Wednesday, June 6, 2012

TEMESA Kagera wahaha kusaka milioni 14 kurejesha kivuko cha Kyanyabasa


                                                  Na Theonestina Juma, Bukoba
MVUA zinazoendelea kunyesha mkoani hapa zimesomba kivuko cha Kyanyabasa na kukipeleka umbali wa kilomita nane hali iliosababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya Kata ya Bujugo na Kasharu katika halmashauri ya Bukoba.
Hayo yamebinika jana wakati Mwenyekiti wa halmashauri ya Bukoba, Kapteni Dauda Kateme akizungumza na BLOG HII  mjini hapa.
Bw. Kateme alisema tangu kivuko hicho kisombwe na maji, wananchi wa maeneo hayo hawana mawasiliano ya usafiri jambo lililolazimu baadhi ya wananchi wa maeneo hayo kutoa mitumbwi yao kufanya kazi ya kuvusha abiria kwa malipo ya sh. 500 huku magari yakitozwa sh. 4,000.
Alisema pamoja na kuwa eneo hilo ni mradi na ni mmoja  ya chanzo cha kuingizia mapato ya ndani halmashauri hiyo, lakini hadi sasa hawaambulii chochote ambapo hata magari ya halmashauri hiyo pia yanatozwa fedha hizo nawananchi hao wanaomiliki mitumbwi hizo.
Hata hivyo kwa upande wa  Meneja wa Wakala wa ufundi na umeme mkoani Kagera (TEMESA) Bw. Wilson Nyitwa akizungumzia suala hilo alisema kivuko  hicho kilisombwa na mvua Mei 18, mwaka huu saa 4 usiku kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mkoani hapa.
Alisema tangu mvua isombe kivuko hicho kutoka eneo hilo hadi kijiji cha Buteinamwa umbali wa kilomita nane, walijaribu kulivuta na kukirudisha  katika eneo lake la awali ambapo hadi hivi sasa inahitajika sh. milioni 14 kwa ajili kurejesha huduma hiyo.
Alisema pamoja na tatizo hilo pia mvua hiyo ilisababisha mrundikano wa magugu maji katika eneo hilo jambo ambalo liliwalazimu kusafisha takribani heka  mbili kuziondoa.
Alisema tayari tatizo hilo na ombi la milioni 14 wameshawasilisha makao makuu lakini bado wanasubiri majibu, kwani shida kubwa ni fedha hizo ambapo zikiingia tu kazi ya kuweka kamba na kurejesha huduma hiyo inaweza kuchukua siku mbili tu.
Hata hibvyo, kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Kagera, Kanali Fabian Massawe alisema atafuatilia suala hilo kwa akaribu ili kuweza kuangalia ni namna gani fedha hizo zinaweza kuharikishwa ili wananchi waweze kurejeshewa huduma hiyo haraka iwezekanavyo.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment