Saturday, May 5, 2012

Massawe- Kagera tunao maprofesa 540 tunawataka warudi kuwekeza kwao.


Na Theonestina Juma,Bukoba
WAANDISHI wa habari mkoani Kagera wametakiwa kuandika habari za vivutio vinavyopatikana mkoani hapa ili kuwezesha kuwavutia kwanza wazaliwa wa mkoani hapa wanaoishi nje kurejea kuwekeza.
Rai hiyo imetolewa leo usiku na Mkuu wa Mkoa Kagera, Kanali Fabian Massawe katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani mkoani hapa,ulioandaliwa na Chama cha Waandishi Mkoani kagera, (KPC) na kudhaminiwa na Umoja wa vilabu nchini (UTPC) ambapo Kanali Massawe alikuwa mgeni rasmi.
Kanali Massawe amesema, ni jukumu la waandishi wa habari kuandika habari za kuchochea maendeleo ya mkoa wa Kagera ili kuwavutia kwanza wazaliwa wa mkoa huu wanaoishi nje ili kurudi kwao kuwekeza.
“Mkoa huu nimepiga mahesabu yangu, unajumla ya Maprofesa 540, hawa wanahitajika kurudi Kagera kuwekeza na ili warejee, ni jukumu lenu nyie waandishi kuandika habari za vivutio na hali ya mazingira mkoa huu, ulivyo ili waweze kurejea”alisema Kanali Massawe.
Amesema mkoa wa Kagera umesheni ardhi nzuri yenye rutuba , misitu, mito, ziwa pamoja na hifadhi za akiba ambazo kwa sasa wako katika harakati za kuziboresha ili kuwa mbuga za wanyama kwa vile kuna wananyama  kama twiga wanaoishi humo  pamoja na soko la Jumuia ya Afrika Mshariki ambapo nchi takribani zote zinazounganisha jumuiya hiyo zinapakana na Mkoa huu.
Pia amewataka waandishi wahabari kujikita zaidi katika habari za uchunguzi ili kuweza kuibua matatizo ya jamii  kama la rushwa ili kuwezesha serikali kuchukua hatua zaidi.
Halikadhalika waandishi hao wanapaswa kutumia kalamu zao kuandika habari za kujenga jamii na si za kuleta machafuko kwani bila amani hakuna maendeleo.
Katika maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbali mbali wa habari mkoani hapa, akiwemo kamanda wa TAKUKURU Mkoa  Kagera, Domina Mukama,Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Vitus Mlolere, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Samuel Kamote na Mwenyekiti wa Mstaafu CCM Mkoa , Bw. Pius Ngeze.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment