Na Theonestina Juma, Bukoba
WAANDISHI wa habari Mkoani Kagera wametakiwa kuwa makini katika kuelimisha
jamii juu ya rushwa kutokana vitendo hivyo huathiri zaidi wananchi masikini kwa kushindwa kupata
haki zao.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Bw.
Samuel Kamote wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya waandishi wa habari
wanachama wa Kagera Press Club (KPC) wapatao 34 yanayodhaminiwa na
Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) yanayofanyika mjini
Bukoba.
Alisema kutokana na vitendo vya rushwa huathiri zaidi
wananchi masikini kwa kuwakosesha kupata haki zao, hivyo waandishi wa habari wanalo jukumu na nafasi kubwa ya kuelimisha
wananchi kuhusu wajibu na namna ya kuepuka rushwa.
Alisema jamii inategemea waandishi wa habari kupitia vyombo vyao
vya habari kupata ufafanunuzi mbali
mbali ya rushwa, na hivyo wanatakiwa kuwa makini wanapoandika masuala ya rushwa ambayo yasipoandikwa na kutangawa kwa usahihi,
yanawachang’anya wananchi.
Aidha Bw.Kamote aliwataka waandishi hao kuwa waadilifu na
waaminifu pindi wanapoandika habari zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Halikadhalika aliwasihi wanahabari hao kutoingilia kesi ambazo zinachunguzwa na TAKUKURU kwa vile kufanya hivyo huathiri
mwenendo mzima wa uchunguzi wao.
Pia alisema waandishi hao wanatakuwa kujielimisha zaidi na
kufahamu vizuri sheria za kupambana na kuzuia rushwa ya mwaka 2007.
Aidha kwa upande wa Kamanda wa TAKUKURU Mkoani Kagera, Bi.
Domina Mukama alisema lengo la mafunzo hayo ni kukuza uelewa kwa waandishi wa
habari juu ya rushwa ili kuweza kufahamisha umma juu ya suala hilo.
Alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mipango ya TAKUKURU
katika kushirikiana na vyombo vya habari
ili kuwawezesha waandishi wa habari kuandika kwa usahihi taarifa zinazohusu
rushwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment