Sunday, April 22, 2012

Sijaamini kama nimetoka hai katika ajali hii.

 Hiki ni choo cha shule ya sekondari  ya Omumwani inayomilikiwa na Umoja wa Wazazi Tanzania CCM,Mkoa wa Kagera kilichototia Machi 4, mwaka huu saa 2.00 akiwemo mwanafunzi wa kidato cha tatu, Edwin Adam aliyekuwa akijisaidia.Mtoto Adam aliweza kuokolewa na wapishi wa shule hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa shule.

Bukoba
MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari ya Omumwani ,inayomilikiwa na Umoja wa wazazi Tanzania (CCM) katika Manispaa ya Bukoba,  Edwin Adam (16) amenusurika kufa baada ya choo cha bweni la wanaume kutitia chini akiwa ndani akijisaidia.
Tukio hilo la kusikitisha na la aina yake  tangu mwaka huu uanze , na kuacha simulizi ya kipekee shuleni hapo lilitokea Machi 4, mwaka huu saa mbili asubuhi, ilioambatana na mvua kubwa ilioanza kunyesha mjini hapa kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa 6 mchana.
“Ni kumsuhukuru Mungu, na ni miujiza tu, kama kweli mtu ameweza  kutoka akiwa hai katika tukio hili…, kweli Mungu ni mkubwa kama  mtoto Adam ametoka akiwa hai…..inasikitisha… sijawahi kuona”alisema Mkuu wa shule hiyo, Bw. Modest Byeshulilo.
Akizungumza na gazeti shuleni hapo, mwanafunzi Adam ambaye ni mwenyeji wa wilaya ya Rorya Mkoani Mara, alisema wakati tukio hilo lilitokea, alikwenda chooni akiwa na wanafunzi wenzake, ambapo walijisadia na yeye akabaki kutokana na wiki hiyo nzima alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria  pia na tumbo la kuharisha.
Alisema alikaa takribani dakika tano, ambapo alisikia kitu kama tetemeko ndani ya tundu la choo alilokuwemo, jambo ambalo lilimshutua na hivyo kunyanyuka haraka na kuanza kufunga ‘pensi’ lake, na alipotaka kuondoka tu, ghafla asikia kishindo, cha kitu kizito, mbele yake kumbe ulikuwa ni paa  la jengo la choo hicho ambalo lilidondokea mbele ya  mlango alikokuwa akitaka kutokea na ukazibwa kabisa.
“Nashindwa hata kupata namna ya kuelezea kwa kweli…., choo hakikuwa na hitalafu yoyote kimtazamo wangu,…. lakini ninachokumbuka nikiwa ndani ya choo tundu namba  tatu mkono wa kushoto ukitokea bwenini kwetu, baada ya kubaki peke yangu, nilisikia tundu la choo nilichokuwemo likitikisika  kama vile tetemeko, jambo lililonifanya kuingiliwa na wasi wasi kwani si kawaida na kunyanyuka haraka  na kuanza kufunga ‘pensi’ langu ili niondoke”
“Lakini baada ya kumaliza  nilipoanza tu kuondoka chooni, mara nilisikia kishindo cha kitu mbele ya mlango niliokuwa nikitaka kupitia, bila kufahamu ni nini, mara nilianza kusikia vitu  vigumu vigumu  vikinidondokea  mwilini  kwa nguvu kutoka juu kama vile mawe mawe, mara nikaonekana ninatumbikia shimoni nikalazimika kushikilia nondo , ambalo nalo hatimaye kana kwamba sijui ilikatika….ndipo nikajua kuwa kumbe niko kwenye kifo” alisema mtoto Adam.
Hata hivyo, kutokana  tukio, wapishi waliokuwa karibu na eneo la tukio hilo ndiyo waliwahi kufika hapo kuokoa maisha ya mwanafunzi huyo kwa kutumia ngazi,  kwani kwa wakati huo tayari baadhi ya sehemu ya kuta za choo hicho kilishabomoka na kutitia ndani ya choo hicho  na mtoto huyo akiwa hatarini kufunikwa na kifusi cha ukuta wa choo hicho kilichokuwa kikibomoka na kutumbukia ndani ya choo hicho.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa shule hiyo, Bw. Byeshulilo alisema , katika tukio hilo, miujiza iliofanyika ya kuokoa maisha ya kijana huyo, ni ya kipekee kwani haijulikani jinsi ilivyotokea, ya sehemu ya ukuta wa choo hicho kutanguliwa chini na kufuatiwa na upande wa tundu la choo alichokuwemo mwanafunzi huyo, kuangukia juu ya ukuta huo ndani ya shimo la choo.
“Mhhh…. Anatikisa kichwa, Mungu anamiujiza yake….kwa sasa tungekuwa tunaongea mambo mengi kabisa…. Kitu kilichosaidia ni sehemu ya ukuta wa choo chicho chenye matundu manane kutangulia chini kabla ya tundu alimokuwemo kuanguka, hebu fikiria kama tundu alimokuwemo ama matundu hayo ndiyo yangetangulia halafu yangefuatiwa na ukuta wa choo hiki … ingekuwaje angefunikiwa humo…..”alisema kwa majonzi huku akiwa ameinamisha kichwa chake chini. 
Alisema pamoja na miujiza hiyo, kijana hayo hakuweza kufikia uchafu, licha ya kuwa alipata majeraha sehemu mbali mbali za mwili wake huku akilalamikia maumivui sehemu za kifuani , mgongoni na kichwani kidogo.
Hata hivyo, kutokana na ajali hiyo, ambayo ilitokea wakati Mkuu wa shule hiyo akiwa nyumbani kwake nje kidogo na shuleni hapo, alipigiwa simu ambapo walilazimika kumkimbiza mwanafunzi huyo,  katika kituo cha afya cha Mtakatifu Thereza maarufu kama Bugimbi mjini hapa ulioko kama kilometa mbili kutoka shuleni hapo  ambapo alitibiwa na kurudishwa shuleni.
Ilielezwa shuleni hapo kuwa  hili ni tukio la pili la choo cha shule hiyo kutitia shuleni hapo, ambapo choo cha kwanza kilititia mwaka 2009 ikiwa bado inajengwa .
Hata hivyo choo hicho ambacho ni inasemekana kuwa ni cha msaada kilijengwa  mwaka 2010 na kiongozi  mmoja Jumuiya hiyo ya wazazi Mkonia Kagera, katika uchunguzi wa gazeti hili licha ya kutokuwa  na utaalamu wa masuala ya unjenzi ulibani kujengwa chini ya kiwango kwani hata saruji iliotumika ilikuwa ni kiasi kidogo sana ikizingatiwa kuwa eneo hilo la shule ni sehemu ya udongo wa kichanga na ni chepeche (chemichemi) nyakati za mvua  kama kipindi hiki.
Aidha hata nondo  na wavu zilizotumika katika ujenzi  huo, ni wa kiwango cha chini jambo mbalo moja kwa moja yanaweka rehani  roho za watoto  iwapo serikali haitakuwa na tabia ya kukagua hata ubora wa vyoo vinavyotumiwa na wanafunzi shuleni.
Katika shule hiyo ambayo ni mchanganyiko wasichana kwa wavulana kwa sasa  wavulana hawana choo ambapo wanalazimika kutumia choo cha walimu, huku choo cha dharura kilianza kuchimbwa  siku hiyo hiyo ya tukio.
Mwisho.

 Wadau wa UKIWMI katika Manispaa ya Bukoba  na wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti  wa Tume ya Kudhiti Ukimwi Taifa TACAIDS,Dkt. Fatma Mrisho.
 Mkuu wa mkoa wa kwanza wa Kagera , Bw.Samuel Luangisa akisalimia na Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa sasa Kanali Fabian Massawe.
Baadhi ya nyumba wanamoishi wachimbaji wadogo wa madini aina ya dhahabu walioko katika wilaya ya Biharamulo.Kwa kawaida ya nchi ya Tanzania wachimbaji wadogo ndio wamekuwa wa kwanza kuvumbua eneo lenye madini na kisha wawekezaji hujitokeza kutaka kuweka katika eneo hilo na kuanza kufanya utafiti kwa miaka mingi bila serikali kuambulia kitu chochote.


No comments:

Post a Comment