Friday, December 7, 2012

Ukatili wa Kijinsia Kagera, ubakaji washika kasi, wanawake 306 wabakwa ndani ya miezi 11 tu



Na Theonestina Juma, Kagera
ZAIDI ya makosa 600 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa kutokea  mkoani Kagera kwa kipindi Januari hadi Novemba mwaka huu.
 Hayo yamebainishwa jana (leo) na Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Phillip Kalangi wakati wa maandhimisho ya 16 ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yaliofanyika mjini hapa na kutanguliwa na maandamano yaliofanyiwa na baadhi ya askari kuzunguka katika barabara mbali mbali za mjini Bukoba.
Kamanda Kalangi alisema  “jumla ya makosa 612 ya ukatili wa kijinsia yametokea mkoani hapa kwa kindi cha miezi 11 tu mkoani hapa, kutokana na ukubwa wa tatizo lenyewe tunapambana nalo kutokana na kuwa ni uhalifu kama mwingine”.
Alisema kwa kipindi hicho, kesi za ubakaji zilikuwa 306, ulawiti 12, shambulio ama vipigo 135, utoroshaji wa wanafunzi wa kike 18, utelekezaji wa familia 96, ukatili dhidi ya watoto 20 na kuwapa mimba wanafunzi 25.
Alisema katika makosa hayo, kesi 170 zilifikishwa mahakamani , ambapo kesi zilizopata mafanikio ni 50 huku kesi 80 zikikosa mafanikio ambapo kesi 56 ziko chini ya upelelezi.
Alisema Makosa ya ukatili ya kijinsia  ni kero kubwa ndani ya jamii kwani yanatishia usalama na maendeleo ya mkoa wa Kagera.
Alizitaja baadhi ya makosa hayo ni pamoja na mauaji, vipigo, kuwapa mimba wanafunzi, shambulio la aibu pamoja na mengine mengi na kutokana na suala hilo, kwa sasa limetolewa fomu pya  maarufu kama ya PF3 kwa ajili ya kutolewa ripoti tofauti na ile ya awali, ambayo haikuonesha sehemu ya kujaza tukio alilotendewa mtu mfano kama ya ubakaji na shambulio la aibu.
Aliwataka watu wote kuungana  pamoja kwa kutumia mikakati wa polisi jamii ama ulinzi shirikishi kuhakikisha wanadhibiti vitendo hivyo vya unyanyasaji.
Awali akisoma taarifa ya dawati la watoto na jinsi la jeshi hilo mkoani hapa, Mwekazina wa dawati hilo, Bi. Grace George alisema kuwa  wanakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na wanajamii ama waathirika wa ukatili huona kuwa ukatili ni sehemu yao ya maisha hivyo hawaripoti matendo maovu wanyotendewa.
Alisema  mtizamo wa jamii imekuwa hasi na jeshi la polisi hivyo huogopa  kufika kituo cha polisi kuelezea ukatili wa kijinsi wanaotendewa.
Halikadhalika alibainisha kuwa ushirikiano mdogo kwa jamii kutoa ushahidi juu ya ukatili walioshuhudia ukitendewa dhidi ya wanajamii wenzao, hivyo hukwamishwa upepelezi na mafanikio ya mashauri hayo mahakamani.
Bi. George alisema kitu kingine ni kesi nyingi za ukatili wa kijisnia husuluhishwa katika ngazi ya kifamilia hivyo ukatili kutoripotiwa kituoni na kusababisha vitendo hivyo kuzidi kuongezeka.
Naye  mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambaye alikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa Kagera, Nassoro Mnambila ambaye alizidia PF3 mpya  alisema ukatili wa jinsia, kwa kiasi kikubwa umekuwa ukigusa ama kuathiri kundi la wanawake  zaidi kutokana na wao ndiyo wanaoongoza kwa kufanyiwa unyanyasaji ambao una madhara makubwa ndani ya jamii.
Alisema “vitendo hivi kwa  kwa ujumla vinadhoofisha afya, uwezo wa jamii katika kuchangia maendeleo yan uchumi ndani ya familia na hatimaye kwa nchi nzima hivyo huchelewesha jitihada za serikali kupunguza umaskini na kukuza uchumi katika nchi yetu na kushindwa kufikia malengo la Milenia”.
Alisema kutokana navitendo hivyo, kama unyanganyaji wa mali, kuridhi mali ndiyo sababu inaamusha amri ya kuanza kupambana na usawa wa kijinsia.
Alisema serikali imekuwa ikifanya juhudi nyingi za kupambana na ukatili wa kijinsia ambapo ni pamoja na kuandaa mpango mkakati wa  kuzuia na kupambana matatizo hayo pamoja na kutunga sera za wanawake na kurekebisha baadhi ya sheria.
Mwisho

No comments:

Post a Comment