Na Theonestina Juma, Bukoba
MKAZI wa kijiji cha Bumai kitongoji cha Kashekulo kata ya Kishanje katika halamshauri ya Bukoba Mkoani Kagera, Bw.Clophace Kirirukwa (65) amenusurika kuuawa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba yake na watu wasiojulikana kumchomea nyumba zake nne kwa tuhuma ya uchawi.
Kwa mujibu wa habari zilizozifikia blog hii mjini hapa jana asubuhi kutoka kijijini hapo na kuthibitishwa kwa nyakati tofauti na Mtendaji wa kata ya Kishanje Bw. Bruno Mathias na Mwenyekiti wa kijiji cha Bumai Bw. Godwin Kazahura zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Machi 24, saa 2. Usiku.
Bw. Kirirukwa aliyekuwa amejenga katika vitongoji viwili tofauti kijijini hapo, nyumba tatu ziliteketezwa kwa moto katika kitongoji cha Kashekulo na moja katika kitongoji cha Lwanga na ambapo pia alikatiwa migomba yake zaidi ya hekari moja.
Watu hao wasiojulikana wala hata idadi yao inasemekana kuwa ni wakazi wa kitongoji hicho, walichoma nyumba nne za makuti zinazomilikiwa na Bw. Kirirukwa kwa kumtaka ahame kijijini hapo kutokana na tuhuma ya kuwachosha na uchawi na kwamba anafuga mapembe ambao amekuwa akiwatuma kuwasumbua baadhi ya vijana wa kijijini.
Mwenyekiti wa kijiji cha Bumai, Bw. Godwin Kazahura akizungumza na MAJIRA kwa njia ya simu kutoka katika eneo la tukio, alisema kabla hya tukio hilo kutokea, juzi (machi 24, mwaka huu) saa 3 asubuhi baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Kashaigi waliandamana hadi kwa Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Bw.Christopher Nshonga wakimtuhumu Bw. Kirirukwa kuwa amewachosha na vitendo vyake vya uchawi, hivyo wanataka ahame.
Alisema chanzo cha wananchi hao kuandamana inatokana na vijana wawili wa kiume wa marehemu Daudi mkazi wa kitongoji hicho, kuugua muda mrefu bila kupona licha ya kupelekwa katika hospitali zote kubwa za hapa nchini ambazo zimekuwa zikitoa majibu kuwa watoto hao hawana ugonjwa wowote unaowasumbua.
Alisema kati ya vijana hao wawili mmoja ameshahitimu kidato cha nne, na mmoja bado yuko shule ya msingi na kwamba kwa kipindi sasa vijana hao wamefikia ni hatua ya wao ni watu wa kula na kulala tu, huku wakitembelea fimbo kutokana ugonjwa usiojulikana wala kukamatwa na vipimo vya kisayansi.
Mwenyekiti huyo alisema, kutokana na hali hiyo, ililazimika kutafutwa ‘mtaalamu’ mganga wa kienyeji ambaye inasemekana kuwa aliweza kuwapatia dawa ya miti shamba na kuwawezesha watoto hao kuanza kutembea bila kutumia fimbo.
Hata hivyo, kutokana na hilo, katika maandamano hayo ya wananchi, uongozi wa kitongoji hicho ulilazimika kumwita Bw. Karirukwa mbele ya waandamanaji hao kumuulizia juu ya tuhuma zinazodaiwa kwake na wananchi hao, ambapo awali alikana na kudai kuwa yeye hana mapembe na si mchawi.
Alisema kutokana na maelezo yake hayo, wananchi hao walichachamaa ambapo aliendelea kuhojiwa na kukiri kuwa anamiliki mapembe na kuahidi kwa njia ya maandishi kuwa watoto hao angewatibu kwa kuwaondolea mapembe hayo ndani ya siku siku.
Hata hivyo, kabla ya hata siku ya kwanza kwisha wananchi hao waliamua kujichulia sheria mkononi wa kutaka kumteketeza ndani ya nyumba yake, ambapo hata hivyo, wakati wa tukio hilo inasemakana kuwa alihamisha familia yake kwingine na yeye peke yake ndiye alikuwa amebaki hapo nyumbani kwake.
Kwa upande wa Jeshi la polisi mkoani hapa, haliweza kupatikana kuthisha suala hilo, baada ya Kamanda wa polisi Mkoani hapa,Henry Salewi kutopatikana kupitia simu yake ya kiganjani.
Hata hivyo, vitu vilivyotekezwa ndani ya nyumba hizo hazijajulikana wala hata thamani ya uharibufu wa vitu vyake vyote.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment