Wajasiriamali kutoka Zanzibar, wakiwaonesha wananchi
waliotembelea banda la Tanzania tarehe 3/12/2012 jinsi ya kutengeneza sabuni ya
maji kwenye maonesho ya 13 ya Nguvu Kazi/Jua kali yanayoendelea katika viwanja
vya Musee Vivant mjini Bujumbura.
……………………………………………………..
Maonesho ya 13 ya Nguvu Kazi/Jua kali
yameanza tarehe 2/12/2012 katika viwanja vya Musee Vivant mjini Bujumbura
Burundi.
Nchi ya Burundi imeandaa
maonesho haya kwa mara ya kwanza baada ya nchi za Burundi na Rwanda kujiunga na
Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2007.
Idadi ya wajasiriamali 700 wanashiriki
maonesho haya ambapo Tanzania imepewa nafasi 185, Kenya nafasi 185, Uganda
nafasi 70, Rwanda nafasi 60 na mwenyeji Burundi imepewa nafasi 200.
Maonesho haya ni mojawapo ya njia muhimu
za kuwajengea uwezo wananchi walio katika ngazi za chini kabisa katika
ujasiriamali.
Akiongea katika viwanja vya maonesho haya,
Mwenyekiti wa muda wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Tanzania (CISO-T)
ambaye pia ni mjasiriamali wa muda mrefu, Bibi Lida Msaki anasema maonesho haya
yana faida kubwa sana kwa wajasiriamali.
Bibi Msaki anasema yeye ameshiriki
maonesho haya tangu yanaanza mwaka 1999 na ameweza kufahamiana na watu wengi
ikiwa ni pamoja na wajasiriamali wa Afrika Mashariki, amepata ujuzi wa jinsi ya
kuboresha bidhaa zake, kubadilishana ujuzi, vile vile ameweza kuuza bidhaa zake
kwa wingi na kuweza kujiongezea kipato kikubwa sana.
Bibi Msaki anatoa wito kwa wajasirimali
kuwa wasiogope na wasivunjike moyo katika kushiriki maonesho haya ili waweze
kupanua uwigo wa bidhaa zao.
Ameishukuru Serikali kwa kuweza kuona
umuhimu wa wajasiriamali na kuwa nao bega kwa bega kwa kutoa msaada mkubwa sana
kwao wa kusafirisha bidhaa zao na kuweza kufika salama kwenye maonesho bila
bugudha yoyote.
Anasema Serikali imetoa mchango mkubwa
sana katika kuwasaidia wajasiriamali maana bila Serikali wasingefika hapo walipo
sasa.
Ameiomba Serikali izidi kuwasaidia
wajasiriamali hasa katika kuboresha bidhaa zao ili ziwe zenye ubora zaidi hasa
kwa upande wa vifungashio
Mjasiriamali kutoka Lindi, Bwana Amir
Chembe ambaye shughuli zake kuu ni uhunzi anasema yeye ni mara yake ya kwanza
kushiriki maonesho haya.
Bwana Chembe anasema yeye ameanza
shughuli hizi muda mrefu ila alikuwa anaogopa kushiriki maonesho haya kwa kuwa
yanashirikisha nchi nyingine za Afrika Mashariki.
“Uoga ulinifanya nishindwe kushiriki
maonesho haya kwa muda mrefu sana, lakini namshukuru sana Mungu kwa kunipa
ujasiri wa kuweza kushiriki maonesho haya kwa mwaka huu, hivyo nawaomba
wajasiriamali wasiogope kushiriki”. Bwana Chembe anasisitiza.
Bwana Chembe anasema matarajio yake
katika maonesho haya ni pamoja na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wengine,
kutafuta masoko ya bidhaa zake na pia kufahamiana na wajasiriamali wa nchi
nyingine.
Maonesho haya yanatarajiwa kufunguliwa
rasmi tarehe 5/12/2012 na Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza na yatafungwa
tarehe 9/12/2012.
No comments:
Post a Comment