Tuesday, April 10, 2012

Misa ya mazishi ya Kanumba yanaendelea katika ukumbi wa Leaders

Kamati ya mazishi ya msanii Steven Charles Kanumba   wametoa taarifa ya ratiba kwa vyombo vya habari ya utaratibu wa kumpeleka katika nyumba ya milele msanii huyo ambaye alikufa Ijumaa Aprili saba usiku.
Msanii huyo ambaye atazikwa muda mchache zijazo katika makaburi ya Kinondoni amefanyiwa utaratibu ambao utamwezesha kila mwenye kuhitaji kushiriki mazishi hayo kuweza kumuaga.
Mwili wa marehemu  umechukuliwa leo asubuhi kwa msafara kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili saa 2.30 asubuhi. Umepitishwa barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.
Mamia ya watu wamejitokeza kwa wingi kuanzia saa mbili asubuhi kumuaga katika barabara ambazo  amepitishwa .
Saa 3.30 asubuhi mwili wa Kanumba utapokelewa viwanja vya Leaders ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk Mohamed Gharib Bilal.
 Saa 4.00 itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo inakadiriwa kuchukua dakika 60 na saa 5 itakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.
Saa 6.00 mchana ratriba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9.00 alasiri na baada ya hapo utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka makaburi ya Kinondoni.Msafara huo utapitia barabara ya Tunisia, utakatisha barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini.
Sa 10.00 maziko yatafanyika kwa kufuata taratibu za imani ya marehemu.
 Kamati hiyo ya  mazishi inayoongozwa na Gabriel Mtitu imewaomba wananchi watakohudhuria shughuli hiyo kwenda na maua ili kumuaga kwa heshima.
Ibada na maziko vitafanyika kadri ya imani ya marehem.
Hadi sasa tayari baadhi ya watu wameanza kutoa salaam za mwisho ambapo baadhi ya watu wanaanguka na kuzimia kutokana na kuona jeneza la marehemu.

No comments:

Post a Comment