Thursday, October 18, 2012

Uwanja wa Bukoba kutokamilika kwa wakati-Dkt.Tizeba atoa karipio


 
Massawe akijadiliana jambo na Naibu waziri  Dkt. Charles Tizeba na watendaji wengine walienda kuona hali ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Bukoba.

 Bukoba
SERIKALI imetishia kumsimamisha kazi mkandarasi anayekarabati na kupanua uwanja wa ndege wa Bukoba  kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya sh. bilioni 25 kutokana na kuwa nyuma kwa utekelezaji kwa zaidi ya miezi minne kinyume na mkataba wake.
Tishio hilo limetolewa  jana na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt.Charles Tizeba alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua maendeleo ya ujenzi na upanuzi wa uwanja  wa mjini Bukoba,  pamoja na hali ya bandari za Bukoba na Kemondo.
Alisema” fedha zipo lakini nashangaa kwa nini mkandarasi huyo amechelewa kumaliza ukarabati na ujenzi wa uwanja huo kwa kiwango cha lami, serikali inaweza kusitisha mkataba na mkandarasi huyo”.
“Wajitahidi wabadili ratiba yao ya kazi ili kuweza kukamilisha uwanja huo kwa muda uliopangwa na kuweza kutukabidhi  uwanja wetu kulingana na mkataba , vinginevyo tunaweza kuchukua fedha yao kwa mkandarasi kwani kuna ile fedha anapewa mkandarasi asipokukabidhi mradi kwa wakati tunataka hiyo… tutachukua, na tusipomwona kama hawezi kumaliza mkataba huo kwa wakati tutamwambia toka”alisema
 Na kuongeza kuwa “Sisi tunachotaka ni huduma, hatutaki mabishano yao, hayo ni ya kwao tunachohitaji ni kukabidhiwa mradi wetu kwa wakati”.
Uwanja huo ambao unaofanyiwa ukarabati na upanuzi na kampuni ya CGG  Mecco joint venture, awamu ya pili  kulingana na taarifa ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera ilipangwa kutekelezwa katika mwaka 2010/2011 inahusha kuweka lami na kujenga “building terminal”.
  Awali Mkuu wa Mkoa Kagera, Kanali Fabian Massawe akitoa taarifa kwa Naibu Waziri huyo alilalamikia kucheleshwa kufidiwa wananchi 46 waliobomulewa nyumba zao kupisha unanuzi wa ujenzi wa uwanja wa ndege huo kwani imefikia hatua sasa wanatishia kuandamana na kwamba tayari wananchi wanne wameshalipwa.
Pia alisema inashangaza katika ujenzi wa nyumba ya kumpuzikia wageni hakuna hata chumba maalum cha wageni mashuhuri  jambo alilomwomba Naibu Waziri kulitafakari.
Alisema ujenzi wa uwanja huo ni fursa mojawapo ya kuleta maendeleo katika mkoa wa Kagera.
Hata hivyo, kwa upande wa Mkurugenzi wa ufundi wa Mamlakka wa Viwanja vya ndege nchini (TAA), Bw. White Majura alisema ndani ya mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha kuwa wanamaliza kulipa fidia kwa wote ambao wametathiminiwa ambapo fedha zote za fidia  ni zaidi ya sh. bilioni 1.9.
Alisema tatizo ni kuwa wanapata fedha kwa awamu kutoka serikalini, na wao watawalipwa kwa mfumo huo wa awamu.
Naye Meneja wa uwanja wa ndege wa mjini Bukoba, Julius Murugwana alisema ujenzi na upanuzi wa uwanja huo utakapokamilisha utawezesha ndege kutua uwanjani hapo muda wote na kwamba pia upo mpango wa kujenga uwanja wa kimataifa katika eneo la Omukajunguti wilayani Missenyi mpakani mwa Tanzania na Uganda.
Alisema ujenzi wa nyumba cha kupumzikia wageni hakuna chumba cha wageni mashuhuri wala hakuna kumbi za kuwahudumia na hiyo inatokana na benki kukataa kuhusisha jengo na mkataba.
Hata hivyo alisema serikali na Mamalaka inajipanga ili kuweza kugharamikia ujenzi wa jengo hilo la wageni mashuhuri.
Kwa upande wa makandarasi wanaojenga uwanja huo waliahidi kuongeza kasi ya ujenzi huo ili uweze kukamilika na kuukabidhi.
                                                    #

No comments:

Post a Comment