-
Hatua na vipengele muhimu katika kuomba
-
MKARIBISHE ROHO
MTAKATIFU. *Rum 8:26-27 *Yoh 14:16-17
Yesu alisema Roho Mtakatifu ni
msaidizi wetu. Atatusaidia na kutufundisha yote, kwa maana pasipo yeye, sisi
hatuwezi neno lolote. Na sisi peke yetu hatujui kuomba ipasavyo, bali yeye
(Roho) ajua kutuombea kwa Mungu kama vile Mungu apendavyo. Hivyo kabla ya kuanza
maombi au kusoma neno au ibada au safari au mitihani au kikao n.k. jifunze
kujikabidhi kwa Roho Mtakatifu, uombe msaada wake, akupe ufanisi/ubora katika
yote yakupasayo kufanya.
Tambua Utu wake, Uungu na Uweza
wake.
Jikabidhi katika Nguvu ya Uongozi
wake.
Tii kila Uongozi anaokupa.
FANYA
TOBA NA UTAKASO. *Isa 59:1-2, Yoh 9:31, 1Yoh 1:8-9,7
Sikio la
Bwana si zito kusikia wala mkono wake si mfupi kushindwa kututendea mambo
tumwombayo, bali maovu yetu ndiyo yanatufarakanisha na Mungu wetu. Mungu
hawasikii wenye dhambi. Hivyo chukua muda wa kutafakari na kuungama dhambi zako
mbele za Mungu na kuzitubu kwa kumaanisha kuziacha. Mungu ni mwaminifu
kutusamehe na kututakasa na uchafu wote. (Isa 1:18). Lakini, kabla hujafanya
toba yako binfsi;
(i) -
Kwanza, samehe wote waliokukosea, hata kama hawajaja
kukuomba
msamaha. Usipowasamehe waliokukosea, na Mungu
hataweza
kukusamehe wewe. (Math 6:12,14-15)
(ii) - Ndipo nawe ufanye toba
yako binafsi. Na Mungu atakusamehe kabisa.
Hata kama ni nyekundu sana, zitakuwa nyeupe sana. (Isa 1:18, Isa
43:25)
3. MSIFU, MUABUDU NA KUMSHUKURU
MUNGU. *Zab 147 na Zab 148
Msifu Bwana
kwa Matendo yake makuu, mwabudu Bwana kwa uzuri wake na kwa sifa zake.
Mwadhimishe Mungu kwa Tabia zake, wema wake, fadhili zake na baraka zake
mbalimbali anazotutendea. Sifa yako ikifika vizuri mbele za Mungu, ndipo atakuwa
tayari kukupa haja za moyo wako. Haja zetu zimefichwa nyuma ya mgomgo wa sifa.
Ndio maana Neno linasema;
‘Nawe
utajifurahisha kwa Bwana (kwa kumsifu, kumwabudu na kumshukuru), naye atakupa
haja za
moyo wako’ (Zab37:4).
Yesu
anatuonyesha mfano; angalia sentensi yake ya kwanza katika kuomba kwake imekuwa
“Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe.” (Math 6:9). Anaanza
maombi kwa kumsifu Mungu. Msifu Mungu kwa kuimba na kwa kunena/kusema/kuelezea.
Mungu anataka kusifiwa na kutukuzwa. Ukifanya sifa nzuri, ya kuufurahisha moyo
wake, atakupa hata na vile ambavyo hukutegemea/hukuomba.
4. MWELEZE MUNGU MAHITAJI NA
HOJA ZAKO. *Wafilipi 4:6-7,19 Isa 43:26
Mweleze Mungu zile hoja zilizokusukumwa kwenda kumwomba. Nenda mbele za
Mungu kama ‘kuhani’ (1Pet 2:9). Kwa unyenyekevu na heshima. Lakini kabla
ya kumweleza mahitaji yako binafsi;
(i) Kwanza
fanya ‘maombezi’ – ombea watu wengine; (1Tim 2:1-4)
Viongozi
mbalimbali na wenye mamlaka, watumishi wa Mungu, marafiki zako, wenye shida,
ndugu zako, nchi yako, shule yako, shirika lenu, ofisi yenu, chama chenu, n.k.
Usianze kujiombea mwenyewe tuu, zoea kuwatanguliza wengine.
(ii) Kisha fanya ‘maombi yako’–
ombea haja za moyo wako. (Math 7:7-11)
Mweleze
Mungu haja zako. Ongea na Mungu kwa uwazi na ukweli. Japo anazijua haja zetu,
lakini ameagiza kuwa tumwombe ndipo atafanya. ‘aombaye hupokea’ yaani;
asiyeomba, hapati. Mungu anasema tumpelekee hoja zenye nguvu (Isa 41:21). Omba
vitu vizuri na mambo makubwa ili upewe (pray for good things and big things)
5. FANYA MAOMBI YA VITA VYA
ROHONI. *Efe 6:10-13 *2Kor 10:3-5
Baada ya
kumwendea Mungu na kumweleza mahitaji yako, sasa simama kama ‘mfalme’, kwasababu
wewe ni ‘mfalme’ (Ufu 5:8), tumia mamlaka yako ya kifalme, ongea na hali/hitaji
ulilokuwa unaliombea, na kwa mamlaka, amuru iwe kama vile
ulivyoomba/unavyotamani. Ndio maana Bwana Yesu alipokabidhiwa mamlaka yote na
Mungu, naye akatukabidhi sisi (kanisa lake) “Tazama, nimewapa amri ya
kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui. Wala hakuna
kitakachowadhuru” (Luk 10:19, Yer 1:10, Yak 4:7). Tuma neno lenye mamlaka
katika hali/jambo ulilokuwa unaliombea, Amuru iwe vile ulivyokuwa unamwomba
Mungu iwe. Kemea kila roho ya shetani inayoweza kuwa inasababisha tatizo katika
swala lako.
6. OMBEA ULINZI JUU YA
ULIYOYAOMBEA. *Math 6:13a
Baada ya
kupiga vita vya kiroho, weka ulinzi katika yale uliyoyaombea, ili shetani na
mapepo yake wasiweze kuirudia hali/jambo/mtu yule uliyemkomboa kwa maombi ya
vita. Yesu alisema shetani akifukuzwa mahali, haendi mbali, anasubiri kuona kama
atapata upenyo wa kuparudia mahali pale alipokuwa kwanza. (Math 12:43-45).
Kwahiyo, usipoweka ulinzi, kuna uwezekano wa adui kurudi na kuliharibu zaidi
lile jambo uliloliombea na kulipata.
Kumbuka,
unapoomba vizuri, unapokea papo hapo (katika ulimwengu wa roho), lakini
udhihirisho wake katika ulimwengu wa mwili, unaweza kuchukua muda fulani. Hivyo
katika muda huo wa kusubiri, shetani anaweza akapita na kuzuia au kuharibu kile
unachokisubiri kidhihirike katika ulimwengu wa mwili. Ndio maana Yesu
alitufundisha kuombea ulinzi, “tuokoe na yule mwovu” (Math 6:13a). Weka
ulinzi juu ya mambo yako yote. Jengea wigo wa moto wa mbinguni (2Fal 6:16-17),
Yafunike kwa damu ya Yesu na agiza malaika walinzi walinde mambo yako masaa
yote. Omba hivyo kila siku. (Zab 34:7, Zab 91:9-11, Ebr 1:13-14)
MSIFU,
MWABUDU NA KUMSHUKURU MUNGU. *Math 6:13b
Yesu alianza
maombi kwa kumsifu Mungu na kumtukuza. Na akamaliza maombi yake kwa kumtukuza
Mungu tena. Akasema “kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu ni zako, sasa na hata
milele” akamaliza. Kwahiyo nawe kwa kumaliza maombi yako, msifu na
kumshukuru Mungu tena, kwa ukuu wake, uaminifu wake, na ahadi zake juu yetu.
Ndipo ufunge maombi yako.
MUHIMU: TUMIA
MAANDIKO KATIKA KUOMBA *Kol 3:16
-Katika kuomba kwako, mara zote tumia maandiko kumkumbusha Mungu ahadi
zake .(Isa 43:26). Mungu analiangalia neno lake ili alitimize. Sababu pekee
itakayomfanya Mungu akupe alichoomba, ni ili kulitimiza neno lake. Hivyo, baada
ya kumweleza unachohitaji (kwa ajili yako au kwa ajili ya mtu unayemwombea)
mpe Mungu andiko/neno lake
linalokupa wewe uhalali wa kuomba hicho kitu mbele zake na kupewa.
-Hata unapompinga
na kumkemea shetani, baada ya kutoa amri yako dhidi yake, shetani atasubiri
kusikia andiko/neno linalomnyima yeye uhalali wa kushika alichoshika. Ndio maana
Yesu alimshinda shetani kwa neno la Mungu. Alisema “imeandikwa” na shetani
akashindwa. “Nao wakmshinda (shetani) kwa damu ya Yesu na kwa Neno” (Ufu
12:11)
MBINU ZA KUKUSAIDIA KUOMBA VIZURI
KWA MUDA MREFU
1.
CHAGUA MAHALI PAZURI PA UTULIVU. *Mk 1:35
ili
uweze kuomba kwa utulivu na kwa umakini, chagua au tafuta mahali pazuri
patakapokupa
utulivu katika kuomba (concentration in prayer). Ndio maana Mungu
alipenda
kuongea na Musa juu ya mlima. (Kut 24:12-18). Hata Yesu alizoea kwenda
kuombea
mlimani, mahali palipo mbali na vurugu za watu, alipenda kwenda mlimani.
(Math
14:22-23). Tafuta mahali patulivu; chumbani, kanisani, mlimani (Math 6:5-6)
2.
CHAGUA MUDA MZURI. *Mhu 3:1,7
Ili
uweze kuomba kwa umakini mzuri, chagua muda mzuri ambao akili yako ma mwili
wako
viko fresh. Usilazimishe kuomba hata kama akili yako au mwili wako umechoka
sana. Kila jambo lina wakati wake. Kama umechoka sana, huo si muda wa kuomba,
bali wa kupumzika. Usilazimishe ratiba. ni bora upumzike ili baadaye uweze
kuomba vizuri baadaye. Usije ukajikuta unamkemea Yesu badala shetani. Penda
kuomba wakati una nguvu ya akili na mwili, ili uwe makini kuongea na Mungu kwa
akili timamu. Ndio maana Yesu alipenda kuamka alfajiri sana kwenda kuomba
mlimani. (Mk 1:35, Luka 4:42)
3. OMBA KATIKA ROHO (NENA KWA LUGHA). *Efe
6:18, Rum 8:26-27
Mbinu nyingine nzuri ya kuomba kwa muda mrefu na kwa ufanisi, ni kuomba
kwa Roho; yaani kuomba kwa kunena kwa lugha. Tunapoomba kwa akili za kibinadamu,
Mungu anasikia pia, lakini maombi yako yanakuwa na mipaka / limited kwasababu
akili ya mtu haijui kila kitu. Bali Roho wa Mungu anajua kila kitu. Naye hutupa
kipawa cha kuomba kwa lugha ya mbinguni iliyo bora zaidi. (Yuda 1:20, Mk
16:17, 1Kor 14:1-4, 15-16,7)
4.
OMBA KWA KUFUNGA WAKATI MWINGINE. *Math 6:16-18
Kufunga
kula kunasaidia kudhoofisha mwili, ili roho iwe makini zaidi kuongea na Mungu
kwa kina zaidi. Mwili huu siku zote haupendi kufanya mambo ya Mungu. Na mwili
ukiwa umeshiba, unakuwa na uchovu na uzito wa kufanya mambo ya kiroho. Mbinu
mojawapo ya kuudhibiti, ni kuunyima/kuupunguzia posho yake ya chakula. Mwili
ukidhoofika kiasi, roho yako inapata nguvu na upenyo mzuri zaidi (Zab 35:13).
Mashujaa wote wa imani walifunga na kuomba. Ndio maana Yesu anasema ‘mfungapo’
akimaanisha ratiba ya kufunga, ipo. Inasaidia.
5.
OMBA NA RAFIKI (PRAYER PARTNER). *Mhu 4:9-10
Neno la Mungu linasema, ni heri wawili kuliko mmoja. Kuna faida ya
kuomba pamoja na rafiki yako. Kwanza, mnapokuwa wawili au watatu, inaleta hamasa
na ari ya kuomba zaidi. Si rahisi kujisikia mvivu unapokuwa na waombaji wenzako.
Pili; nguvu ya kiroho inaongezeka. Neno linasema, mwombaji mmoja anafukuza adui
elfu moja, bali wakiwa wawili, wanafukuza (sio elfu mbili) bali elfu kumi!
Shangaa! (Kumb 32:20) Hiyo ni kanuni ya mbinguni/kanuni ya Ki-Mungu. Kadri
mnavyoongezeka, nguvu ya Mungu huongezeka.
Kwahiyo, wakati mwingine, omba na rafiki yako, unayemwamini, unayeweza
kumshirikisha mambo yako ya binafsi. Mashujaa wengi wa imani, walikuwa na
marafiki wa kiroho. (Prayer Partners). Kwa Mfano:- Math
17:1-9
Musa
- alikuwa na Joshua, Haruni na Huri
Eliya
- alikuwa na Elisha
Daniel
- alikuwa na Shadrack, Meshack na Abednego.
Yesu
- alikuwa na Petro, Yakobo na Yohana.
Paul
- alikuwa na Barnaba, Timotheo na Tito.
Wewe Je? Uko na nani katika urafiki wa kiroho?
Kama huna rafiki wa karibu wa kuomba naye, usikurupuke kujichaglia.
Tulia umwombe Mungu akupe mtu atakayekuwa wa msaada kwako. Mtu
mtakayefungamanishwa naye katika roho, hata kama mmetengana kijiografia, lakini
katika roho, mko na umoja mzuri wa imani. (Math
18:18-19)
6.
OMBA KATIKA MKAO UNAOKUPA UHURU NA NGUVU ZAIDI.
Katika
kuomba kwa muda mrefu, mkao uliouzoea utakusaidia kwenda mwendo mrefu. Yakupasa
kujua nguvu yako na udhaifu wako (strong point and weak point). Wakati wa
kuomba, epuka mikao inayokuchosha haraka na tumia mikao inayokua nguvu zaidi.
Kwa Mfano:- Ukiwa umechoka, usipende kuomba kwa kupiga magoti au kwa kuegemea
kitandani. Ni bora uombe ukiwa umesimama au unatembea tembea, ili kuepuka
usingizi na uchovu. Waombaji hodari wanaujua mikao inayowasaidia kuomba maombi
marefu. Wengine hawana mikao maalum, bali wakiwa katika maombi,
huwa wanabadilisha-badilisha mikao ili wasichoke. Hiyo ni mbinu nzuri
pia.
Mifano ya
Mashujaa wa imani;
Ibrahim
– aliomba kwa kusimama (Mwa 18:22)
Daniel
- aliomba kwa kupiga magoti (Dan 6:10)
Paul
- aliomba kwa kupiga magoti (Efe 3:14)
Yesu
- aliomba kwa kulala chini (Math 26:38-39)
Eliya
- aliomba kwa kukaa chini na
kuweka kichwa kati ya miguu (1Fal 18:42)
Mimi
- huwa napenda kuomba kwa kutembea tembea
Naweza
kumaliza kilomita nyingi chumbani kwangu
Nikitembea
huku nikiomba.
Wewe Je? Unaujua mkao wa nguvu? Kama hujui, Tafuta kujua.
OMBA
NA MUZIKI LAINI KWA KUMWABUDU MUNGU.
Muziki wa
kiroho, na wataratibu, unaweza kukutengenezea mazingira mazuri sana ya kuomba
kwa muda mrefu. Muziki wa kuabudu, unavuta uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee.
Neno linasema, waimbaji na wanamuziki walipoimba na muziki ukapigwa, nao wakawa
kama mtu mmoja, utukufu wa Mungu ukashuka na kulijaza lile hekalu hata makuhani
hawakuweza tena kuhudumu (2Nyak 5:12-14). Kule mbinguni, kila
malaika wa sifa, ana kinubi (zeze/gitaa). Elisha hakutoa unabii, mpaka mpiga
kinubi alipopiga kwa ustadi, ndipo mkono wa Bwana (Roho wa Mungu) alipokija juu
yake, naye akatabiri.
Najaribu kukuonyesha, kuna connection
kati ya muziki wa kiroho na utukufu wa Mungu. Kwahiyo, ukiweza kuomba huku
umeweka kanda au CD ya nyimbo za kiroho za taratibu, utapata (experience) hamasa
ya kiroho (motivation) na utasikia una nguvu ya kuomba kwa muda mrefu. Kama
unaweza, tengeneza kanda au CD maalum yenye nyimbo nzuri unazozipenda wewe, ili
uwe unaipiga wakati wa maombi. Utajikuta unaweza kuomba kwa muda mrefu na kwa
bubujiko zuri zaidi
Mwl. Mgisa
Mtebe,Bsc Economics
Mzumbe
University,+255 713 497
654
mgisamtebe@yahoo.com
No comments:
Post a Comment