikia hatua ya mwanafunzi huyo kuchukua  jukumu la kujitia kitanzi, ni baada ya baba  mzazi yake ,Bw. Sosithenes Mulima  kumpatia sh. 500,000 kwa ajili ya ada ya shule, lakini hakuweza kwenda shule na badala yake aliamua kumchukua  hawara yake na kwenda naye Bunazi wilayani Missenyi.
Alisema wakiwa Bunazi msichana huyo alilazimika kupanga chumba maalum kwa ajili ya kufanya starehe na hawara yake  ambaye hakutajwa jina lake,  ambapo baba yake aliweza kupata taarifa hizo na kwenda Bunazi kumfualia.
Hata hivyo, kutokana na kujua kuwa amefanya kosa, mwanafunzi huyo alitaka kunywa sumu jambo ambalo baba yake alibaini na hivyo kumzuia.
Mwanafunzi huyo hakuweza kukata tamaa kwani waliporejea nyumbani kwao mjini hapa ndipo aliweza kuchukua jukumu la kuchukua kamba na kutundika juu ya miti wa mwembe na kisha kujinyonga huku akiacha ujumbe kwenye nguo yake  kuwa amechoshwa na wazazi wake kufutilia mambo yake.


Serikali imesahau zao la pareto

Wakulima wa pareto wakivuna pareto. Ili kuweka ubora wa zao hilo unatakiwa mkakati wa kushirikiana na serikali za vijiji kuandaa na kulitunza.

Rais Kikwete alivyoongoza wananchi maadhimisho siku ya Mashujaa nchini

Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo Juli 25, 2012 ameongoza Watanzania katika kuadhimisha siku ya Mashujaa Kitaifa katika Bustani ya Mnazi Mmoja Dar es salaam.
Zifuatazo ni taswira ya hafla hiyo ya kila mwaka
PICHA NA IKULU


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wakati alipowasili kwenye uwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo Julai 25, 2012 kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, akiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo, Julai 25, 2012 kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, leo Julai 25, 2012. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Rais Dkt. Jakaya Kikwete, akiweka Ngao  na Mkuki kwenye Mnara wa Mashujaa, wakati wa maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo Julai 25, 2012. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Kutoka (kushoto) Rais Dkt. Jakaya Kikwete, Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi,  Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho....., Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Said Meck Sadiq,  wakiwa katika viwanja vya Mnazi  Mmoja wakihudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, leo Julai 25, 2012. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Rais Dkt. Jakaya Kikwete, akisalimiana na baadhi ya wazee waliopigana vita mbalimbali vya ukombozi wa nchi ya Tanzania, waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo Julai 25, 2012. Picha na Muhidin Sufiani-OMR

Timu ya wanawake ya Marekani yaichabanga Ufaransa mabo 4-2

Bukoba
 HATIMAYE kipenga cha mchezo wa olimpiki kimepulizwa leo jioni ambapo timu nne ya wananwake wameingia dimbani.
Katika mechi nne zilizomalizika muda si mrefu, timu ya wanawake ya Marekani imeichabanga timu ya Ufaransa mabao 4-2.
 Halikadhalika timu nyingine ya Japan nayo imetoka kifua mbele kwa kuifunga timu ya Canada mabao 2-1. Muda mfupi ujao timu nne zinatarajiwa kushuka dimbani kuwania point tatu muhimu.
Ambapo usiku huu timu mbili kutoka Afrika zinatarajiwa kushuka uwanjani.Timu hizo ni pamoja na Cameroon na Brazil, Afrika Kusini na Sweden. Kila la heri timu za wanawake kutoka bara la Afrika.

Monday, July 23, 2012

Wanachi wa mgodi wa Butiama wanuia kuishtaki serikali

Augustine Mgendi
BUHEMBA

WANANCHI vijiji Vitatu wanaozungukwa na Mgodi wa Buhemba  wilaya ya Butiama mkoani Mara wamesema kuwa wanakusudia kuishitaki Serikali ya Tanzania katika Taasisi za Umoja wa Mataifa zinazohusika na haki za binadamu  ikiwa ni shinikizo la kulipwa fidia ya shilingi Bilioni 30.

Mbali na kusudio hilo la kuelekea umoja wa Mataifa lakini pia wananchi hao wamesema kuwa wanakusudia kumuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete kumueleza madhara yaliyosababishwa na Mgodi huo ambao ulidaiwa kumilikiwa na Serikali kupitia Kampuni ya Meremeta. 

Wananchi hao kutoka vijiji vya Tarani,Biatika na Magunga huku wakiomba Wabunge kuungana na kutoipitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini had hapo Serikali itakapo wafidia.   

Akiongea na waandishi habari katika eneo hilo la Buhemba,Diwani wa kata ya Buhemba Boniphace Masero amesema kuwa Mgodi huo umeachia athari kubwa kutokana na machimbo yaliyoachwa kuleta athari kubwa huku Ardhi yao ikiwa haina rutuba kutokana na Kemikali zilizomwagwa katika eneo hilo

Amesema athari zingine zilizoletwa na Mgodi huo ni pamoja na Shule iliyokuwa katika eneo hilo kubomolewa lakini walishindwa kuijenga kama walivyokuwa wameahidi wahuska hao wa mgodi huku miundombinu ya barabara nao ikiwa haifai kutumika.
“Huu Mgodi umetuachia madhara makubwa sana maana Mashimo hayakufukiwa,Milima inaleta uchafuzi wa Mazingira,shule iliyokuwa imejengwa hapa ilibomolewa,Nyumba zikabomoka kutokana na Baruti za mgodi,katika hili sisi tunakusudia kumuona Rais ili tumueleze haya Manyanyaso tunayoyapata” alisema diwani huyo

Diwani Masero ameongeza kuwa athari nyingine ni pamoja na baadhi nyumba za wakazi wa eneo hilo kubomoka kutokana na baruti zilizokuwa zikipigwa katika Mgodi huo lakini mpaka sasa hawajalipwa fidia na hivyo wanawaomba Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoipitisha Bajeti ya wizara ya Nishati na Madini mpaka walipwe fidia yao

Aidha Pasta wa Kanisa la Anglikana Samweli Nyakarungu alisema kuwa mgodi huo wa Buhemba ulikuwa ni Mgodi wa kitapeli ambapo wahusika hao wamechuma raslimali za Taifa na kushindwa kufanya shughuli za Maendeleo katika Jamii. 

Pasta Nyakarungu alisema kuwa mbali na wawekezaji hao wa Kitapeli kuiba mali ya Watanzania lakini pia wamesababisha madhara makubwa kwa jamii ya Buhemba kwa kushindwa kujenga miundombinu ya barabara,kujenga shule kama inavyotakiwa.

Kutoka na adha hiyo Pasta huyo alisema kuwa Serikali imeshindwa kuwajali wananchi wake na hivyo wanawaomba Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoipitisha Wizara ya nishati na Madini mpaka hapo wananchi wa eneo hilo watakapopata fidia yao. 

  “Hawa wawekezaji mimi naona hawakuja hapa kwa lengo la kumsaidia mtu wa Buhemba huu Mgodi naona ulikuwa wa Kitapeli kabisa,wamechuma raslimali za Taifa na kushindwa kumsaidia mtu anayezungukwa na mgodi na hata kurekebisha miundombinu huska na hii inaonyesha jinsi Serikali isivyojali wananchi wake” alisema Pasta Nyakarungu

Naye Mwalimu mstaafu Sita Nyamhanga na bi Hadja Yasini walisema kuwa mgodi huo umewaachia matatizo makubwa ikilinganishwa walivyokuwa wameahidiwa wakati wanaanza uchimbaji katika mgodi huo.

  “Tunavyojua ni kwamba wawekezaji wanapowekeza eneo lolote lazima watu wanaozungukwa na Mgodi ule wanufaike lakini hapa Buhemba sisi wananchi ndiyo tumepat tabu kabisa kwani mpaka sasa hatuna shule,barabara inayopitika muda wote,eneo letu limebaki Jangwa huku wakina mama wanapata tabu kutafuta maji kutokana na vyanzo vingi vya maji kuchafuliwa na mgodi” alisema Mwalimu mstaafu huyo.

Kwa upande wake Bi Hadja Yasini alisema kuwa wanapata tabu hata kutafuta kuni kutokana na eneo kubwa la Buhemba kubaki Jangwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kulingana na adha hiyo Bi Hadja alisema kuwa ni vyema Waziri mwenye dhama huska akawasaidia watu wa Buhemba ili waweze kupata fidia zao kutokana na madhara waliyoyapata kutokana na mgodi huo.

Mgodi wa Buhemba ambao ulianza kuchimbwa mwaka 2002 ni moja ya mgodi ambao ulikuwa ni mkubwa hapa nchini ukielezwa kumilikiwa na Serikali na kufungwa mwaka 2006 huku ukiacha eneo hilo la Buhemba kupoteza rutuba yake

Wednesday, July 18, 2012

Ole wenu watakaobuni au kukadiria takwimu ya sensa-Massawe


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe afungua rasmi mafuzo ya wakufunzi wa sensa mkoani Kagera jana tarehe 17/07/2012 na kuwaasa wajumbe wa mafunzo hayo kuzingatia yote watakayofunzwa ili takwimu sahihi za sensa na makazi ziweze kupatikana kwa ajili ya maendweleo  ya mkoa wa Kagera.

Mratibu wa sensa mkoa wa Kagera akimkaribisha Mkuu wa Mkoa katika ufunguzinduzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Linas Night Club, alisema dhumuni kubwa la mafunzo hayo  ni kuwafundisha wajumbe hao kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Kagera ili watakapoiva wawe wakufunzi  wa makarani wa sensa kuanzia ngazi ya Tarafa.
Mkuu wa Mkoa katika hotuba yake aliwasistiza sana wajumbe wote ambao walitoka katika kila wilaya kuzingatia sana mafunzo hayo kwa kuhakikisha kila kitu watakachofunzwa wanakizingatia kwa umakini mkubwa ili kuwa na uelewa mkubwa  wa kwenda kuwafundisha makarani  kule kwenye tarafa.
Pia Mkuu wa Mkoa aliwaonya wakufunzi hao kutojihusisha na vitendo vya kubuni au kukadilia takwimu pale watakapokuwa wanakusanya takwimu kwani ni muhimu sana kupata tawimu sahihi  zitakazosaidia katika kupanga maendeleo ya taifa zima kwa miaka kumi ijayo. Vile vile alisistiza sana kuwa taarifa zote za sensa ni siri na hakutakuwa na mtu ambaye atatoa taarifa za kaya au za mtu binafsi zitakazoulizwa wakati wa sensa.
Wito; Mkuu wa Mkoa  pia alitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kuhesabiwa siku ya kuamkia tarehe 26/07/2012 kwa kila sehemu ya mwananchi atayokuwa amelala. Pia alitoa wito kwa Taasisi za dini, na Taaasisi mbalimbali zote mkoani Kagera  kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kujitokeza na kuhesabiwa. Mhe. Massawe alitoa angalizo kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote atakaye jaribu kuvuruga zoezi la sensa, hatua za kisheria zitachukuliwa mara moja.
Mafunzo hayo ya sensa Mkoani Kagera yanaendeshwa na wakufunzi kutoka ngazi ya Kitaifa, aidha mafunzo yanayotolewa ni juu ya kutambua maeneo ya sensa, namna ya kuuliza maswali, namna ya  kujaza madodoso pia mafunzo hayo yanafanyika kwa nadharia na vitendo na mwisho wa mafunzo hayo wakufunzi watafanya mtihani wa kujaribiwa kuona kama wameiva.
Imetolewa na:
Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa,
Kagera

Ajali ya meli yaua zaidi ya 285 Bahari ya Hindi Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiwa katika Eneo la Bandari akishuhudia kuletwa kwa majeruhi mbalimbali waliookolewa katika meli ya Star Gate iliozama  huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar na ikiwa na abiria 250.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Amer Kificho pamoja na mawaziri mbalimbali wakiwa katika Eneo la Bandari wakishuhudia kuletwa kwa majeruhi mbalimbali waliookolewa katika meli ya Star Gate iliozama  huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar na ikiwa na abiria 250.
-Majeruhi wakipatiwa Mablangeti kwa ajili ya kujihifadhi baada ya kuokolewa katika meli ya Star Gate iliozama  huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar na ikiwa na abiria 250.
Majeruhi alieokolewa katika meli ya Star Gate iliozama  huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar na ikiwa na abiria 250.
 
Wananchi wakiwa wamekusanyika eneo la Bandari mjini Zanzibar kuona ndugu zao waliookolewa wakiwa hai na waliofariki katika ajali hiyo[PICHA ZOTE NA
RAMADHAN OTHMAN IKULU]
Askari wa Vikosi mbalimbali wakiwa katika kazi ya Uokozi kwa Abiria waliokuwa katika Meli ya Star Gate ambayo iliozama katika ikiwa imebeba abiria 250 huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar.
 
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamad akiwa katika hali ya huzuni Baada ya kushiriki katika uokoaji na kuwaona Majeruhiwaliookolewa katika Meli iliozama ya Star Gate wakiteremka hapo Bandarini Zanzibar.
Abiria waliyookolewa kutoka katika meli iliozama ya Star Gate katika bahari ya Chumbe Zanzibar.PICHA ZOTE NA YUSSUF SIMAI-MAELEZO ZANZIBAR
Raia wa kigeni waliookolewa katika meli ya Star Gate iliozama  huko katika bahari ya Chumbe Zanzibar na ikiwa na abiria 250.

Nyoka mwenye miaka 209 mkongwe duniani anayepatikana Msitu wa Minziro kuanza kusakwa

Dkt.Felician Kilahama Mkurugenzi Mkuu wa Misitu na Nyuki nchini.
Na Theonestina Juma
KUWEPO kwa nyoka mwenye umri wa miaka 209 sasa katika msitu wa akiba ya serikali ya Minziro wilayani Missenyi, serikali imeazimia kuanza kumsaka kwa udi na uvumba .
Aidha kutokana na ukongwe wake duniani kote huenda akawa kivutio muhimu katika sekta ya utalii na hivyo kuifanya serikali kuanza kupiga mahebu yake ili kuweza kumnasa kirahisi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Misitu na nyuki nchini, Dkt. Felician Kilahama wakati akizungumza na waandishi wa habari  mjini Bukoba.
Dkt. Kilahama alisema nyoka huyo mwenye futi 47  anapatikana baada ya kuona viashiria ya mapito yake  yakiwa yameburuzwa buruzwa katika pori hilo, ambapo imekuwa vigumu sana kuonekana hadharani kutokana na kuishi kwenye mapango.
“Huyu nyoka lazima tumfanyie mahesabu, ya kumpata kirahisi, miaka 209…,sio mchezo…. ameweza kutambulika miaka baada ya kupima urefu wa mapito yake, kuna chatu na nyoka wenye mapembe pia…. “alisema Dkt. Kilahama.
Alisema licha ya kumfuata fuata nyoka ni jambo la hatari na inahatarisha maisha ya mtafiti hivyo lazima ifanyike uharaka wa kupandisha hadhi msitu huo wa akiba ili iwe hifadhi ya taifa ambapo utaweza kuboresha hata usimamizi wake, ambapo hata hivyo katika Kamati ya ushauri wa Mkoa Kagera (RCC) ulipitisha msitu huo upandishwe hadhi.
Nyoka huyo ambaye ni aina ya Giant Forest Cobra kichwa chake kina rangi nyekundu na sehemu ya kiwili wili ikiwa ni rangi ya kijani alianza kufanyiwa utafiti tangu mwaka 2000 baada ya kupatikana kwa taarifa kutoka kwa wenyeji wa maeneo hayo juu ya kuwepo kwa aina ya nyoka huyo katika msitu huo.
Kutokana na hali hiyo, ililazimu uongozi wa Halmashauri ya Missenyi, kupitia Maofisa wa Misitu mwaka 2010 kumtengeshea sindano katika mapito yake  kwa lengo la kuchukua damu yake, kwa ajili ya kupima  vina saba yake  iliyobainika kuwa na miaka zaidi ya 207 kwa mwaka huo.
Dkt. Kilahama alisema nyoka huyo atakuwa ni kivutio muhimu katika Mkoa wa Kagera iwapo atatafutwa na kupatikana  licha ya kuwa wanakabiliwa na tatizo la ukumbwa wa msitu huo ambao unajumla ya hekta 25,000 kwani  nyoka huyo amekuwa akihama hama katika harakati zake za mawindo.
Afisa Misitu wa Wilaya ya Missenyi, Bw. Wilbard Bayona alisema nyoka huyo anayo uwezo wa kuishi siku 68 bila kula chochote zaidi ya maji baada ya kumeza mnyama yeyote anayefanikiwa kumkamata.


Nyoka mwenye miaka 209 katika msitu wa Minziro anavyoinyima serikali usingizi

 Hapa baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa Kagera pamoja na Maafisa Maliasili wa Halmashauri zote za Mkoa huo wakiwa katika  mkutano na Mkurugenzi Mkuu wa Misitu na nyuki, Dkt. Felician Kilahama.
 Waandishi wa habari mkoa Kagera wakiwa kazini
 Sehemu ya wajumbe na waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Dkt. Kilahama
 Dkt. Kilahama akizungumza na waandishi wa habari wa Kagera leo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
 Kushoto ni Mkurugenzi wa Msitu nchini, Dkt. Kilahama na  kulia kwake ni Afisa Misitu ofisi ya  Mkuu wa mkoa Kagera, Bw. Jafari Omary
Sehemu ya wajumbe.

Tuesday, July 17, 2012

Ukiona vitu adimu kama hivi Rorya ujue kuna disko vumbi mahali

Mtu huyu alinaswa na kamera yetu katika kijiji cha Randa barabara ya Mika Shirati akisukuma baiskeli ikiwa imebeba pipa, speka pamoja na vifaa vya muziki, ndiyo mtindo wa Rorya kwani pipa hutumika badala ya sub woofa kwa ajili ya kuongeza sauti wakati wakupiga disko vumbi, ndugu yangu akili ni nywele kila mtu anazake.

Add caption

Thursday, July 12, 2012

Waandishi wa habari Kagera wahimizwa kuandika habari za uchumi

 Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza mafunzo ya siku nne juu ya namna ya kuandika habari za uchumi na biashara uliodhaminiwa na umoja wa vilabu vya habari nchini (UTPC)
 Wakiwa katika ziara ya mafunzo kwa vitendo


Katibu Tawala Msaidi wa Mkoa Kagera ambaye pia ni Afisa Uchumi, uzalishaji na biashara, Bw. Fikiri Kisimba akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani) waliohudhuria kwenye mafunzo ya siku nne namna ya kuandika habari za uchumi na biashara walipotembelea ofisini kwake leo.

 Katibu Mtendaji wa TCCIA Kagera , Bw. Kamugisha Rwiza akifurahia jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari (Hawamo pichani) ofisini kwake leo.
Kati kati ni Mkufunzi wa mafunzo hayo, Bw. Manaku Mbani ambaye pia ni Mhariri wa gazeti la Business Times na kulia kwake ni Bi. Ashura Jumapili mwandishi wa Tanzania Daima

Nawakumbuka ile mbaya

 Mumiliki wa blog hii, akiwa na rakifiki yake Helen Andrew
Mumiliki wa Blog hii, Bi. Theonestina Juma akiwa kazini kati kati ya pori la Nyakafandi Wilayani  Ngara.

Wednesday, July 11, 2012

Vodacom kutoa tuzo kwa waandishi wa mitandao za kijamii na tovuti