Pata habari moto moto kila siku, kwa Mawasiliano zaidi piga Simu Na. 0755 856991/ 0712 992434 Email:-theonestinajuma@yahoo.com/rorya.09@gmail.com
Wednesday, June 6, 2012
Muafaka wa sakata la viwanja 800 vya miaka 10 iliopita bado kitendawili Bukoba
Na Theonestina Juma, Bukoba
UONGOZI wa Manispaa ya Bukoba, umeshauriwa kutumia busara badala ya nguvu na mabavu kama inavyoonekana kwa sasa katika kutatua mgogoro wa viwanja 800 vya watu waliotoa fedha zao kwa ajili ya gharama ya kupimiwa viwanja takribani miaka 10 iliopita.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Maendeleo (CHADEMA) wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Victor Sherejei wakati akichangia majadiliano juu hatima ya wananchi 800 wanaodai viwanja vyao katika Manispaa ya Bukoba, katika kikao cha Kamati ya Ushauri wa Mkoa Kagera uliofanyika mjini hapa.
“Kwa sasa Uongozi wa Manispaa unatumia nguvu na mabavu kutaka kuwapora wananchi viwanja vyao, suala hili haliwezekani na haingii akilini, lazima Manispaa itumie busara kuwapatia wananchi 800 viwanja vyao, bila kutoza riba, suala la kusema kuwa waongeze pesa ili wapewe viwanja vyao sio sahihi” alisema na kuongeza
“ Jiulizeni mwaka 2002 mfuko wa saruji uliuzwa kiasi gani na mkwaka huu ni kiasi gani, thamani ya dola mwaka huo ilikuwa ni kiasi gani, sasa kwa nini hawa wananchi watakiwe kuongeza pesa tena? waingie hasara kwa uzembe wa Uongozi wa Manispaa? hii sio haki ni dhuluma…. msitumie dhuluma kuwanyang’anya wananchi haki zao’alisema Mwenyekiti huyo.
Bw. Sherejei alisema viwanja hivyo 800 wananchi walitoa fedha zao kwa ajili ya kuchagia gharama ya upimani kati ya mwaka 2002,2003 hadi 2004 ambapo baadhi ya watu walipimiwa na kupewa viwanja vyao ambapo walibaki watu 800 hivyo, katika mradi wa Manispaa uliopima viwanja 5000 uongozi utoe viwanja 800 uwapatie wananchi wanaodai kwani ni haki yao.
“Huu ni uzembe uliofanywa na Manispaa kuwapatia wananchi viwanja vyao, sasa hili suala la kupatia wananchi hao penati, hii ni kuwapa adhabu… adhabu ya kuwachelewesha tena mnawawekea riba, huu ni unyanyasaji”alisema
Alisema pendekezo lake manispaa hiyo ikae na kuangalia na kujadili ili kuweza kutoa viwanja 800 kati ya 5000 vilivyopimwa iwapatie wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kagera, Bi. Costancia Buhihe akichangia juu ya hatima ya wananchi 800 wanaodai viwanja vyao hakuwa tofauti na mawazo ya Mwenyekiti wa CHADEMA, kwani alisema Manispaa itoe viwanja 800 kutoka mradi wa viwanja 5000 vilivyopimwa ili kuwapatia wananchi.
Alisema wananchi hao 800 wanatarajia kupata jibu chanya kutokana na uwagawaji wa viwanja hivyo 5000 hivyo, waitishwe wale wote wanaodai viwanja vyao waitishe mkutano ya wao peke yao ili wakae wajadiliane nao.
“Nadhani Manispaa wanao mawasiliano ya watu hawa 800 wanaodai viwanja vyao, wawaite, watumie njia zozote kwama ni kwa njia ya vyombo vya habari, wahakikishe watu hawa wote wanapata taarifa ya kuhudhuria kwenye kikoa hicho ambacho kitakuwa maalum, ili wajadiliane,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema “ muawatangazie tarehe maalum, ya kukutana nao wawe peke yao wasichanganywe na watu wengine, hawa watu nadhani hata ikifika siku mnatangaza majina ya waombaji wapya watakuwa tayari kupokea majibu aina yoyoye yale, hii itatuondolea migogoro isio ya lazima”.
Alisema kwa wale ambao hawatahudhuria, bado wataendelea kuthaminiwa na hapa itajulikana kabisa kuwa watu kadhaa matatizo yao wametatuliwa na walio baki ni watu kadhaa ndipo mtangaze majina ya waombaji wapya.
Bi. Buhiye alisema pamoja na kuwa Manispaa ya Bukoba inatakiwa kubadilika na kukua na tunapoelekea katika Jumuia ya Afrika Mashariki Bukoba iko kati kati na hivyo haiwezekani ikaendelea kuwa kama mji wakati ni Manispaa hiyo haiweze kuendelea kama hawatakubali mipangilio mipya, miundombinu bila mabadiliko.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa Kagera, Bw. Nassor Mnambila akichangia suala hilo alisema haiwezekani ikachukuliwa fedha ya leo wakati watu hao walichangia fedha zao mwaka 2002.
“Kama nahitaji kitu, lazima nipewe leo, haiwezekani kitu nataka natoa hela halafu eti nalipwa baada ya miaka mitatu kupita ninapaswa kulipwa leo, si hela nimetoa kwa ajili ya hitaji langukwa siku ya leo… hivyo watu hao ni haki yao”alisema
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Bw. Khamis Kaputa akizungumzia juu ya mgogoro huo alisema mwaka 2002 sheria mpya ya ardhi ilianza kutumika ilimtaka mtu kuchangia gharama ya upimaji lakini si kwamba fedha hizo ndizo zilitakiwa kutumika mpaka kuwapatia hati, kwani walitakiwa kulipia na kuna gharama zingine zilizokuwa zikiongezeka.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa Kagera, Kanali Fabian Massawe alijaribu kuwatetea uongozi wa Manispaa hiyo kwa madai kuwa mwaka huo ambao wananchi hao walitoa fedha zao kwa ajili ya kupimiwa viwanja viongozi wa sasa, Mstahiki Meya, Dkt. Anatory Amani na Mkurugenzi wake, Bw. Kaputa hawakuwepo na hivyo haukuwa uzembe wao jambo ambalo liliokana kutokubaliwa na baadhi ya wajumbe wa kikao hicho.
Hadi mwisho aliushauri uongozi huo kurudi tena kukaa na kujadili suala hilo ikiwa ni pamoja na kuwaita wananchi hao na kuongea nao ana kwa ana na kupatiwa viwanja vyao.
Wananchi hao 800 katika miaka 10 iliopita wanadaiwa kuwa walitoa fedha zao kati ya sh. 50,000 hadi 70,000 kwa ajili ya kuchangia gharama ya kupimiwa viwanja ambapo hadi leo hajawajapatiwa licha ya kuwa Manispaa hiyo imepima viwanja 5000 lakini wanawaka kuongeza hela ili kuweza kupewa kipaumbele wakati zoezi hilo litapoanza ambapo mwisho wa kununua fomu ya viwanja hivyo imeisha jana Juni 5, 2012 katika benki ya posta.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment