Monday, June 11, 2012

Albino anusurika kuuawa na kundi la watu Missenyi


                            Na Theonestina Juma, Missenyi
MGONJWA wa ngozi (Albino) Bw.Harubu Nusu mkazi wa wilayani Missenyi Mkoani kagera amenusurika kuuwa na kundi la watu waliokuwa wamepanga njama ya kutaka kumteka nyara na kumuua ili kuchukua viungo vyake.
Alibino huyo alinusurika kuuawa Juni 6, mwaka huu wilayani humo, baada ya kupangwa njama ya watu wanne, watatu kutoka wilaya hiumo na mmoja kutoka karagwe ambapo njama hizo ziliweza kupanguliwa na Jeshi la polisi Mkoani hapa baada ya kupata taarifa hizo mapema.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani hapa, Philip Kalangi, watu wanoshikiliwa kuhusika na njama hizo  ni pamoja na  Bw. Gaison Galela (50) Mnyarwanda mkazi wa Karagwe.
Wengine ni pamoja na Bw. Njenwa Charles (50), Bw. Byamungu Felician (53) na Bw. Masanja Mabula (40) wote wakazi wa Mutukula wilayani humo.
Kamanda Kalangi alisema kutokana na Jeshi la polisi kupata taarifa mapema juu ya njama za kumtaka kumuua albino huyo, kupitia Mkuu wa upepelezi wa makosa ya jinai wa mkoa Kagera, Bw. Peter Matagi aliandaa mtego kwa kuwatumia askari wake ambao walifanikiwa kuwakamata watu hao .
Alisema miongoni mwa watu waliokamatwa Bw. Galela alikamatiwa katika wilayani Chato mkoani Geita akiwa ameenda  kutafuta mganga wa kienyeji.
Kutokana na tukio hilo ambalo ni la mara ya kwanza kutokea mkoani hapa tangu mwaka huu uanze Kamanda huyo amewataka wakazi wa mkoani hapa kuachana na imani za kishirikina kwani hakuna utajiri unaopatikana kupitia walemavu wa ngozi na kwamba wasidanganyike  na waganga wa kienyeji walio na tamaa ya kujipatia pesa za haraka haraka.
Aidha amewataka wananchi pindi wanapowaona watu wenye mienendo ambayo wanayatilia shaka watoe taarifa mapema ili jeshi liweze kujipanga vyema kukabiliana na nao.
Watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakato wowote mara baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika.
Mwisho

No comments:

Post a Comment