Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa Kimataifa wa wadau
wa chanjo Duniani “Global Alliance for Vaccine and Immunisation (GAVI) Partners
Forum. Mkutano huo utafanyika mjini Dar es Salaam kuanzia tarehe 5 hadi
7 Disemba 2012.
Mkutano unatarajia kuwa na washiriki
wapatao 600 kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwemo Wake wa Marais, Mawaziri wa
Afya, Fedha na watu mashuhuri kutoka nchi 73 zinazohisaniwa na
GAVI.
Lengo la mkutano huu ni pamoja na kujadili
mafanikio na changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma za chanjo duniani.
Mkutano huo ni wa kwanza kufanyika katika bara la Afrika na ni wa tano duniani
tangu kuanzishwa ushirika wa wadau hao wa GAVI. Mikutano kama hii ilishafanyika
katika nchi za Netherland (2000), Senegal (2002), India (2005) na Vietnam
(2009).
Sababu ya mkutano huu kufanyika nchi
Tanzania ni pamoja na nchi yetu kuonyesha mafanikio makubwa katika utoaji wa
huduma za chanjo za watoto na akina mama wajawazito. Hivyo basi washiriki
watapata fursa ya kutembelea vituo vinavyotoa huduma za chanjo nchini ili
kujionea mafanikio, changamoto zilizopo pamoja na kujifunza.
Aidha, katika mkutano huo, washiriki
watapata fursa ya kujadili masuala ya chanjo ikiwemo uingizwaji wa chanjo mpya
na masuala ya afya ya mama na mtoto. Pia washiriki watapata nafasi ya
kubadilishana uzoefu kutoka nchi zao jinsi ya uanzishaji wa chanjo mpya,
utengenezaji, uhusishwaji wa viwanda vya chanjo, pamoja na mikakati ya kuboresha
huduma za chanjo katika nchi mbalimbali. Aidha, kutakuwa na mkusanyiko wa
wataalam wa huduma za chanjo, wafanyabiashara mashuhuri na viongozi mbalimbali
ambao kwa ujumla wao huhusika sana katika maamuzi ya utoaji wa huduma za
chanjo
Mkutano huo wa siku tatu utafunguliwa
rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
tarehe 5 Desemba, 2012. Kutakuwa na uzinduzi wa chanjo mbili mpya za magonjwa ya
Kuhara , Nimonia na homa ya Uti wa Mgongo kwa watoto (Pneumoccocal na Rotavirus
vaccines) chini ya mwaka mmoja) ambazo zitatolewa hapa nchini kwa uhisani wa
GAVI. Chanjo hizo zinatarajiwa kuanza kutolewa mapema mwezi ujao nchi
nzima.
Imetolewa na:
Regina L. Kikuli
KAIMU KATIBU MKUU
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA
JAMII
04/12/2012
No comments:
Post a Comment