Na Theonestina Juma, Ngara
ZAIDI ya sh. bilioni 120 zimetumika katika kuboresha mradi wa zao la migomba na usalama wa chakula hapa nchini kwa kipindi cha mwaka 2009/2012 kupitia Shirika la Maendeleo la Belgium technical Cooperation (BTC) kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.
Hayo yamebainishwa jana na Afisa wa miradi BTC Tanzania, Bw. Cranmer Chiduo wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya zao la Migomba mkoani Kagera yaliofanyika katika kitongoji cha Kihanama kijiji na kata ya Rusumo wilayani Ngara.
Alisema kwa kipindi hicho, 2009/2012 BTC imechangia kiasi hicho katika mkoa Kagera na Wilaya ya Kibondo kwa mkoa wa Kigoma mradi ukiwa ni wa kilimo cha migomba ya kisasa aina ya FHIA 17,23,25 na Yangambi (KM5).
Bw. Chiduo alisema kwa upande wa mkoa wa Kagera BTC imechangia kiasi cha sh. bilioni 2.4 katika miradi ya migomba na sh. bilioni 1.5 ni kwa upande wa usalama wa chakula, ambapo mradi huo unatarajiwa kumalizika mwaka 2013.
Naye Mratibu wa mradi huo katika mkoa wa Kagera, kutoka katika kituo cha utafiti Maruku, Bw. Mugenzi Byabachwezi akitoa maelezo juu ya mradi huo wa migomba alisema, lengo lake kuu ni kuongeza kipato na uhakika wa chakula katika mkoa wa Kagera na Wilaya ya Kibondo.
Alisema katika mradi huo, unaofadhiliwa na serikali za Ufalme wa ubelgiji na Tanzania,ufalme wa ubelgji ulitoa sh. bilioni 2.362 na serikali ya Tanzania sh. milioni 262.5 katika kutekeleza mradi huo.
Alisema kituo cha utafiti Maruku kilichopewa jukumu la kuzalisha miche bora na kuwasambazia wakulima , hadi kufika Desemba 31, 2011 miche milioni 2,037,220 zilikwisha sambazwa kwa wakulima wapatao 45,843.
Alisema miche hizo zilisambazwa katika wilaya zote za mkoa wa Kagera na Wilaya ya Kibondo, ambapo wilaya ya Ngara ilisambaziwa miche zaidi ya 45,000 kwa wakulima 6,821 ikifuatiwa na wilaya ya Muleba iliopewa miche 311,484 kwa wakulima 5,568 huku wilaya ya Biharamulo ikisambaziwa miche 30,588 kwa wakulima 674 tu.
Alisema mradi ulilenga kusambaza miche milioni 2.3 kwa kipindi cha miaka mine, ambapo hadi sasa wakulima wamepewa miche milioni 2.1
Alisema mafanikio ya mradi huo ni pamoja na wataalam wa ughani 134 wamepewa mafunzo kutoka kituo cha Maruku na wakulima zaidi ya 8,000 nao wamepata mafunzo kupitia wataalam wa wilaya na kituo cha utafiti wa Maruku.
Alisema kwa sasa migomba si zao la chakula tu bali pia ni ya biashara kutokana na kwa sasa inauzwa ndani na nje ya nchi.
Kuhusu malengo ya sasa ya mradi ni pamoja na kuwa usawambazaji wa miche unaridhisha kwani wakulima wanaweza kuendelea kupeana miche kama ilivyo desturi na wenye uwezo kuendelea kujinunulia ambapo mradi unalenga kutafuta masoko kwa ajili ya ndizi na mazao yake na njia ya kusindika mazao ya migomba.
Alisema kutokana na mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2013, mradi untafuta njia za kuwasaidia wakulima wa migomba ,wachuuzi, wasindikaji na wasafirishaji mbinu na ujuzi wa kufanya vyema zaidi ili waweze kuzalisha kulingana na mahitaji ya soko hasa kuboresha ubora wa mikungu.
Pia kuhakiki masoko kutegemeana na mikungu inavyokomaa na ili yote yaweze kufikiwa, juhudi zinafanyika ili muda wa mradi uongezwe na dalili toka kwa mfadhili zinaonesha kuwa kuna uwezekano wa kuongeza muda ili kuweza kukamilisha hayo kwa ubora zaidi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment