MSANII maarufu nchini, Elizabeth Michael (Lulu),
anayekabiliwa na mashitaka ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven
Kanumba, amedai mahakamani kwamba walikuwa wapenzi, walipendana sana lakini
hawakuaminiana.
“Siku mbili kabla ya kifo chake alitabiri kifo hicho kwani alinitumia ujumbe
unaosema, nitakufa kwa ajili yako, nakupenda sana,” hayo yalikuwa maneno ya Lulu
aliyoyatoa Polisi wakati akihojiwa.Muhtasari huo wa ushahidi ulisomwa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Augustino Mmbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kweka alidai, Sajenti Revonatus aliyechukua maelezo ya Lulu baada ya tukio, alidai lulu alianza uhusiano wa mapenzi na Kanumba Junuari mwaka huu, katika uhusiano wao walikuwa wanagombana kama mtu atapokea simu ya mwenzake.
Alidai Lulu wakati akiwa Mikocheni kwa rafiki yake Ritha, kabla ya kutoka akampigia simu mpenzi wake Kanumba na kumwambia kuwa anataka kutoka, alipofika nyumbani kwa Kanumba alimkuta anazungumza na simu.
Lulu alidai na yeye alipigiwa simu na rafiki yake wa kike, alipotaka kwenda kupokea simu nje Kanumba alimzuia asitoke nje na yeye alitoka nje na ndipo Kanumba alipomkimbiza mpaka barabarani.
Alipomshika akaanza kumpiga makofi na mateke, walipoingia ndani, Kanumba alimtupa kitandani na kuchukua panga chini ya kitanda kisha kuanza kumpiga na ubapa wa panga katika mapaja yake.
“Lulu alikubali kutoa maelezo hayo akiwa peke yake na kwamba alikuwa huru katika uhusiano wake na Kanumba, kwani alikuwa anaenda kulala kwake kila alipokuwa akijisikia kufanya hivyo, lakini hawakuwahi kuishi pamoja.
“Aprili 5 mwaka huu usiku, Kanumba alimtumia ujumbe kuwa ‘you will kill me soo, I love you so much, akamfariji kwa kumwambia kuwa achana na mambo hayo na akawa sawa.
“Tarehe 6, Kanumba alimpigia simu na kumwambia anatarajia kusafiri kwenda Marekani April 14, mwaka huu amletee zawadi gani naye akamjibu zawadi yoyote,” alidai Kweka wakati akisoma muhtasari wa ushahidi.
Alidai walikuwa wanapendana lakini hawaaminiani wakiwa mbali, kwani Kanumba alikuwa na wivu wa kimapenzi na alikuwa anasema anamdharau.
Mshitakiwa alidai hakumsukuma Kanumba, Kanumba alivyompiga na ubapa wa panga alilitupa chini na kuanza kuhema kwa hasira ambazo hakuwahi kuona tangu wawe wapenzi.
Alidai mshitakiwa alijigonga kisogoni katika ukuta na kuanguka chini, lakini alipomuona kama anataka kunyanyuka, alikimbilia chooni na kujifungia ndani, baada ya muda aliona Kanumba anatokwa na povu ndipo alimwagia maji na kutoka nje kwenda kumwita mdogo wake Seth.
Lulu alipopewa nafasi ya kusema chochote katika Mahakama ya Kisutu, alisema hana chochote cha kusema.
“Nawatakia mafanikio mema huko Mahakama Kuu katika kesi hii, nawashukuru mawakili wote, waandishi wa habari na wananchi wote ambao tumeshirikiana pamoja, Lulu utarudi gerezani mpaka utakapoitwa Mahakama Kuu,” alisema Hakimu Mmbando.
Upande wa Jamuhuri utawasilisha mashahidi tisa na vielelezo vya ushahidi wa ramani ya eneo la sehemu alipofia Kanumba, ripoti ya ukaguzi wa daktari na maelezo ya onyo ya Lulu aliyopewa.
Mawakili wa utetezi ni Fuljensi Masawe, Kenedy Fungamtama na Peter Kibatala.
No comments:
Post a Comment