Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi-
Zanzibar
VIONGOZI wanne wa Kundi la Uamsho waliohusika katika
uchochezi wa vurugu za wiki iliyopita mjini zanzibar, leo wamejisalimisha kwa
Makachero wa Jeshi la Polisi na kuhojiwa kwa masaa kadha kabla ya kuachiwa kwa
mashariti.
Taarifa ya Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi
Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, imewataja viongozi
waliojisalimisha kuwa ni Shekhe Suleiman Juma(62) mkazi wa
Makadara na Shekhe Fikirini Majaliwa(47), mkazi wa Jang’ombe.
Taarifa hiyo imewataja wengine waliojisalimisha kuwa ni
pamoja na Katibu wa Jumuia ya Uamsho Sheikhe Abdallah Saidi(45), mkazi wa
Misufini pamoja na Afisa Usalama wa Jumuiya hiyo Bw. Haji Sadifa(51), mkazi wa
Mwembenjugu.
Viongozi hao pamoja na mpambe wao, walijisalimisha
mapema asubuhi leo kwa Viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Mangaribi
Zanzibar na kuhojiwa kwa muda kabla ya kupelekwa Makao Makuu ya Upelelezi
Zanzibar kwa mahojiano zaidi na baadaye kuachiliwa kwa
dhamana.
Tangu kutokea kwa vurugu zilizopelekea kukamatwa kwa
baadhi ya wafuasi wa kundi la Uamsho mjini Zanzbar na kufikishwa mahakamani
kujibu tuhuma zao, viongozi hao watatu pamoja na mpambe wao walikuwa
hawajapatikana.
Mara baada ya vurugu hizo za wiki iliyopita, Kamishna
wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, alisema kuwa Jeshi la Polisi
litahakikisha kuwa wale wote waliochoche vurugu hizo wanakamatwa na kufikishwa
mahakamani kujibu mashtaka yao.
Katika vurugu hizo zilizodumu kwa muda wa siku tatu,
pia zilizopelekea kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa na mali nyingine za
madukani kuporwa na nyingine kuharibiwa na wafuasi wa kikundi hicho.
Jeshi la Polisi Visiwani hapa limeendelea kutoa wito
kwa viongozi wengine walioshiriki katika vurugu hizo kujisalimisha wenye Polisi
badala ya kusubiri kutafutwa.
Hadi sasa watuhumiwa 78 wakiwemo viongozi wa kundi la
Uamsho, wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo baadhi yao wameachiliwa kwa
dhamana na wengine wakipelekwa rumande kwa kukosa wadhamini wenye kuaminika hadi
Juni 11, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment