Na Theonestina Juma, Bukoba
MWANAFUNZI wa kike wa kidato cha pili katika shule ya
sekondari ya Kaagya, Advea Makanyaga (16) amekutwa akiwa ameuawa kikatili kwa
kunyongwa shingo, kuvunjwa taya la kulia na kubakwa na kisha mwili wake kutupwa
shimoni.
Habari zilizopatikana mjini hapa jana na kuthibitishwa na
Kamanda wa Polisi Mkoani Kagara, Phillip Kalangi tukio hilo lilitokea Juni 24,
mwaka huu majira ya jioni katika kitongoji cha Bishaka kijiji cha Mushoju
kata Kaagya tarafa ya Bugabo katika halmashauri
ya wilaya ya Bukoba.
Kamanda Kalangi alisema siku ya tukio mwanafunzi huyo ambaye
alikuwa akiishi na bibi yake Bi. Meriselina Bigira (53) alimpelekea chakula
mchungaji wao aliyejulikana kwa jina la Peter Mabara (25) katika eneo la machugani
nje kidogo na nyumbani kwao.
Alisema lakini kwa siku hiyo mtoto huyo hakuweza kurejea
nyumbani kama ilivyo kawaida yake, hivyo bibi yake kuanza kuingiliwa wasi wasi
na kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Kishanje Juni 25, mwaka huu ambapo
alianza kutafutwa.
Alisema katika utafutaji huo, mwanafunzi huyo alikutwa akiwa
ameuawa na mwili wake kutupwa kwenye korongo lililopo kwenye mbunga ya kuchungia
mifugo akiwa ametumbukizwa kwenye shimo kichwa chini na miguu juu huku jiwe
kubwa likiwa limemkandamiza kichwani.
Hata hivyo, kutokana na tukio hilo, mwili wa marehemu
ulipofanyiwa na uchunguzi na daktari ambaye kamanda hakuweza kusema ni wa hospitali
gani ulibaini amevunjwa taya la kulia na
shingo na pia alibakwa kabla ya kuuawa.
Alisema katika uchunguzi huo ulibaini pia marehemu alikuwa
na michumbuko yenye kutoa damu kwenye sehemu zake za siri, huku nguo chupi yake aliokuwa amevaa kwa wakati huo
ikiwa imechanwa pia ‘skin tight’aliokuwa amevaa ikiwa imepandishwa tumboni.
Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kuwa chanzo cha mauaji
hayo, ni kuwa mchungaji wao huyo, Bw.
Mabara alikuwa akimtaka kimapenzi mwanafunzi huyo lakini alikuwa akimkataa.
Mchungaji huyo ambaye amefanikiwa kufanya kazi ya kuchunga
ng’ombe katika familia hiyo kwa miaka miwili mfululizo hadi hivi sasa
alifanikiwa kukamatwa jana katika kituo cha mabasi cha Bukoba mjini akijaribu
kutoroka kwenda kwao Kahama.
Bw. Mabara anashikiliwa katika kituo kikuu cha Polisi mjini
hapa kwa mahojiano zaidi ambapo anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote
mara baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment