Msafara
wa watu 25 wa timu ya Taifa ya wanawake ya Ethiopia umewasili leo (Juni 14 mwaka
huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwa ajili ya mechi dhidi ya
Twiga Stars.
Mechi
hiyo ya marudiano kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Afrika kwa
Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea
itachezwa Jumamosi (Juni 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia
saa 10 kamili jioni.
Mshindi
baada ya matokeo ya mechi ya awali ambapo Twiga Stars ilifungwa mabao 2-1 na
mechi ya Jumamosi atafuzu kwa fainali hizo za Equatorial Guinea. Nchi ambazo tayari zimefuzu
kwa fainali hizo ni wenyeji Equatorial Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC).
DRC
ilikuwa icheze raundi ya pili na Equatorial Guinea, lakini baada ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuipa uenyeji Equatorial Guinea, DRC nayo imefuzu
moja kwa moja kucheza hatua hiyo ya fainali.
Makocha
wa Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa na mwenzake wa Ethiopia, kesho (Juni 15
mwaka huu) saa 5 asubuhi watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi
za TFF kuelezea jinsi timu zao zilivyojiandaa kwa mechi
hiyo.
Viingilio
katika mechi hiyo vitakuwa sh. 10,000 kwa VIP A na sh. 5,000 kwa VIP B na C.
Sehemu nyingine zilizobaki kiingilio ni sh. 2,000 na tiketi zitauzwa uwanjani
siku ya mechi kuanzia saa 3 asubuhi.
No comments:
Post a Comment