Tuesday, April 24, 2012

Wajumbe wa mkutano Mkuu KCU 1990 Ltd wapigwa mbumbuwazi faida sh. milioni 1 kwa mwaka mtaji sh.milioni 86!


Bukoba
WAJUMBE wa mkutano mkuu wa Chama cha Ushirika wa Kagera (KCU) 1990 Ltd wamesikitishwa na mradi wao wa hoteli ya Lake kuzalisha sh. milioni moja tu kwa mwaka wakati mtaji ukiwa ni sh. milioni 86.
Wajumbe hao walionesha kusikitishwa na kiasi hicho, katika Mkutano wa Mkuu wa Mizania ya mwaka 2010/2011 wa Ushirika huo uliofanyika katika hoteli yao ya Coop walionunua kwa zaidi ya sh. milioni 300 takribani miaka mwili iliopita ilioko kando kando ya ziwa Victoria mjini Bukoba.
Wajumbe hao walisema haiwezekani kwa mwaka mtu apate sh. milioni 1,000,300 huku mtaji wake ukiwa ni sh. milioni 86 hivyo inahitaji kuangaliwa suala hilo kwa makini.
Hapa kuna tatizo pale wanauza nyama choma, bia, soda na kuna baadhi ya wageni wanalala humo iweje ipatikanaje kiasi hicho, inamaana kila mwezi wanafanyia faida ya sh. 25,000?alihoji Mjumbe mmoja kutoka katika Chama cha msingi ha Tukutuku wilayani Muleba.
Mjumbe huyo alisema inawatia wasi wasi juu ya kiasi hicho, ambapo alitoa angalizo kwa uongozi wa Ushirika huo, kuangalia kama kweli watendaji wanaofanya kazi hotelini hapo wanafanya kazi kweli ama la.
“Kuna hatari hapa, Wataalam waliowekwa katika mradi huu, wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi au vipi?alihoji tena mjumbe huyo.
Alimtaka Mwenyekiti wa Ushirika huo, Bw. John Binunshu ambaye anatoka katika Chama cha msingi cha Muhutwe Muleba, asimamie kikamilifu mradi wa hoteli ili iweze kuzalisha kile wanachokitegemea na si fedha za wakulima wa kahawa kupotea bure.
Hata hivyo, kwa upande wa Meneja wa (KCU 1990) Ltd Bw. Vedasto Ngaiza akijibu malalamiko ya baadhi ya wajumbe hao alisema faida ndogo iliopatikana katika hoteli hiyo inatokana na mapungufu makubwa ilinayo hoteli hiyo tofauti na hoteli zingine zilizopo mjini Bukoba licha ya kuwa kongwe.
Alisema huduma zinazotolewa katika hoteli hiyo ni hafifu, na hivyo inahitajika kuboreshwa zaidi ili kuweza kushindana na hoteli zingine nyingi zilizoko mjini hapa.
“Kwa sasa Bukoba kuna hoteli nyingi sana, zimeboreshwa  na kuwa katika viwango vya juu, tofauti na hoteli yetu licha ya kuwa kongwe, ambapo fedha ambazo zilitengwa  mwaka jana kwa ajili ya kuiboresha ililazimika zitumike kwenye ujenzi wa nyumba nyingine ambayo pia ikikamilika itakuwa ni kitega uchumi nzuri kwa wakulima”alisema Bw. Ngaiza.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment