Kikosi cha Simba kilichotwaa ubingwa leo kikiwa kambini Zanzibar, baada ya Mtibwa Sugar kuituliza Azam kwa kichapo cha mabao 2-1 |
SIMBA leo wanaanza
kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya Azam FC
kufungwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Simba ina pointi
59, ambazo sasa haziwezi kufikiwa na timu yoyote msimu huu na imebakiza mechi
moja dhidi ya watani wa jadi, Yanga Jumapili ambayo kwao itakuwa ya kulinda
heshima tu.
Lakini Azam tayari
imejihakikishia nafasi ya pili kwenye ligi hiyo na hivyo kukata tiketi ya
kushiriki Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwakani.
Waliokuwa mabingwa
watetezi Yanga, hawana tena chao- kwani hata wakiifunga Simba keshokutwa
watabaki nafasi ya tatu tu, hivyo mwakani hawavuki mipaka ya nchi.
Tumaini pekee la
Yanga kucheza michuano ya Afrika mwakani ni iwapo Simba SC itaingia hatua ya
makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu- ikiwa imebakiza mitihani miwili
kufikia mafanikio hayo.
Inatakiwa kuitoa Al
Ahly Shandy ya Sudan- na baadaye iitoe timu itakayokutana nayo kwenye mchujo wa
kuwania kucheza hatua hiuyo, ambayo itakuwa imetolewa kwenye Ligi ya
Mabingwa.
Hapo, Tanzania
itakuwa na nafasi mbili kwenye Kombe la Shirikisho mwakani, kwa mujibu wa kanuni
mpya za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Tayari Simba
imeifunga Shandy mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza na inahitaji sare katika
mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kusonga mbele.
Katika mchezo wa
leo, hadi mapumziko, tayari Mtibwa walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0 lililowekwa
kimiani na Awadh Issa dakika ya 25, wakati kipindi cha pili, Wakata Miwa hao wa
Manungu waliokuwa wanashangiliwa kwa nguvu na mashabiki wa Simba, walipata bao
la pili dakika ya 59, mfungaji akiwa ni Juma Abdul.
Awadh alifunga bao
lake akiunganisha kona iliyochongwa na nyota wa mchezo wa leo, Juma Abdul ambaye
naye alifunga bao la pili kwa
mpira wa adhabu, baada ya Luckson Kakolaki kumchezea rafu Vencent Barnabas
Saramba.
SOURCE: BIN ZUBEIRY
(http/bongostaz.blogspot.com)
No comments:
Post a Comment