Saturday, June 23, 2012

Taarifa ya simba sport klabu kwa vyombo vya habari


  • KLABU ya soka ya Simba imepokea kwa furaha taarifa kwamba Rais wa Shirikisho la Mpira was Miguu Tanzania (TFF), Leodger Chila Tenga, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusiana na namna mchezaji wa Simba na Taifa Stars, Kelvin Patrick Yondani, alivyoondoka kambini usiku wa kuamkia Juni 7 mwaka huu.
    Katika barua ambayo Tenga ameiandikia Simba, ameahidi kwamba uchunguzi utafanyika katika maeneo makuu mawili. Mosi, iwapo ni kweli Yondani aliondoka kambini usiku, pili iwapo aliondoka kwa ruhusa maalumu au alitoroka. Tenga ameahidi kwamba kama ikibainika kwamba aliondoka bila ruhusa, basi hatua zitachukuliwa kwa wote waliohusika chini ya taratibu za maadili kwa wachezaji (Players Code of Conduct).
    Kutokana na kauli hiyo ya Tenga, uongozi wa Simba umeamua sasa kwamba hautozungumza lolote kuhusiana na masuala ya Yondani. Tayari timu imewasilisha vielelezo vyake TFF na kote kwingine ambako suala hilo linaweza kufika. Kilichobaki sasa ni kusubiri vyombo husika vifanye kazi yake.
    Simba SC inapenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wapenzi na wanachama wake kutulia na kutobabaishwa na taarifa za wachezaji wake kusajiliwa na timu nyingine. Kwa sasa Simba inaendelea na mikakati yake ya usajili unaokidhi vigezo vya kimataifa ambao ulisababisha msimu uliopita itwae ubingwa wa Tanzania na kuifunga YANGA goli 5-0 !
    Simba si timu ya maneno mengi kwenye usajili bali ni vitendo. Tunaomba wanachama wetu watulie na mara ifikapo tareje 15 Juni mwaka huu, mbivu na mbichi zote zitajulikana. Siku hiyo, Simba itatangaza wachezaji wake wote iliyowasajili na iliyowaacha.

    Simba ndiyo mabingwa wa Tanzania na washabiki wake wanatakiwa kutembea vifua mbele popote pale walipo na wasichanganywe na taarifa za pembeni.

    Uongozi wa Simba uko makini na unafanya kazi zake kisayansi.
    Imetolewa na:

    Ezekiel Kamwaga
    Ofisa Habari
    Simba SC

No comments:

Post a Comment