Sunday, September 30, 2012

Wiki ya kumbu kumbu na maziko rasmi ya masalia ya Kadinali Rugambwa yaanza leo Bukoba


Na Theonestina Juma, Bukoba
MAKAMU wa Askofu waKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Dkt. Methodius Kilaini amewataka waumini kanisa Katoliki Mkoa Kagera kushiriki kikamilifu katika wiki ya sherehe ya Muadhama Laurean Kadinali Rugambwa anayetarajiwa kuzikwa masalia yake rasmi Oktoba 6, mwaka huu katika kanisa kuu la Jimbo la Bukoba.
Rai hiyo imetolewa leo na Askofu Dkt.Kilaini wakati akihubiri katika misa ya pili iliofanyika katika la kanisa la Rumuli ikiwa ni kuanza kwa wiki ya maadhimisho ya Kadinali Rugambwa.
Askofu Kilaini alisema kwa kumuenzi zaidi matendo ya Kadinali huyo, mweusi wa kwanza Mwafrika, waumini wanapaswa kushiriki katika sherehe zake zilizoanza kuadhimishwa katika Jimboni humo Septemba 30, mwaka huu ambapo kilele cha maadhimisho hayo yatakuwa Oktoba 7, mwaka huu.
Alisema katika sherehe hizo za kuhamisha masalia ya Kadinali Rugambwa Oktoba 6, shughuli hizo zitaanza asubuhi katika parokia ya Kashozi alikozikwa kwa muda ambapo yatafanyika maandamano kutoka katika parokia hiyo hadi kanisa kuu la Bukoba mjini.
Alisema shughuli za kuzika rasmi masalia yake yatafanyika kuanzia saa 9.00 alasiri ndani ya kanisa kuu ambalo alitaka akizikwe ambapo kanisa hilo tayari limeshakamika kukarabatiwa.
Akielezea kwa wiki nzima shughuli zitazofanyika, alisema kuwa ni pamoja na kusomwa misa katika kijiji alikozwaliwa cha Rutabo, alikobaziwa parokia ya Kagondo  na Rutabo alikojenga seminari ,Bunena mjini Bukoba  na kisha Kashozi ambako siku anatangazwa kuwa Askofu alikuwa akifanya shughuli za kiuchungaji katika parokia yote hayo ni kuadhimisha kumbu kumbu yake.
Alisema enzi za uhai wa kadinali Rugambwa alikuwa kiungo wa Waafrika, maaskofu wa kiafrika na waumini nje ya nchi hadi ikafikia hatua wazungu wakaanza kuwapa waafrika nafasi za uongozi.
“Kadinali Rugambwa alikuwa kama bendera iliowekwa juu ya milingoti ili kila mtu aione, hii ni kutokana na yeye aliweza kukaa na wazungu katika kiti kimoja kujadili mambo mbali mbali yahusuyo jamii na dini, hivyo yeye alikuwa kama kiungo”alisema askofu  Kilaini.
Alisema katika Tanzania Kadinali Rugambwa ni muasisi wa Baraza la maaskofu na alikuwa mchungaji mwema kutokana na kuwapenda waumini, watawa na mapadri wake.
Halidhalika alikuwa mpenda maendeleo, ambapo katika enzi za uhai wake aliweza kuanzisha miradi mbali mbali za kanisa kama ujenzi wa shule za sekondari, hospitali na vtuo vya afya ambapo alikubalika kwa dini zote kulingana na maelezo ya watu mbali mbali waliokuwa naye karibu.
Mwisho.

Friday, September 28, 2012

Hayawi hayawi hatimaye yamekuwa, maandalizi ya maziko rasmi ya Kardinali Rugambwa yapamba moto Bukoba

Ukiona tangazo kama hili limetundikwa juu ujue mambo yameiva, ni kweli Oktoba 6, hiyoooo, masalia ya Kadinali Rugambwa kuhamishwa na kuzikwa rasmi.
 Hii sehemu ya barabara ya Jamuhuri karibu na Kanisa kuu Jimbo la Bukoba likiwa katika ukarabati kwa ajili ya sherehe ya kuhamisha masalia ya Kadinali Rugambwa.

Hii ni barabara ya Kashozi inayoelekea katika parokia ya Kashozi alikozimwa kwa muda Kadinali Rugambwa ambapo masalia yake yatapitishwa wakati akienda kupumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Humu ndimo masalia ya Kadinali wetu, Laurean Rugambwa yatakapopumzishwa milele

Hii sehemu ya jengo la kanisa kuu Katoliki la Jimbo la Bukoba linavyoonekana kwa upande wa kushoto.
 Sehemu ya kasani kuu Jimbo la Bukoba ambamo atazikwa rasmi  Kadinali wa kwanza Mwesi  Mwafrika Kadinali Laurean Rugambwa anakotarajiwa kupimzishwa milele hapo Oktoba 6, mwaka huu linavyoonekana kwa mbele licha ya kuwa bado mafundi wanasawazisha maeneo yaliobaki.
 Hivi ndivyo kanisa hilo linavyoonekana.
 Sehemu hii ya geti la lango kuu la kanisa hilo, ambalo masalia ya Kadinali Rugambwa unatarijia kupitishwa wakati akingizwa kanisani humo tayari kwa kuhifadhiwa milele.

Hii ni barabara ya Jamhuri ambayo masalia ya mwili wa Kadinali Rugambwa utapitishwa wakati wa kuingizwa katika ikulu yake ya milele(PICHA ZOTE NA THEONESTINA JUMA)

Thursday, September 27, 2012

Mwanamke ajinyonga Ngara baada ya kupata ujumbe kutoka kwa majini kumtaka afanye hivyo


Na Theonestina Juma
MWANAMKE mmoja makazi wa kijiji cha Buhororo wilayani Ngara, amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani kwa madai ya  kila mara alikuwa akipata ujumbe kutokana na watu kama majini yaliokumtaka  ajinyonge.
 Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka wilayani Ngara na kuthibitishwa na Kaimu  Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Paul Bwinyo tukio hilo la aina yake lilitokea Septemba 26, mwaka huu kijijini hapo.
Mwanamke aliamua kujitia kitanzi amejulikana kuwa Bi.Christina Zemitembe (37) na kwamba alijinyonga nyumbani kwao alikokuwa akiishi na mama yake mzazi Bi.Zemitembe (70).
Alisema siku ya tukio, mwanamake huyo aliamuaka asubuhi na kupanda juu ya meza na kisha kujitia kitanzi, ambapo kwa wakati huo mama yake mzazi alikuwa ameenda shambani.
Imeelezwa kuwa muda wa saa saba mama yake aliporejea kutoka shambani alikuta mlango wa nyumba yake ukiwa umefungwa kwa ndani jambo ambalo lilimlazimu kuomba msaada kwa majirani.
Alisema majirani hao walilazimika kuharibu mlango ambapo walipoingia ndani hawakuweza kuamini kilichotokea, kwani tayari  mwanamke huyo alishajitia kitanzi na kubaki akining’ngia juu.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Winfrida Thomas akielezea hali aliokuwa nayo mwanamke huyo kabla ya kujiua, alisema kila mara Bi. Christina alikuwa akisema juu ya kutaka kujiua kwa kujinyonga.
“Mwezi Aprili mwaka huu Christina  alikuwa akisikika akisema kuwa amekuwa akipata maono (ujumbe) kutoka watu kama majini ambayo yanamtaka ajinyonge.”alisema.
Hata hivyo, Bi. Thomas alisema kuwa kutokana na maneno yake hayo walidhani kuwa alikuwa akitania na hawakujua kama kweli alikuwa akidhamiria kutenda kitendo hicho,Jehi la Polisi Mkoani Kagera, bado linafuatilia juu ya tukio hilo.
Mwisho.

Wednesday, September 26, 2012

Niko Tayari kushiriki mazishi ya Kadinali Rugambwa hapo Oktoba 6, 2012

Yap, niko tayari kwa siku hiyo muhimu katika historia ya maisha yangu, ikizingatiwa kuwa wakati Kadinali Rugambwa akifariki dunia nilikuwa kidato cha tatu, bado kinda sasa mazishi yake rasmi mimi bonge la mama.


Changia kanisa kwa kununua sare zao rasmi ili kufanisha sherehe hizo.Hiki kitenge nilichojifunga ni moja ya aina ya sare itakayotumika siku hiyo ya Oktoba 6, mwaka huu, siku ambayo mwili wa Kadinali Rugwambwa utahamishwa kutoka katika Parokia ya Kashozi alikozikwa kwa muda na kisha kupumzishwa katika nyumba yake ya milele katika kanisa Kuu la Jimbo la Bukoba.Siku hiyo maelfu ya wageni wanatarajiwa kufurika katika Manispaa ya Bukoba.

Tuesday, September 25, 2012

Kuhamishwa mwili wa Kadinali Rugambwa, wasiovaa sare maalum wataonekana kama watu wa mitaani tu-Katibu


Na Theonestina Juma, Bukoba
ZIKIWA zimebaki takriban siku 10 mwili wa aliyekuwa Kadinali wa kwanza Mwafrika,Muadhama Laurean Rugambwa kuhamishiwa katika jengo la Kanisa katoliki mjini Bukoba, uongozi wa kanisa hilo umetoa onyo kali kwa wafanyabiashara walioanza kunufaika tukio hilo bila ridhaa yao.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya baadhi ya wafanyabiashara katika Manispaa ya Bukoba kutengenezesha fulana zenye nembo ya kanisa hilo pamoja na picha ya Kadinali Rugambwa wakiziuzwa  kwa sh. 12,000 bila ridhaa ya uongozi wa kanisa hilo.
Kutokana na hali hiyo Katibu wa Askofu wa Jimbo la Bukoba, Padri Deodatus Rwehumbiza akizungumza na gazeti hili jana (leo) alisema waumini watakaonunua bidhaa za wafanyabiashara ambao zimetengenezwa bila baraka za kanisa hilo, hawatapewa kipaumbele siku ya sherehe hiyo kama ilivyo kwa waumini watakaovaa sare yalioandaliwa na uongozi wa kanisa hilo na watawaona kana kwamba hawajavaa sare za sherehe hiyo.
Alisema watu hao hawatapata mafao kama wale watakao vaa sare zao kwani bidhaa hizo wamezitengeza kwa ajili ya kuwezesha siku ya tukio watakaohudhuria waweze kufahamika kiurahisi na kununua sare hizo wanachangia ufanisi wa sherehe hiyo na kwamba sare zao zinafahamika na hivyo hao ndiyo watakaopewa nafasi ya kwanza.
Alisema kwa wale watakaokuwa na sare za kughushi na kwa kuwa wameshambulia hilo mapema na kuwataarifu, watakaokaidi watawaona kama wale waliotoka mitaani na kuingia katika shehere hiyo.
Hata hivyo, gazeti hili lilipotaka kujua kwa siku hiyo hawatawathamini, Padri Rwehumbiza alisema kuwa watawathamani, lakini kupata hudhuma kama wale watakaovaa sare zao, haitakuwa rahisi mfano kama sehemu za kukaa zitakazoandaliwa.
Katibu hiyo alitoa kauli hiyo, baada ya gazeti hili kutaka kujua, iwapo waumini  wao watakuja kanisani siku hiyo wakiwa wamevaa mavazi yaliotengenezwa na wafanyabiashara bila ridhaa ya uongozi wa kanisa hilo, watafanyaje.
Alisema kutokana na kuwa makini katika maandalizi ya sherehe ya Agosti 6  na 7,ya kuhamisha mwili wa Kadinali Rugambwa kutoka katika kanisa ya Kashozi alikozikwa kwa muda, tayari walishabaini ujanja wa baadhi ya wafanyabiashara hao na wamekuwa wakiwataarifu waumini wao juu ya jambo hilo.
Alisema mmoja wa mfanyabiashara wa mjini hapa ambaye hakuwa tayari kumtaja jina lake, walifika katika duka lake na kukuta fulana ambazo zilitengenezwa rasmi kuhusiana na siku ya tukio hilo.
“Tulifika katika mmoja ya duka mjini Bukoba  na kukuta fulana zinazohusiana na sherehe ya kuhamisha mwili wa Kadinali Rugambwa,… na kubariki kanisa kuu….tulijifanya kama wanunuzi, tulinunua sh.12,000 na kukatiwa risiti”alisema
Alisema kutokana na hali hiyo tayari walishatoa taarifa kituo cha polisi kuhusiana na tukio hilo, ambapo katika mahojiano zaidi mfanyabiashara huyo alisema kuwa fulana ndizo zilikuwa bidhaa za kwanza kuingizwa sokoni ambapo walikuwa na mpango wa kuteneza vitambaa.
Hata hivyo, Padri Rwehumbiza alipotakiwa na gazeti hili kueleza kama fulana hizo zimetengezwa mjini Bukoba au nje ya mjini hapa alisema kuwa haijajulikana fulana hizo zimetengenezwa wapi, wala haijajulikana wako wafanyabiashara wangapi, zaidi hilo sasa ni jukumu la polisi kufuatilia.
Kuhusiana na hatua walikofikia ya maandilizi ya sherehe hizo, Katibu huyo alisema kuwa yanaendelea vizuri na kwamba yatafanyika jinsi yalivyo pangwa na kwamba zaidi ya wageni 5000 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria.
Kuhusiana na viongozi wa kitaifa  alisema kuwa mialiko wametuma kwa wote  ambapo majibu yanayopatikana hayaoneshi kukatisha tamaa.
Septemba 23, mwaka huu katika kanisa katoliki la Rumuli yalisikika matangazo ya kanisa hilo yakieleza juu ya kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara waliotengeneza fulana na vitenge yenye maandishi kuhusiana na matukio ya sherehe hizo, bila idhini ya kanisa hilo.
Katika matangazo hayo yalieleza kuwa fulana hizo zina maandishi kwa nyuma, ambapo hata bei zao hawajaafikiana nao na uongozi wa kanisa.
Sare zinazouzwa na kanisa hilo katika maduka yake mjini hapa, fulana na vitenge vinauzwa sh. 13,000 ambapo fulana za wafanyabiashara binafsi zinauzwa sh. 12,000.
 Mwili wa Mwadhamu Kadinali Rugambwa unatarajiwa kuhamishwa rasmi Oktoba 6,saa 9.00 alasiri mwaka huu ukitokea katika parokia ya Kashozi alikokuwa amezikwa kwa muda  kupekelekwa katika Kanisa kuu la Jimbo hilo lililochukua zaidi ya miaka 10 kukamilika kwa ukarabati wake.

  Aidha  Oktoba 7, mwaka kutafanyika sherehe nyingine ya kubarikiwa kwa kanisa hilo na kumbukumbu ya  miaka 100 ya kuzaliwa kwa kadinali huyo wa kwanza Mwafrika.

 Muadhama Kadinali Rugambwa alizaliwa  Julai 12, 1912 katika kijiji cha Bukongo Rutabo Kamachumu wilayani Muleba katika familia ya kifalme na kufariki dunia mwaka 1997.
 
mwisho.
Top of Form

Top of Form
Bottom of Form

Friday, September 21, 2012

MKUU WA MKOA ATATUA MGOGORO WA SHULE KATI YA WANANCHI NA MBUNGE WAO.


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe hatimaye ametatua mgogoro wa shule ya sekondari ya Wasichana ya Ruth Msafiri kati ya Wananchi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Muleba Kaskazini Ruth Blasio Msafiri kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010.
Mhe. Massawe alikabidhi shule hiyo kwa Wananchi wa Kata ya Katoke jana tarehe 17/09/2012 ili waendeleze ujenzi baada ya kuwa na mgogoro zaidi ya miaka miwili kati ya Wananchi na aliyekuwa mbunge wao 2005 hadi 2010 kwa kudai shule hiyo ni mali yake binafsi baada ya kuwa ameshindwa ubunge mwaka 2010.
Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana ya Ruth Msafiri iliyoko katika kitongoji cha Kimbugu, Kijiji Katoke Tarafa Izigo Halmashauri ya Wilaya Muleba ilianzishwa na Ruth Blasio Msafiri wakati huo akiwa Mbuge wa Jimbo la Muleba Kaskazini mwaka  2009.
Kulingana na taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na seriklai ya kijiji Katoke Ruth Msafiri alitoa wazo la kuanzisha shule ya wasichana na kuomba ardhi katika serikali ya kijiji na kupewa Ekari 40 za ardhi kwa kuwa walikubaliana shule hiyo iwe ya wananchi wa Kata ya Katoke.
Pia wananchi walikubaliana shule hiyo iitwe kwa jina la Ruth Msafiri baada ya kuwa yeye ndiye aliyeanzisha wazo la kuwa na shule ya wasichana katika kata hiyo. Vilevile Bi Ruth Msafiri alianza kuomba michango kwa niaba ya wananchi  ili kuanzisha ujenzi wa shule hiyo mwaka 2009.
Wananchi walichangia nguvu zao pia mfuko wa jimbo ulichangia Shilingi 3,000,000/=, Benki ya NMB ilichangia shilingi 5,000,000/= Wizara ya Maliasili na Utalii shilingi 6,000,000/=, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kikwete alichangia mabati 300 na ndipo ujenzi wa shule hiyo ulianza.
Baada ya uchaguzi Mkuu 2010 Ruth Msafiri hakubahatika kuchaguliwa tena kuliwakilisha jimbo la Muleba Kaskazini na ndipo mgogoro ulianza na akadai kuwa shule ni mali yake jambo ambalo wananchi hawakukubaliana naye na kuanza kulalamika na malalamiko hayo yalimfikia Mkuu wa Mkoa.
Tarehe 20/02/2012 Mkuu wa Mkoa alitembelea kijiji cha Katoke na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi na alisikiliza mgogoro huo kwa undani na akaagiza wananchi wapitie kwenye ngazi husika za kisheria kuanzia ngazi ya kijiji Balaza la Kata na Balaza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ili kulidhia kuwa shule hiyo ni mali ya wananchi.
Aidha baada ya hatua zote Mkuu wa Mkoa alizoagiza  kufuatwa nay eye kuridhia jana tarehe 17/9/2012 Mhe. Massawe aliikabidhi shule hiyo kwa wananchi ili kuendeleza ujenzi kwaajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2013.
Kutokana na furaha ya kukabidhiwa shule yao wananchi wakiongozwa na Mhe. Massawe na Mkuu wa Wilaya ya Muleba walianza kuchangia ujenzi wa shule hiyo kwa kutoa fedha taslim, ahadi na zaidi ya shilingi 1,800,000/= zilichangwa pia mawe, mchanga, sementi, misumari na mbao vilihaidiwa kuchangiwa na wananchi hao.  
Shule hiyo ina jengo la utawala pia na vyumba viwili vilivyo pauliwa tayari, na msingi wa vyumba vitatu ambavyo havijakamilika. Wananchi walimhaidi Mkuu wa Mkoa kufikia mwezi Oktoba 2012 majengo hayo tayari yatakuwa yamekamilika kwa ajili ya Januari mwakani.
Imetolewa na:
Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa,
Kagera @2012