Tuesday, June 26, 2012

Wahabeshi 45 wafa kwa kukosa hewa, watelekezwa msituni Dodoma

 Dodoma
RAIA 45 wa Ethiopia wamekufa na wengine 72 wako taabani baada ya kukosa hewa katika lori walilokuwa wakisafiria kwenda Malawi.

Maiti za watu hao na wenzao ambao wako katika hali mbaya, waligundulika leo asubuhi katika msitu wa Chitego wilayani Kongwa, Dodoma.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alithibitisha  leo tukio hilo baada ya kufika katika eneo hilo na msafara wa polisi, akiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen.

Silima aliitaja idadi ya watu waliokufa kuwa ni 45 na kuwa wengi wao walikuwa katika umri mkubwa. Vijana walinusurika, lakini nao walionekana kudhoofu, alisema.

“Ni kweli niko katika eneo la tukio, inasikikitisha watu hawa wamekufa vibaya. Inaonyesha kuwa walikufa kwa kukosa hewa wakiwa ndani ya lori, lakini bado tunafanya uchunguzi zaidi ikiwa ni pamoja na kusaka roli hilo ambalo lilitokomea kusikojulikana,’’ alisema Silima.

Naibu Waziri huyo alisema kuwa uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa watu hao walikuwa wakifa mmoja baada ya mwingine na dereva alipogundua hilo aliona hakuna namna zaidi ya kuwatupa porini.

Alisema kitendo cha kusafirisha watu hao kimekuwa ni mchezo wa kawaida kwani Watanzania ndio wanaosaidia kuwasafirisha kutoka Nairobi kupitia Arusha na mara nyingi hupita usiku katika njia za panya.
Kwa mujibu wa Silima, miili ya watu hao ilichukuliwa jana na kupelekwa kwa ajili ya uchunguzi huku wakitafuta mawasiliano na Ubalozi wa Ethiopia ili kuona namna watakavyofanya.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya alithibitisha kupokea maiti hiyo na wengine walio hai kupewa msaada wa kimatibabu.

Dk Mpuya alisema katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alitegemea kupokea maiti 25 na wagonjwa wawili waliokuwa katika hali mbaya, huku maiti 20 zilitarajiwa kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi.

Mganga huyo alisema watu wengine ambao walionekana kuwa na hali nzuri kidogo wangepita hospitalini hapo na kupewa huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa kwenye vyombo vya sheria kwa mahojiano zaidi.


No comments:

Post a Comment