Thursday, May 3, 2012

Msitumie fedha za wakulima kupelekeana mahakamani-RC Massawe


 Bukoba
VYAMA vya Ushirika mkoani Kagera vimetakiwa kuacha mara moja kujihusisha na kesi mbalimbali zinazoweza kuvizoofisha vyama hivyo , kutokana na  fedha za wanachama ambao ni wakulima waliowengi ndiyo hutumika kuendesha kesi hizo mahakamani.
Karipio hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa Kagera, Kanali Fabian Massawe katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Ushirika mkoani Kagera  (KCU) 1990 Ltd uliofanyika  jana mjini hapa.
Alisema wanachama wa vyama vya Ushirika wa mkoani hapa, wanatakiwa kuacha tabia ya kufikishana mahakamani pindi inapotokea migogoro na badala yake, wawe na desturi ya kusuluhishana ili kuweza kuleta maendeleo ya ushirika.
Alisema fedha zinazotumika katika kuendeshea kesi mahakamani ambazo ni za wakulima walio wengi wa ushirika huo, zielekezwe kwa wakulima ili kuleta tija na pato la wakulima hao.
 “Msiwe na tabia ya kupelekeana mahakamani, ambao huwanufaisha watu wengine, badala ya kushughulikia kazi za maendeleo, mnabaki kulumbana mahakamani, hakuna tija kwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wenu kuyatatua kama ni tofauti zenu”alisema.
Mkutano huo wa KCU 1990 Ltd ulikuwa ni kufunga mwaka wa msimu wa mwaka 2011/2012 na kufungua msimu mpya wa kununua kahawa wa 2012/13, pia kupisha makisio ya msimu mpya wa kununua kahawa ambao mkutano huo ulienda sambamba na kufanyika uchaguzi  mkuu .

Mwisho.

No comments:

Post a Comment