Friday, October 19, 2012

Sheria ndogo zilizotungwa kwa kimombo chanzo cha wananchi kutozitekeleza kikamilifu- Wabunge


Na Theonestina Juma, Bukoba
SHERIA ndogo nyingi za halmashauri za wilaya Mkoani Kagera hazieweki kwa wananchi wengi kutokana na kuwa katika lugha ya kiingereza, imeelezwa.
Aidha kutokana na sheria hizo kuwa katika lugha hiyo ya kigeni ni miongoni  mwa  changamoto zinazojitokeza katika hatua ya utekelezaji wa sheria hizo mkoani hapa.
Hayo yamebainishwa jana (leo) na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogo, Bw. Sylvester Mabumba wakati akitoa taarifa ya majumuisho ya ziara yao mjini hapa  yaliohudhuriwa na baadhi ya watendaji  na Wenyeviti wa halmashauri za mkoani Kagera.
Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo iliziagiza halmashauri zote kuhakikisha zinatafsiri sheria ndogo hizo kuwa katika lugha ya Kiswahili ambayo wananchi wote wanaielewa vyema.
Mbunge Mabumba alisema kulingana na takwimu zilizopo ambazo ni theluthi tatu sawa na asilimia 33 hadi 36 katika sheria za halmashauri za mkoa wa Kagera zilizotungwa ziko katika lugha ya kiingereza.
Alitoa mfano kama wilaya ya Karagwe sheria ndogo 11 sawa na asilimia 36.6 ya sheria ndogo 30 zilizotungwa ziko katika lugha ya kiingereza.
Halikadhalika wilaya ya Ngara sheria nne sawa na asilimia 36.3 kati ya 11 zilizotungwa ziko katika lugha hiyo ambayo asilimia kubwa ya wananchi hawaimudu kabisa.
Hata hivyo, kamati hiyo ilisema kuwa sheria hizo ndogo za halmashauri hazipewi kipaumbele unaostahili ikilinganishwa na sheria zinazotungwa na Bunge, na kwamba wananchi wanauelewa mdogo juu ya umuhimu wa kuzihemu mfano katika suala nzima ya usafi.
“Sheria ndogo zina hadhi na umuhimu kama sheria zilizotungwa na Bunge, hivyo hazina budi kuheshimiwa na makundi yote ya jamii, wakiwemo wanasiasa ambao wamekuwa wakilalamikiwa kushawishi wananchi wasitii sheria ndogo kwa manufaa yao binafsi”alisema.
“Tunawakumbusha na kusiistiza kwamba hakuna aliye juu ya sheria katika nchi hii”aliongeza.
Kwa mantiki hiyo, aliwataka watendaji wa halmashauri za mkoani hapa wabadilike na kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa mujibu wa sheria zilizopo na si kwa mujibu wa viongozi walio juu yao na wanasiasa.
Alisema usimamizi wa sheria unapaswa kutekelezwa na halmashauri zenyewe kwani ni mamlaka zilizopo kisheria.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo ya Bunge itashauriana na serikali kuhusu namna ya bora ya kuwa na mfumo na utaratibu wa kuharakisha utuingwaji wa sheria ndogo za halmashauri zote nchini ili kuondoa usumbufu unaosababishwa na kuchelewa kukamilika kwa sheria hizo.
Alitoa mfano kama wilaya ya Karagwe kuna sheria zilipekwa katika Ofusi ya Waziri Mkuu, Tawala za M ikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kufanyiwa kazi tangu mwaka 2006 hadi leo hazijarudishwa katika halmashauri hiyo.
Hata hivyo alizishauri halsmahauri hizo ziwe na utaratibu wa kuwezesha wanasheria wake kufuatilia na kuhakikisha sheria ndogo zilizopo katika mchakato wa kutungwa zinakamilika kwa wakati ili kurudi kwa ajili ya kuanza kutumika.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment