Wednesday, April 4, 2012

"Padri apigwa butwaa kumaliza miaka sita bila kuendesha misa ya mazishi"

Na Theonestina Juma, Rorya 
PAROKO wa Kanisa Katoliki parokia ya Ingri  Jimbo la Musoma Mkoani Mara, Romanus Ciupaka ameonesha kusikitishwa na waumini wa kanisa hilo  kupenda kufunga ndoa za ng’ombe badala ya kanisani.
Padri huyo alisema hayo hivi karibuni wakati akihubiri misa takatifu ya mazishi ya mzee Alloyce Amworo (90) yalioanzia parokiani hapo na kisha kumalizikia kijijini kwake Randa kata ya Kigunga wilayani humo.
Paroko Ciupaka alisema waumini wa parokia hiyo hasa wa kigango cha Randa wamekalia mambo ya majungu ikiwa pamoja na kumpiga vita jambo linalotokana na ukweli analozimzungumza juu yao, wa kutopenda kujishughulisha, kupenda kufunga ndoa za mifugo yaani kulipana mahari nyingi bila hata kufunga ndoa takatifu kanisani.
“Mimi nitaendelea kusema ukweli tu hata kama baadhi ya waumini wa kanisa hili wananichukia, mnapenda ndoa za mifugo tu, kwa nini hamtaki kufunga ndoa takatifu za kanisani…., huu ni mwaka wangu wa sita katika Parokia hii, hakuna ndoa yoyote kutoka katika Kigango cha Randa ambacho kimeshafungwa ndani ya kanisa hii, ina maana mnafunga ndoa za ng’ombe pekee”alisema paroko huyo.
Alisema pamoja na tatizo la ndoa pia tangu apangiwe katika parokia hiyo, misa takatifu  ya mazishi aliosoma kanisani hapo kwa mara ya kwanza ni hiyo ya Mzee Amworo ndani ya miaka sita ya maisha yake parokiani hapo jambo ambalo alionesha kushangazwa na tabia ya waumini wa parokia hasa Kigango cha Randa.
Alisema waumini wengi wanapenda mazishi ya kipagani, huku katika kigango cha Randa wakiwa hawana hata moyo wa kijitolea zaidi ya kukaa kwenye vijiwe kupiga umbea.
Alisema katika Kigango cha Randa ambacho Mzee huyo alijitolea kwa hali na mali katika harakati za ujenzi wake, kati ya miaka ya  1990 hadi 1994 hadi sasa wanaumini hao wanakalia mawe badala ya mabenchi jambo linachongiwa kutokuwa na moyo wa kijitolea.
Halidahalika hata watoto wanaosoma komunio ya kwanza takribani miaka miwili sasa hakuna hata mmoja suala linalotakiwa kuangaliwa kwa makini kiini cha tatizo  hilo ni nini.
Hata hivyo, paroko huyo alimwagia pongezi marehemu  Amworo kuishi ndani ya ndoa yake tangu mwaka 1952 hadi mauti yalipomkuta, ambapo ameacha mjane, watoto watano, wanne wakiwa wakiume mmoja wa kike, wajukuu 13 na vitukuu watano.
Baaadhi ya aombolezaji waliohudhuria misa ya mazishi hayo kanisani hapo, hasa kutoka nje ya mkoa wa Mara walisikika wakisifia  mahubiri ya Paroko huyo, kwa kuzungumzia ukweli, kwani asilimia kubwa ya waumini hawataki kuchanga fedha kwa ajili ya maendeleo ya kanisa lao zaidi ya kubaki kutaka kuchangiwa na kufanyiwa kila kitu.
Mmoja wa waombolezaji hao, aliyejitambulisha kwa jina la Bi.Happness Odira ambaye ni muumini wa Parokia ya Karoli Lwanga Jijini Dar Es Salaam alisema, pamoja na kuonekana wazi baadhi ya waumini wa parokia hiyo kutompenda Padri huyo ambaye ni Mzungu lakini ukweli unauma na unabaki pale pale kutokana na asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo kupenda kuoa wake wengi.
“Unajua asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hili, wanapenda kuoa wake wengi, na imani ya kanisa Katoliki, inataka ndoa ya mke mmoja, sasa hii ni tatizo kubwa…. , mtu akipata ng’ombe ama ameachiwa urithi wa mifungo anaona bora aongeze mke badala ya kushughulikia kujenga imani katika familia yake, na pia watu wengi hawapendi masuala ya michango ya makanisani zaidi ya harusi”alisema. 
Mwisho.

No comments:

Post a Comment