Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Fenella Mukangara kuomboleza kifo cha Mhariri
Mtendaji wa Gazeti la JamboLeo, Ndugu Willy Edward Ogunde kilitokea usiku wa
kuamkia jana, Jumapili, Juni 17, 2012 mjini Morogoro.
Katika salamu zake za rambirambi, Mheshimiwa Rais
Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha ghafla cha Ndugu
Willy Edward Ogunde ambaye amepoteza maisha akiwa bado kijana ingawa tayari
alikuwa amekwishakutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya habari
kutokana na umakini wake, uzingatiaji wa weledi kikamilifu na misingi mingine
mikuu ya uandishi wa habari.
“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa na huzuni nyingi kifo cha
ghafla cha Ndugu Willy Edward Ogunde ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea usiku wa
kuamkia jana, Jumapili, huko Morogoro ambako alikuwa amekwenda kikazi. Ndugu
Willy Edward Ogunde amepoteza maisha akiwa bado kijana sana hata kama ni kweli
katika muda mfupi wa maisha ametokea kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya
habari kwa mchango wake wa kudumisha weledi na misingi mingine mikuu ya uandishi
wa habari.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mheshimiwa
Waziri salamu za dhati ya moyo wangu za rambirambi kuomboleza kifo cha kijana
huyu wetu na mwanataaluma wako. Aidha, kupitia kwako nakuomba uniwasilishie
salamu zangu kwa wanataaluma wote wa tasnia ya habari nchini kwa kuondokewa na
mwenzao. Lakini zaidi, nakuomba unifikishe salamu zangu nyingi kwa wanafamilia,
ndugu na jamaa wa Marehemu Willy Edward Ogunde.”
“Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa kwa
sababu msiba wao ni msiba wangu pia. Naelewa machungu yao katika kipindi hiki
kigumu cha kufiwa na mpendwa wao. Nawaombea subira na uvulivu. Aidha, wajulishe
kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema
peponi roho ya Marehemu Will Edward Ogunde. Amina,” amesisitiza Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
IMETOLEWA
NA:
KURUGENZI
YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
18
Juni, 2012
DAR
ES SALAAM
No comments:
Post a Comment