MAGARI manne yaliyokuwa yamesheheni askari wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) Kanda Maalum ya Tarime na Rorya mkoani Mara, jana
yalivamia hospitali ya wilaya na kisha kutwaa kwa nguvu mwili wa
marehemu Mgosi Magasi Chacha (30), aliyeuawa kwa kupigwa risasi na
askari polisi wanaolinda mgodi wa North Mara uliopo wilayani hapa.
Askari hao wakiwa wamebeba bunduki aina ya SMG, mabomu ya machozi na
virungu, waliwasili hospitalini hapo majira ya saa 5:10 asubuhi na
kuanza harakati za kuchukua mwili huo kwa nguvu, hali iliyozusha vurugu
kubwa kutoka kwa waombolezaji, wakiwemo wazazi wake, mke na viongozi wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambao baadhi yao
walikamatwa.
Waombolezaji hao waliopinga kitendo hicho wakidai kuwa ni
udhalilishaji na ukatili wa hali ya juu, wakitaka taratibu zifuatwe,
walipambana na askari polisi hao waliokuwa wametanda aneo kubwa la
hospitali hiyo, kiasi cha kumlazimu mke wa marehemu kuziba mlango wa
chumba cha kuhifadhia maiti, kuzuia polisi kuuchukua mwili bila ndugu na
yeye kuridhia.
Hata hivyo, polisi walimburuza kwa nguvu kiasi cha kusababisha baadhi
ya nguo zake alizojifunga kudondoka na kumwacha wazi baadhi ya sehemu za
maeneo ya mwili wake, jambo ambalo lilionekana kama ni udhalilishaji
mkubwa.
Kitendo hicho kiliibua hasira kutoka kwa waombolezaji wengi, ambao
walitaka kuanzisha mapambano na polisi, lakini walikumbana na nguvu
kubwa ya jeshi hilo, na baadhi ya wananchi wakiwemo viongozi wa CHADEMA
wilaya walikamatwa.
Waliokamatwa ni Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Tarime, Lucas Ngoto,
Katibu wake, Mroni Mwita pamoja na Diwani wa Kata ya Sabasaba,
Christopher Chometa, huku Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA
(Bavicha), Wilaya ya Tarime, Chacha Heche akiponea chupuchupu kukamatwa
kwa madai ya kutaka kuzuia mwili huo wa marehemu usiondolewe hospitalini
hapo kwenda kuzikwa.
Katika vurumai hiyo iliyodumu takribani dakika 45, polisi walifanikiwa
kuuchukua mwili huo wa marehemu Chacha na kuuondoa hospitalini ukiwa
katika gari la Halmashauri ya Mji wa Tarime lenye namba SM 5241, huku
likisindikizwa na askari hao waliokuwa katika magari namba PT 2036, PT
1873, PT 1863, T 754 BLF pamoja na pikipiki moja ya doria.
Akizungumza kwa uchungu, baba mkubwa wa marehemu, Charles Matiko
alisema kuwa, nguvu kubwa iliyotumiwa na polisi kuchukua mwili wa kijana
wao ni ya kinyama, kwani familia ilikuwa haijaridhia kutokana na ukweli
kwamba mipango ya mazishi ilikuwa haijakamilika.
Chacha aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Nkende na mwendesha pikipiki
wilayani Tarime, aliuawa Juni 4 mwaka huu majira ya saa 1:45 asubuhi,
kwa kupigwa risasi tumboni na askari polisi wanaolinda mgodi wa North
Mara, unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick.
Taarifa ya polisi kanda hiyo maalumu, iliyotolewa na Kaimu Kamanda
Sebastian Zacharia, ilidai kuwa awali Chacha alijeruhiwa kwa risasi
tumboni na askari polisi, kwa madai ya kumkata panga mguu wa kushoto
mlinzi mmoja wa mgodi huo, Winchlaus Petro (26).
“Kabla mauti kumkuta, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi tumboni na askari
polisi waliokuwa doria eneo hilo la mgodi. Alianza kumshambulia askari
kwa panga na kuikata silaha ya askari huyo mara mbili hata baada ya
kuonywa kwa kupiga risasi hewani wakati wa kukamatwa,” ilisema sehemu ya
taarifa hiyo ya polisi yenye kurasa moja.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Nagga Marco
iliiambia Tanzania Daima kwamba, uchunguzi wake umebaini kuwa, Chacha
alipigwa risasi ubavuni karibu na mgongo, kisha ikatokea tumboni.
Kumekuwa na mauaji ya kila mara katika eneo hili la madini, ambapo
mwaka jana vijana watano waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi, na Mei 7
mwaka huu kijana mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mwikwabe, aliuawa
pia kwa risasi.
|
No comments:
Post a Comment