Thursday, May 31, 2012

Pinda kumwakilisha Rais JK Angola

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda anaondoka Dar es Salaam leo mchana (Alhamisi,  Mei 31, 2012) kwenda Luanda, Angola kuhudhuria kikao cha Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Mkuu Pinda anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye leo anatarajiwa kufungua mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) huko Arusha.
Mara baada ya kuwasili,  leo jioni Waziri Mkuu atahudhuria kikao cha TROIKA ambacho kinajumuisha Wakuu wa Nchi kitakachofanyika Ikulu ya nchi hiyo na usiku atashiriki hafla maalum iliyoandaliwa kwa viongozi wakuu wa nchi za SADC.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za SADC ambao umepangwa kufanyika kesho (Juni Mosi, 2012), utatanguliwa na mkutano wa mawaziri unaoanza leo (Alhamisi, Mei 31, 2012) chini ya uenyekiti wa Waziri ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe.

Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea jijini nchini kesho kutwa (Jumamosi, Juni 2, 2012).

No comments:

Post a Comment