Na Theonestina Juma, Kagera
RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kujihadhari na baadhi ya watu wanaotaka kuwagawa watu katika misingi wa kidini na kusababisha nchi kutumbukia katika vitendo vya kuuana wenyewe kwa wenyewe.
Rais Kikwete ametoa kali hiyo jana wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku sita mkoani hapa.
Rais Kikwete alisema kuna baadhi ya watu wachache ambao  hawafurahishwi na jinsi Watanzania wanavyoishi bila vurugu zozote na hivyo hawaoni raha.
“Mnajua katika jamii hii, kuna sampli nyingi sana , kuna  baadhi ya watu  mazingira ya utulivu haiwapi raha , wanabaki kujiuliza hivi ni kwa nini kumetulia, wapo … msikubali kuwapa nafasi sampli hii watawavuruga kweli , mkishavurugana ndiyo furaha yao, kwa kawaida wapenda vurugu huwa na sauti kubwa.. wanapiga kelele na sauti zao zina mwangwi mkubwa kweli”alisema
Alisema wapo wapenda amani wengi hapa nchini lakini kupitia utofauti wa dini kamwe wasikubali kutoa nafasi hata kidogo.
Watu hao mambo ambayo hayana msingi kwa kawaida yao huyakuza ili yawe makubwa na kuleta uvunjivu wa amani miongoni mwa wananchi,hasa katika sakata lililoibuka kuwa ni nanianastahili kujinja.
“Hivi nyie mnadhani , kuwa wazee wetu wa zamani walioamua kuweka mambo hayo yawe hivyo walikuwa hawafai …walijua… ndiyo maana amani imedumu miaka yote katika nchi hii”alisema.
Alisema watu wengi kutoka nchi tofauti mara nyingi hujiuliza ni kwa nini Tanzania haina matatizo ya amani na utulivu , hawana ugomvi na nchi yoyote, wala wa kijeshi, watu hao wanataka Tanzania ifanane na nchi zingine ambazo ziko kwenye vita.
“Kwa nini hatunanani nao, wanaona kikabila haiwezekani, kwa sasa wanaota ni kidini ndiko kunawezekana, Watanzania wenzangu tusipotanabahi hii, tutauana bure kwani ugomvi wa kidini biblia itabaki bibblia na Quarani itabaki hivyo hivyo, wala haitakuwa na ukurasa mpya utakaoandikwa leo kwani wakristo walikuwapo tangu miaka 200 iliopita vivyo hivyo kwa Waislamu kwa nini wagombane leo kuna kitu hapa”alisema
Hata hivyo alionesha kusikitishwa na baadhi ya viongozi wa dini nao kushindwa kutanabahi hilo jambo  badala yake baadhi yao wanazidi kuenesza chuki.
Alisema watu  ambao hawaitakii mema Tanzania ameona kuwa kupitia dini ndiko kunaweza kuivuruga nchi hivyo, hivyo viongozi wa dini wasikubali kuwapatia nafasi.
“Kamwe msikubali kucheza ngoma ambayo siyo yetu,hawataiweza, mimi niko leo na miaka mitano  ijayo sijui nitakuwepo, na nitaendelea kusema kwani nikisema kuna baadhi ya waislamu wanaonichukuia vivyo hivyo kwa wakristo lakini nitawaambia kuwa hii ni mbaya”alisema
Aidha alisema mbaya zaidi suala la dini kwa sasa linatumbukizwa katika siasa, ndiko wanakopeleka, watu wanatengeneza wafuasia wa wanasiasa wawe wa dini yake pekee nchi haiwezi kuwa na amani.
“Huko wanakopeleka nchi siko, nchi itakuwa na matatizo makubwa iwapo hayo tutayaendekeza, jambo ambalo Watanzania wengi wanalikataa’alisema.
Alisema vitu hivyo havina maana wala faida kwa jamii, na bali waache watu wajigawe kwa kufaa kuwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi na sio kuingiza shughuli za dini katika siasa, na matokeo yake wataka wakuu wa wilaya nusu wawe wakristo nusu waislamu vivyo hivyo katika idara zote za serikali jambo ambalo haliwezekaniki.