Friday, June 1, 2012

Waratibu wa Sensa hatimaye wafunguka kwa vyombo vya habari

Mkurugenzi wa Operesheni ya Takwimu  Bi,  Radegunda Maro  (kulia) akiongea na wamiliki mbalimbali wa vyombo vya habari nchini  juu ya namna ya Uelimishaji jamii kwenye Sensa inayotarajia kuanza mapema mwezi ujao  tarehe 26 ambapo alisema kuwa wao kama tume nzima wamejipanga sawasawa katika uelimishaji wa jamii juu ya swala hilo la sensa. Mkutano huo umefanyika leo katika Hoteli ya PeakCook jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Sensa nchini  Bi, Hajjat Amina  Mrisho (kushoto) akielezea namna walivyojipanga kushirikiana na vyombo vya habari katika mkutano huo ambapo alisema kuwa wametenga kiasi cha Bilioni 141.5 kwa ajili ya kuhakikisha kuwa swala hilo linakamilika ipasavyo. kulia ni Mkurugenzi wa operesheni ya Takwimu Bi,  Radegunda Maro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The Guardian Bw, Kiondo Mshana wa kwanza kushoto pamoja na wakurugenzi wengine  wakisikiliza kwa makini mjadala huo.
Mwandishi wa habari kutoka wapo Radio Bw, Willison Kibubu akiuliza swali kwenye mkutano huo.

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetangaza kutoa matokeo ya sensa ya watu na makazi mwishoni mwa mwaka huu.
 Mwenyekiti wa tume hiyo, Hajjat Amina Mrisho alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wamiliki wa vyombo vya habari ambako aliwahakikishia kufanyika kwa umakini mkubwa pamoja na kwamba watachukua muda mfupi wa miezi minne.
Hajjat Amina aliwaondoa hofu wamiliki hao kwa kuwaambia kwamba wasiwe na shaka na muda utakaotumika hadi kutangaza matokeo ya Sensa hiyo kama ilivyokuwa ikifanyika huko nyuma.
Alisema kutokana na Tume hiyo kujipanga vilivyo ndio maana kuna uhakika wa kupatikana matokeo hayo haraka na kwa mafanikio pindi zoezi hilo litakapofanyika Agosti 26 mwaka huu.
“Watu waliolengwa kuhesabiwa katika zoezi hilo ni wale waliolala katika kaya usiku wa kuamkia Siku ya Sensa, na lengo likiwa kupata idadi ya watu wote waliopo nchini ikiwa ni pamoja na kukusanya taarifa za kijamii na kiuchumi,” Alisema.
Aliongeza kuwa kushiriki sensa ni muhimu kwa kuwa kutaipa nafasi Serikali kufahamu mahitaji ya Wananchi wa kila rika, mahali walipo na watu wenye mahitaji maalum.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa elimu kuhusu zoezi hilo, Mwenyekiti huyo aliviasa vyombo vya habari kuweka uzalendo mbele kuliko kulenga maslahi ya kupata matangazo kwanza kutoka kwenye Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Takwimu.
Hata hivyo, Kauli hiyo ilionekana kuzua mjadala kwa baadhi ya wamiliki na wandishi wa habari wa vyombo mbalimbali walioishauri tume hiyo kutobagua baadhi ya vyombo vya habari kwa kuvipa matangazo.
Walisema kwamba uzoefu unaonesha kwamba kumekuwa na tabia kwa Idara za serikali kutoa matangazo kwa kuvibagua baadhi ya vyombo hivyo kitendo ambacho kinawakatisha tamaa.

No comments:

Post a Comment