Friday, June 1, 2012

Tumieni upashanaji habari kuokoa ziwa letu


                              Na Theonestina Juma
IMEELEZWA kuwa njia moja kubwa ya kushiriki katika kulitunza Ziwa Victoria ni upashanaji wa habari.
 Kauli hiyo imetolewa leo na Afisa Utumishi wa Mkoa Kagera, Bw.Richard Kwitega kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kagera Kanali Fabian Massawe wakati akifungua semina elekezi ya uhifadhi wa mazingira ya Ziwa Victoria awamu ya pili ya bonde la Ziwa hilo inayohudhuriwa na viongozi wa Halmashauri naManispaa zilizo ndani ya bonde la ziwa hilo inayofanyika katika ukumbi wa Kolping mjini hapa.
 Alisema njia hiyo ikitumika itarahisisha hatua za haraka zikuchuliwe kila inapobidi, kuokoa bayoanuai ya ziwa hilo ambalo ndilo tegemeo kubwa la wananchi wa maeneo hayo.
 Alisema viongozi wanatakiwa kusimamia na kuhimiza juhudi za kuhifadhi rasilimali za ziwa Victoria kwa kuzingatia mbinu zote  za kutunza na kuhifadhi mazingira na rasilimali zake ili uhai uwe wa uhakika na wa kudumu.
 Bw.Kwitega alisema Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na lina hazina kubwa zaidi ya samaki wa maji baridi duniani.
 Alisema samaki wa thamani kubwa wanapatikana katika ziwa hilo na wanailetea nchi kipato kupitia soko la ndani na nje ya nchi hivyo ni jukumu la watu wote kulilinda.
 Alisema inakadiriwa kuwa miaka ya nyuma kabla ya uharibifu wa ziwa hilo kuanza samaki walivunwa kati ya tani 400,000 na 500,000 kwa mwaka ambapo walichangia pato la taifa takribani dola za Marekani bilioni 3 hadi 4 kwa mwaka.
 "Pamoja na hayo kwa sasa inakadiriwa mavuno ya samaki yameshuka kufikia tani 243,564
kwa takwimu za mwaka 2010.Semina hiyo ya siku mbili inahudhuriwa na Wenyeviti, Mameya, Wakurugenzi na Makatibu Tawala wa mikoa ya Geita, Kagera,Mara na Mwanza.


No comments:

Post a Comment