Thursday, October 18, 2012

Ujenzi wa ofisi mpya ya RC Kagera kwa bilioni 11 wagawa wajumbe wa RCC

                                      Pichani chini ni baadhi ya wajumbe wa kikao cha ushauri mkoani Kagera.

Na Theonestina Juma, Bukoba
UJENZI wa ofisi ya kisasa ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera uliotarajiwa kugharimu zaidi ya sh. bilioni 11, umewagawa wajumbe wa kikao cha kamati ya Ushauri ya Mkoa,baadhi yao wakitaka usitishwe kwa muda huku wengine wakitaka uachwe kabisa.
Hayo yamebaikana jana baada ya Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Mkoa Kagera, Kanali Fabian Massawe kutaka kupata msimamo wa wajumbe wa mkutano huo, ambao mwaka 2008 waliridhia kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa katika Kata ya Kahororo nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba kwa gharama ya. bilioni 11,640,043,127.
Katika suala hilo ambalo lilikuwa ni vuta ni kuvute kwa baadhi ya wabunge wa Mkoani Kagera na watendaji wa serikali,wabunge walitaka ujenzi huo uachwe na badala yake ubadilishwe mradi huku watendaji wa serikali na wenyeviti wa halmashauri wakitaka ujenzi usitishwe na utafutwe fedha kwa ajili ya ujenzi huo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe, Bw. Kashunju Rwenyogote alisema kama hakuna fedha wanapaswa kupumzika na kuangalia ni wapi wanaweza kupata fedha lakini si kuacha kabisa ujenzi huo, kutokana na kikao hicho ndicho kilisharidhia kuanza kwa mchakato wa ujenzi huo.
“Hili wazo tulishaliridhia sisi wenyewe, hivyo si jambo nzuri kualiacha, lazima wazo letu liendelezwe”alisema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Bukoba vijijini, Jasson Rweikiza akizungumzia suala hilo, alisema lazima kuwepo na vitu vizuri katika mkoa wa Kagera kama wanavyodhamiria kuendelea kuishi katika jengo la mkoloni kila mara kukarabatiwa na kupakwa rangi imeshapitwa na wakati.
“Lazima tuwe na vitu vizuri kama tulivyodhamiria,jengo la mkoloni linapakwa rangi halifai kwa karne hii, suala la kujenga makao makuu ya mkoa sio jukumu la mkoa ni la serikali kuu”alisema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Asumpta Mshama  uongozi wa mkoa ulioanza ujenzi huo kwa wakati usiofaa wa kujenga jengo la bilioni 11 wakati hakuna kitu kinachoingiza.
Alisema eneo hilo wanatakiwa kuingia ubia na Shirika la nyumba la taifa (N.H.C) kujenga hoteli ya kitalii ili kuweza kuwaingizia kipato.
Aidha alionesha kushangazwa na unjenzi wa nyumba hiyo yenye vyumba 90 hali iliomlazimu kuhoji vyumba vyote hivyo vitawekwa nini.
“Vyumba 90… mnaenda kuweka watu gani? Kujenga ofisi kwa sasa sio wakati wakati, wakati mkoa unamahitaji mengi sana, heri sisi tuna ofisi maeneo mengine hawana”alisema.
Halikadhalika alitoa tahadhari kwa ujenzi wa ofisi hiyo mpya usiwe chanzo cha kuanza kuwachangisha wanakagera fedha kujenga ofisi ya mkuu wa mkoa Kagera, wakati si wakati wake.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Kyerwa, Mhandisi Benedict Kitenga akizungumzia suala hilo alisema hata katika wilaya ya Rorya imejengwa ofisi yenye vyumba 95 hivyo ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa ukiwa na vyumba 90 hakuna tatizo.
Alisema kutokana na mkoa wa Kagera kuwa na rasilimali nyingi hakuna haja ya kuuliza fedha zitatoka wapi, kwani watu wanafedha.
“Vyumba 90 sio tatizo, wala watu wasihoji fedha zitatoka wakati, ni wakati kujengwa ofisi mpya ya Mkuu wa mkoa Kagera, watu wa mkoa huu ni matajiri, tunachotaka sisi ni Mkuu wa mkoa Kagera kuwana ofisi yenye hadhi”alisema.
Kwa upande wa Mkuu  wa wilaya ya Bukoba, Bi. Zipora Pangani alisema kwa sasa ofisi alimo halimtoshi, na kwamba wazo la ujenzi ofisi hilo lilikuwa la msingi na hivyo serikali kuu linatakiwa lichukuwe jukumu la kujenga ofisi hiyo.
Alisema licha ya kuwa kwa sasa fedha zimekosekana, uongozi uweza kuwapatia wawekezaji kiwanja hicho, na wao baadaye watafute kiwanja kingine kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo pindi pesa zitakapopatikana.
Naye Katibu Tawala Msaidizi miundombinu Bw. Seif Hussein mkoa kagera uko katika hadhi kutokana na kupapaka na nchi nchi za Afrika Mashariki.
Alisema imefika wakati sasa, kuwa jengo la kisasa ya mkuu wa mkoa kwani hakuna anayejuwa huenda mkoa Kagera ukawa ni makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Awali katika taarifa hiyo ambayo ilisomwa na Katibu Tawala wa Mkoa Kagera, Mnabila Nassor alisema kuwa jengo  hilo lililobuniwa ni vyumba vya ofisi 90, ni sawa na jengo la Mkuu wa mkoa wa Manyara, likiwa na mgahawa, vyumba vya mikutano pamoja na ukumbi mkubwa wa mikutano wenye uwezo wa kuchukuwa watu 500 kwa wakati mmoja.
Alisema sekretarieti ya mkoa ilianza kukasimia na hatimaye makisio hayo yaliidhinishwa na Bunge katika mwaka wa fedha 2008/2009 ambapo mradi huo ulitarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
Alisema serikali iliahidi kutoa kiasi cha sh. bilioni 3 kila mwaka ambapo utekelezaji wa mradi huo ulipangwa kufanyika katika awamu tatu.
Hata hivyo, sababu kubwa ya kurudishwa tena wazo hilo katika kikao cha RCC,  na uongozi wa mkoa ni kutokana na maoni tofauti yanayotolewa juu ya mradi huo, ambapo Juni mwaka huu Kamati ya kudumu ya Bunge ya hesabu za serikali (PAC) walipotembelea mkoa Kagera waliuagiza  sekretarieti wa mkoa kufikiria kwa makini kuona kama kuna haja ya kuendelea na ujenzi huo.
Pia iliagiza sekretarieti hiyo, ifikirie kupaendeleza mahali hapo kwa njia nyingine ambayo itakuwa faida katika mkoa.
Hatua hiyo ilitokana na kuwepo kwa tatizo la fedha  ambapo badala ya kutumia sh. bilioni 11 katika kujenga ofisi  na badala yake wazielekeze katika kutatua matatizo mengine.
Hadi mwisho, Mkuu wa mkoa huo, Knali Massawe alisema maamuzi yataletwa katika kikao kijacho, kusitisha kwa muda ama kuacha na kumtafuta mwekezaji.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment