Friday, October 19, 2012

Kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogo yapigwa butwaa na madai ya Uongozi wa Missenyi kutojua mapato halisi ya uzalishaji wa kiwanda cha sukari cha Kagera

Na Mwandishi Wetu, Bukoba
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya sheria ndogo, imeugiza uongozi wa
halmashauri ya Wilaya ya Missenyi,kufuatilia na kuhakikisha inapata
taarifa sahihi kuhusiana na mapato halisi yanayozalishwa na Kiwanda
cha sukari cha Kagera ili iweze kupata ushuru stahiki.
Agizo hilo limetolewa jana (LEO) na Mwenyekiti wa Kamati
hiyo,Sylvester Mabumba wakati akisoma taarifa ya majumuisho ya ziara
yao mkoani yaliofanyika mjini hapa na kuhudhuriwa na Watendaji na
Wenyeviti wa halmashauri zote za Mkoani hapa.
Alisema hayo kutokana na kamati hiyo kushangazwa na maelezo ya
halmashauri hiyo kuwa inapata ushuru wa huduma (service levy) kutoka
kiwandani hapo bila kuwa na takwimu zinazoiwezesha halmashauri kujua
mapato halisi ya kampuni hiyo.
"Ili ijiridhishe kama mapato wanayopata ni stahiki, ni lazima
halmashauri iendelee kufuatilia na kuhakikisha inapata taarifa sahihi
kuhusiana na mapato halisi yanayozalishwa na kampuni, kamati
haikubaliani na hali hii" alisema katika taarifa hiyo.
Alisema kamati hiyo imegundua kuwa halmashauri nyingi hazipati ushuru
wa huduma kutokana na minara ya mawasiliano ambayo imewekwa na kampuni
za simu za mkononi.
Kutokana na hali hiyo kamati hiyo imeziagiza halmashauri kuhakikisha
zinatunga sheria zitakazoziwezesha kutoza ushuru wa huduma kutoka kwa
kila kampuni ambayo ina minara ya mawasiliano kati halmashauri
husika."
Kila halmashauri ina haki ya kupata ushuru wa huduma kutoka kwa mtu au
kampuni ambayo imewekeza ndani ya mipaka ya ene la halmashauri hiyo si
vinginevyo"alisema.
Aidha halmashauri zote za mkoa Kagera zinatakiwa kutambua kuwa
madhumuni ya kutungwa kwa sheria ndogo hayapo katika kukusanya mapato
tu, bali pia kuwezesha uwepo wa utawala wa sheria katika uendeshaji wa
shughuli za kila siku za halmashauri.
mwisho.

No comments:

Post a Comment