Thursday, May 17, 2012

Kuwaona Twiga Stars na Banyana Banyana ni Buku

Baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars
KIINGILIO kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) na Afrika Kusini (Banyana Banyana) itakayochezwa Jumapili (Mei 20 mwaka huu) ni sh. 1,000.
Mechi hiyo ambayo ni sehemu ya maandalizi kwa timu hizo zinazoshiriki mashindano ya Afrika itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni. Viingilio hivyo ni kwa maeneo yote, isipokuwa VIP A ambapo itakuwa sh. 10,000 na VIP B sh. 5,000.
Baada ya mechi hiyo, Twiga Stars itakwenda Ethiopia kwa ajili ya mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) itakayochezwa Mei 27 mwaka huu jijini Addis Ababa.
Tayari Meneja Usalama wa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA), Percy Makhanya ameshawasili nchini kuratibu ujio wa Banyana Banyana. Timu hiyo pia iko katika kinyang’anyiro cha kutafuta tiketi ya Fainali za Nane za AWC ambapo katika raundi hii ya pili imepangiwa Zambia na itaanzia mechi hiyo ugenini jijini Lusaka.

No comments:

Post a Comment