Na
Theonestina Juma, Bukoba
WAVUVI na
wakala wa samaki katika Ziwa Victoria upande wa Mkoa Kagera wameiomba serikali
kuingilia kati kutatua mgogoro ulioibuka kati yao na wamiliki wa viwanda vya
samaki vilivyoko mkoani Mwanza, kutokana na kile kinachodaiwa kushuka kwa bei
ya samaki katika soko la dunia.
Wavuvi na
wakala hao wamesema hayo jana wakati wakizungumza na Blog hii kwa nyakati
tofauti kwa njia ya simu kutoka katika visiwa vya ikuza Wilayani Muleba.
Walisema
mgogoro uliopo kati yao ni kutokana na kushuka kwa bei ya samaki wanaowauzia
kutoka sh. 4,800 - 5,500 hadi kufikia sh. 3,000 - 2,600 kwa kilo, kiasi ambacho
hakilingani na kazi wanayoifanya na hivyo kuona kufanya biashara ya hasara tu,
hata hakiwezi kuwasaidia kukidhi maisha yao.
Walisema
tangu mgogoro huo uanze kufurukuta ni takribani wiki tatu sasa jambo
lililowalazimu baadhi ya makambi ya wavuvi kufungwa baada ya wakala na baadhi
ya wavuvi wa samaki kukaa vikao zaidi ya mara nne kujadili muafaka wao bila
mafanikio.
Mmoja wa
wavuvi na wakala wa samaki katika kisiwa cha Ikuza, Bw. Collins Joshua
akizungumza na Majira kwa njia ya simu kutoka visiwani humo alisema, hatua
waliofikia kwa sasa inasikitisha kwani wavuvi wamelazimika kupaki mitumbwi yao
na hivyo hakuna anayejisughulisha na kuvua samaki kwa ajili ya kuwauzia
wamiliki wa viwanda ambao wanaonekana hawana bei inayoeleweka kwao.
Bw. Joshua
alisema serikali inatakiwa kuingilia kati ili kuweza kubaini kama bei ya samaki
imeshuka katika soko la dunia ni kwa kiasi gani na kwa nini na wamiliki wa
viwanda wanatakiwa kununua samaki kutoka kwao kwa kiasi gani na si kubaki
kujipangia bei kama ilivyo kwa hivi sasa ambapo kila kiwanda kina bei yake.
“Juni 4, mwaka
huu tulipewa taarifa kutoka kwa wamiliki wa viwanda kuwa bei ya samaki imeshuka
katika soko la dunia, tena Juni 8 tukaambiwa kuwa sasa watanunua samaki kwetu
kwa sh. 3,500, hatujatulia kutafakari hilo Juni 9 mwaka huu tunapewa taarifa
nyingine kuwa wananunua samaki iliochakatwa kwa sh. 3,000 kwa kilo,
hatujatafakari tena tunashangaa Juni 12, mwaka huu tena tunaambiwa kwa sasa
wananunua samaki aina hiyo kwa sh. 2,600, huu ni ubabaishaji, ya serikali
kuwaachia watu hawa kufanya watakalo”alisema.
Alisema kwa
kiasi hiki, wao hawawezi kupata kitu chochote zaidi ya kuwafanyia wamiliki wa
viwanda jambo ambalo alieleza kuwa inatakiwa ijulikane wazi sasa biashara hiyo
inafanywa kwa mfumo upi na sio kila kiwanda kujipangia bei yake.
“Kilio chetu
kwa sasa tunataka kujua bei rasmi, samaki ambaye hajachakatwa ni shilingi
ngapi, hali ya soko la samaki duniani iko vipi, bei imeshuka kwa kiasi gani na
sababu ni nini, kuna maeneo mengine samaki wa maji baradi wameongezeka”alisema.
Alisema
awali samaki alinunulia kutoka kwa mvuvi kati ya sh. 3,800 hadi 4,000 kwa kilo,
ambapo wao mawakala walilazimika kuwauzia wamiliki wa viwandani kati ya sh.
4500 hadi 5500 kwa kilo lakini wanashangazwa na bei kushuka kutoka kiasi hicho
hadi 2,600 kwa kilo jambo linalowashinda wao wanunue samaki hao kwa mvuvi kwa
kiasi gani ikizingatiwa kuwa bei ya mafuta na vifaa vya uvuvi vikipanda bei
kila kukicha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment