Na  Theonestina Juma, Bukoba
WATU watano wamefariki dunia na wengine 26 wamejeruhiwa katika ajali ya gari la polisi la mkoani Kagera wakati wakitoka kwenye mashindano ya mpira wa miguu wa polisi Jamii wilayani Ngara.
Habari zilizopatikana mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa polisi Mkoani Kagera, Phillip Kalangi, ajali hiyo imetokea Oktoba 14, mwaka huu saa 2 usiku katika barabara ya Kabanga  Rusumo wilayani Ngara.
Imeelezwa kuwa  ajali hiyo ilihusisha gari la polisi lenye namba ya usajili PT 2007 iliokuwa imebeba mashabiki wa timu ya polisi jamii, wapatao 31 kutoka kwenye mashindano ya mpira yaliofanyika Kabanga.
Gari hilo lilipata ajali baada ya kugongana na semi trella ambayo ilikuwa ikienda nchini Rwanda, ambapo gari  la polisi  lilikuwa likikwepa semi trella hilo lakini lilijigonga kwenye jiwe kwa mbele na kupinduka.
Watu waliofariki katika  ajali hiyo wamejulikana kuwa ni pamoja na Rwekaza Philipo, James Rutaihwa  na  Erick Richard.
Wengine ni pamoja na Kazungu na Nature waliopatikana kwa jina moja moja na wote ni wakazi wa wilayani Ngara.
Aidha majeruhi 26 wamelazwa katika hospitali Teule ya Omurugwanza ya wilayani Ngara, ambapo watu watatu walimelezwa kuwa hali yao ni mbaya  na watu 23 walitibiwa  na tayari wamesharuhusiwa.
Kamanda Kalangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka tairi  baada ya gari la polisi kugonga jiwe wakati likikwepa semi trella.
Mwisho.