Friday, October 12, 2012

Kagera watangaza unyanjano wa migomba janga la mkoa, miche zaidi ya mil.1 yaathiriwa ,hupata hasara ya sh. bil.16 kila mwaka


Na Mwandishi wetu, Bukoba
UGONJWA wa migomba ya unyanjano umeubabishia mkoa Kagera hasara ya sh. bilioni 16 kila mwaka, imeelezwa.
Kutokana na hali hiyo mkoa Kagera umetangaza ugonjwa  huo unaoshambulia migomba kuwa ni janga la mkoa.
Hatua hiyo ilifikiwa jana na wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa Kagera kilichofanyika jana mjini hapa na kuhudhuriwa na wadau mbali mbali kutoka taasisi  binafsi na serikali.
Wajumbe hao walisema kutokana na  hasara kubwa  ambayo wakulima wa mkoa huo wameshaupata na wanaendelea kuupata  kutokana na ugonjwa wa unyanjano wa migomba umeathiri uchumi wa mkoa huo.
Akitoa  taarifa ya kuenea kwa ugonjwa huo wa unyanjano , Mshauri wa kilimo mkoani hapa, Bw. Diyonysius Mabugo alisema kutokana na ugonjwa huo umesababisha uzalishaji kushuka kwa asilimika 10 hadi 17 jambo ambalo linahitaji mikakati ya kuudhibiti ikiwa ni pamoja na kutangaza gonjwa hilo kama janga la mkoa.
Bw.Mabugo alisema mavuno ya ndizi umepungua kwa asilimia tatu na uuzaji wa zao hilo pia umepungua kwa asilimia 35 jambo ambalo linahitaji mikakati kabambe ya kupambana nalo.
Alisema kutokana na hali hiyo hata ulaji wa ndizi umepungua kwa silimia 25 huku bei yake ikipanda zaidi hadi asilimia 46 na kusababisha kaya nyingi kupata mlo mmoja kuongezeka hadi asilimia 15 ambapo upungufu wa chakula umetoka asilimia 14 mwaka 2006 hadi 64 kwa mwaka huu.
Akielezea ufahamu wa ugonjwa huo kwa wakazi wa mkoani Kagera ambao uliweza kuonekana kwa mara ya kwanza kwa wakulima wa kijiji cha Kabale tarafa ya Izigo wilayani Muleba Septemba 2005 na kuthibitishwa na wataalam kuwa ni unyanjano Januari 2006 ni asilimia 97.
Alisema pamoja na utafiti kuonesha kuwa ni asilimia 93 ya wanakagera wanaufahamu wa ugonjwa huo Uganda wakiwa ni asilimia 74 na Rwanda asilimia 61 lakini katika utumiaji  wa kanuni bora za kuudhibiti ugonjwa wa Unyanjano Tanzania mkoani Kagera ni asilimia 13,Uganda asilimia 55 na Rwanda ni asilimia 47.
 Alisema changamoto inatokana na kutokuwepo kwa mpango kazi madhubuti wa kupambana na mnyauko bacteria (BXW).
Pia Wakulima hawamilikishwi katika kuandaa mipango ya kudhibiti BXW na mipango ya kudhibiti BXW si endelevu.
 Halikadhalika wakulima ambao mashamba yao hayajashambuliwa hawashituki na siasa mufilisi za kugeuza BXW kuwa mtaji wa kisiasa.
Alisema hadi Juni mwaka huu ugonjwa huo umeshaathiri jumla ya kaya 56,520 katika vijiji 389 kwenye kata 110.
 Pia ugonjwa huo umeathiri jumla ya miche 1,131,192 kwa mwaka huu na mwaka 2011 uliathiri miche ya migomba 596,034
 Hata hivyo, Mkuu wa mkoa Kagera Kanali Fabian Massawe alisema kwa sasa ungonjwa huo ni janga la mkoa ambapo wanasubiri serikali nayo iweze kulitangaza kama janga la taifa, kwani tayari wameshawasiliana na waziri wa Chakula, kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiiza aliyekuwa mkoani hapa.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment