Mchezaji wa kimataifa Patrick Mafisango wa Simba
SC enzi za uhai wake akisakata kabumbu.
Patrick Mafisango (kwenye picha ndogo) enzi za uhai
wake. Juu ni gari aliyopata nayo ajali. Picha na Bin Zubery Blog
MCHEZAJI wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) na timu ya
Simba Patrick Mutesa Mafisango (32), amefariki dunia jana alfajiri kwa ajari ya
gari.
Amepata ajali hiyo akitokea kwenye Ukumbi wa Starehe wa Club Maisha uliyopo
Masaki. Akizungumza Dar es Salaam leo, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba
Geofrey Nyange Kaburu, alisema Mafisango alikubwa na mauti hayo eneo la Keko
jirani na Chuo cha VETA jijini Dar es Salaam.
Alisema Mafisango amekufa kwa ajali ya gari, baada ya gari alilokuwa
anaendesha kuacha njia na kugonga mti ulio pembezoni mwa barabara ya Chang’ombe
majira ya saa kumi kasorobo alfajiri na kufariki papo hapo.
Kaburu ameongeza gari hilo ndani lilikuwa na abiria wengine wanne, lakini
aliyekutwa na mauti baada ya ajali ni Mafisango pekee. Alisema mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari kwa kusafirishwa kwenda
kwao Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako atazikwa.
Kaburu alisema ingawa alikuwa na uraia wa Rwanda na akiichezea timu ya taifa
ya nchi hiyo (Amavubi), Mafisango alikuwa ni mzaliwa na raia wa DRC na uamuzi wa
kuzikiwa huko ni wa familia yake. Msiba wa Mafisango uko katika eneo la Keko
Toroli jirani na kituo cha Chang’ombe Maduka Mawili eneo la njia Panda ya
Sigara.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa kesho Ijumaa saa nne asubuhi katika
viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam kabla ya mwili
wake
kusafirishwa kwenda Kinshasa majira ya saa kumi jioni.
Mafisango alizaliwa Machi 30, 1980 huko Kinshasa Zaire wakati huo na ameacha
mke na mtoto mmoja wa kiume, Chris Paul, mwenye umri wa miaka
mitano.
Mafisango ameichezea Simba kwa msimu mmoja tu akitokea Azam ya Dar es
Salaam lakini kabla ya hapo alichezea pia TP Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda na
pia aliwahi kuwa nahodha wa Amavubi kwa takribani miaka mitano.
Mara baada ya taarifa hiyo wanachama wa klabu ya Simba na wachezaji walipatwa
na mshtuko mkubwa ikiwa ni pamoja na kuamua kwenda Muhimbili
kuhakikisha kama
ni kweli mwenzao huyo amewatoka.
Miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa karibu na Marehemu kama marafiki ni
Haruna Moshi Boban ambaye yupo kwenye kambi ya timu ya Taifa, Taifa Stars
alishindwa hata kufanya mazoezi na kuomba apewe nafasi ya kwenda kushuhudia
mwili wa mchezaji mwenzake katika chumba cha maiti.
Boban ambaye watu wamemzoea kumuona akiwa kimya alionekana mwenye uzuni
nyingi kwa kulia moja kwa moja huku akiomba apewe nafasi ya kushuhudia mwili wa
mpendwa wake huyo. Wengine ni haruna Niyonzima, ambaye anaichezea Yanga, Uhuru
Suleman ambao walionekana wakishindwa kuvumilia.
Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa
masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi),
Patrick Mafisango kilichotokea jana alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ajali ya
gari Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa jana na ofisa habari wa TFF Boniface Wambura, alisema
kuwa msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa
kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye
Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.
Kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali
ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri
uwanjani. Wakati mauti inamkuta, Mafisango alikuwa ameitwa Amavubi kwa ajili ya
mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika zinazochezwa mapema mwezi
ujao.
TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira
wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali
pema peponi.
Habari hii ni kwa hisani ya Gazeti la Jambo Leo
No comments:
Post a Comment