Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) itacheza nusu fainali ya
michuano ya Kombe la Chalenji 2012 Alhamisi (Desemba 6 mwaka huu) kwenye Uwanja
wa Mandela ulioko Namboole jijini Kampala, Uganda.
Kilimanjaro Stars ambayo itacheza
mechi hiyo na mshindi wa robo fainali ya inayochezwa leo
kati ya wenyeji Uganda na Ethiopia imeingia hatua hiyo baada ya kuitoa Rwanda.
Mechi imechezwa leo (Desemba 3 mwaka huu) Uwanja wa KCC ulioko Lugogo,
Kampala.
Mabao ya Amri Kiemba dakika ya 33 na John
Bocco dakika ya 53 ndiyo yaliyoifanya Kilimanjaro Stars itinge nusu fainali na
kuifungisha virago Rwanda (Amavubi) inayofundishwa na Milutin ‘Micho’ Sredojovic
kutoka Serbia.
Vijana wa Kilimanjaro Stars wanaonolewa
na Kim Poulsen walitawala pambano hilo, hasa kipindi cha kwanza kwa pasi fupi
fupi. Kilimanjaro Stars imefungwa bao moja katika mechi nne ilizocheza tangu
michuano hiyo ilipoanza Novemba 24 mwaka huu jijini Kampala.
Kilimanjaro Stars ambayo katika michuano
hiyo iliyofanyika Dar es Salaam mwaka jana iliishia hatua ya nusu fainali
iliwakilishwa na; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomari Kapombe,
Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Salum Abubakar/Athuman Idd, Frank Domayo, Mwinyi
Kazimoto, John Bocco na Mrisho Ngasa.
No comments:
Post a Comment