Sunday, June 10, 2012

Hii ndiyo Bukoba tuitakayo


Bukoba
LICHA ya baadhi ya wafanyabiashara katika soko kuu la Bukoba kupinga kuvunjwa soko hilo na kujengwa la kisasa, Mbuge wa Jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki amewahakikishia kuwa mradi huo unatekelezwa ili kuharakisha maendeleo ya mji huo na kuwa hawezi kugeuka ahadi yake aliotoa kwao mwaka 2010.
Mbunge Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii alisema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi wa Manispaa ya Bukoba, katika viwanja vya Mashujaa mjini hapa, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu awe waziri Kamili mwaka huu.
Balozi Kagasheki, alisema pamoja na kupata malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara na wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuhusiana na uongozi wa Manispaa kutaka kuvunja soko hilo, na kujenga la kisasa, hawezi kupingana na mawazo hayo kutokana na hata yeye anahitaji mabadiliko katika mji huo na kwamba ujenzi wa soko aliahidi katika kampeni zake ya uchaguzi mwaka 2010.
‘Siwezi kugeuka maneno yangu, ujenzi wa soko nakumbuka suala hilo nilisema katika kampeni yangu katika mtaa wa Omukigusha, hata nyie mkanipigia makofi, hivyo ujenzi huo lazima ufanyike lengo ni kutaka kuleta mabadiliko na kuarakisha maendeleo katika Manispaa ya Bukoba”alisema.
“Kama mnataka kuthibitisha zaidi katafuteni mikanda ya video zangu za nyuma  za  kampeni kuhusiana na soko hili suala mtalipata”alisisitiza.
Alisema kabla ya kuanza ujenzi wa soko hilo, hakuna mfanyabiashara yeyote atakayeondoka ndani ya soko hilo mpaka wapatie maeneo mbadala kwa muda kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.
Alisema  walioko sokoni wote wataorodheshwa majina yao  ambapo yatapitiwa na uongozi wa soko hilo baadaye wataingia mkataba na halmashauri ya Manispaa ambapo soko likikamilika  wao ndiyo watakuwa wa kwanza kupewa nafasi ndani ya soko hilo.
Alisema suala la soko lisivunjwe kwake halina nafasi kwani katika soko hilo ni aibu tupu kutokana na nyakati za mvua baadhi ya wafanyabiashara wa nafaka hunyeshewa na hivyo kushindwa kufanya biashara zao kwa uhuru.
Alisema soko la Bukoba mjini linahitaji mabadaliko kwani ni la muda mrefu hata wakati akisoma elimu ya dini lilikuwepo ambapo kwa miji mingine tayari yameshajenga masoko ya kisasa tofauti na Bukoba pekee ndiyo bado.
Alisema kwa wale ambao hataki soko hilo lisivunjwe wawape mbadala wake, kama kweli Bukoba hauhitaji mabadaliko kwa ajili ya kuvutia hata wawekezaji.
Kwa takribani miezi miwili sasa uongozi wa Manispaa ya Bukoba umeingia katika mzozo mkali kati yao na baadhi ya wafanyabiashara wa soko kuu la Manispaa ya Bukoba ambao hawataki soko hilo lisivunjwe kwa madai kuwa hawana maeneo mazuri ya kuuza bidhaa zao na badala yake wanataka soko hilo lijengwe wakiwa wanaendelea na biashara zao humo humo.
Katika malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara hao walisema wamekabiliwa na mikopo kutoka katika taasisi za fedha ambapo wanatakiwa kurejesha na hivyo kuvunjwa kwa soko hilo litawaathiri na huenda wakakamatwa kwa kutowasilisha mikopo kwa wakati,ujenzi wa soko hilo linatarajia kugharimu kiasi cha sh. bilioni 11 ambapo litajengwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwishoni mwa mwaka huu.
Hata hivyo katika uchuzi wa gazeti hili katika utekelezaji wa mradi wa soko hilo kupingwa na baasdhi ya wafanyabiashara na wakazi wa manispaa hiyo inatokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi waliowahi kuwa Madiwani katika Manispaa hiyo, ambao wanamiliki vibanda vya baiashara kuanzia sita hadi 10.
Baadhi ya watu hao ambao wamekuwa wakiwapangisha wafanyabiashara wengine kwa malipo ya juu, ndiyo wanaowashikini baadhi ya watu kukataa kutelekezwa kwa miradi hiyo kwa kuhofia kutoipata vibanda katika jengo hilo pindi litakapokamilika.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment